The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma 43

0

500000-dollar-billsILIPOISHIA…
Inspekta Masala yupo katika kazi maalum kwa miaka minne na nusu akiwasaka wanawake wawili hatari; Dk. Viola na pacha wake Vanessa ambao wanatafutwa kwa mauaji ya watu wengi duniani, kwanza waliangusha ndege na kuua abiria wote na kabla ya hapo walikuwa wakiwaibia watu figo katika miili yao na kuwazika chini ya ardhi kwenye nyumba ambayo Dk. Viola alikuwa akiishi.

Mifupa na mabaki ya miili ya watu waliowaua ilifukuliwa kutoka kwenye handaki kubwa ambako Dk. Viola alilijenga chini ya nyumba yake hiyo, dunia nzima ikashtuka kwamba watu hao hawakuwa Wasamaria wema kama walivyokuwa wakijionyesha mbele ya jamii, ndiyo maana CIA, Scotland Yard na Interpol wakaingia kazini kuwasaka bila mafanikio.

Jambo ambalo Dk. Viola na Vanessa walifanya baada ya kugundua wanasakwa kwa udi na uvumba ni kukimbilia nchini Thailand ambako bingwa wa upasuaji wa urembo na plastiki, Dk. Jeremy, aliwafanyia mabadiliko makubwa ya sura zao na kuwafanya waonekane wazee wa Kijapan na wakapatiwa hati za kusafiria zenye majina ya Bw. Hui na Chu.

Baada ya hapo wakarejea nchini Tanzania kama wawekezaji, wakanunua kisiwa cha Bongoyo na kuamua kujenga mji wa kisasa sawasawa na Dubai kwa gharama ya dola milioni mia sita, kazi hiyo ikakamilika kwa miaka minne bila serikali ya Tanzania kufahamu ni kwamba watu hao hawakuwa wazee wa Kijapan, bali ni wanawake wa Kitanzania waliobadilisha sura zao ili kujificha wasikutwe na mkono wa sheria.

Katika mazingira ya kutatanisha, wapelelezi wote waliokuwa wakishirikiana na Inspekta Masala wanakufa kifo cha kufanana wakiwa na sindano ya heroine kwenye mishipa na chupa ya Vodka!

Hilo linamfanya Inspekta Masala aamini kuna mtu anawaua ili kukwamisha upelelezi, anahitaji kitu kimoja tu ili aweze kuwapata Dk. Viola na mwenzake, kukutana na Dk. Jeremy aliyewafanyia upasuaji na kumshawishi ampe picha za sura walizozipata baada ya upasuaji, jambo ambalo huko nyuma Dk. Jeremy aliwahi kukataa.

Masala ameamua kwenda nyumbani kwa Dk. Jeremy, huko anakutana na mazishi, Dk. Jeremy amekufa kifo kama walichokufa wapelelezi jambo linaloashiria kwamba mtu pekee aliyebaki hai ni Inspekta Masala, akiwa hapo anakutana na dumejike aitwaye Jen, ambaye amemwambia anazo picha za Viola na nduguye baada ya kufanyiwa upasuaji, Inspekta Masala amepatwa na mshituko wa ghafla pamoja na furaha kubwa.Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…SONGA NAYO…

Wawekezaji wa Kijapan, Jonathan Magafu na Andrew Kisanji, waliketi juu ya jengo refu walilolijenga kwenye kisiwa cha Bongoyo, wakiangalia kwa chini namna boti zilivyosomba watu kwenda na kutoka kisiwani ambako sasa paliitwa Dar es Salaam Disney. Maelfu ya watu walimiminika kwenda kwenye kisiwa hicho kula raha ambazo hazikupatikana sehemu nyingine yoyote ya Jiji la Dar es Salaam na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Makadirio ya chini ya watu waliokwenda kisiwani humo hayakupungua elfu ishirini kwa siku na wote walilipa si chini ya shilingi elfu kumi bila kujali ni mtoto au mtu mzima, fedha iliyoingia mfukoni mwa wawekezaji hao wenye majina mengi waliyowahi kutumia maishani mwao kiasi cha mengine kuyasahau, haikuwa chini ya shilingi za Kitanzania milioni mia mbili kwa siku, hakika utajiri ulikuwa ukiingia mifukoni kwao kwa kasi.

Walikuwa wamefanya uwezekaji mkubwa lakini uhakika wa kurejesha fedha zao ulikuwa ni mkubwa mno, watu kutoka nchi mbalimbali za dunia walifika nchini Tanzania kuuangalia mradi huo na wengine hata kunakili ili wakaujenge katika nchi zao, Jonathan Magafu na Andrew Kisanji wakawa maarufu duniani kiasi cha kuhojiwa na vyombo mbalimbali vya habari bila mtu kugundua kwamba wao ndiyo walikuwa Dk. Viola na Vanessa ambao dunia ilikuwa ikiwasaka kwa udi na uvumba.

“Ile kazi ya kule Thailand inaendeleaje?”
“Nilipewa taarifa kwamba wapelelezi wote wamekwishakufa, Dk. Jeremy naye pia ameuawa usiku wa kuamkia leo!”

“Na Inspekta Masala ameuawa?” Dk. Viola aliuliza.
“Yeye bado, ila wanammalizia leo usiku baada ya mazishi, mipango inakwenda vizuri!”
“Waambie wammalizie haraka, nataka kuishi kwa amani, huyo mtu akiendelea kuwa hai utajiri wetu wote hauna maana, lazima tutaingia mikononi mwa sheria, usione yuko kimya lazima anatusaka kwa gharama yoyote!”

“Nitawasisitizia!” Vanessa alijibu.
Mpaka wakati huo waliishi kwa amani mno, hakuna mtu yeyote aliyewatilia mashaka, hawakumsogeza mtu karibu kabisa na maisha yao, waliishi peke yao kwa hofu ya kugunduliwa! Hakuna siku hata moja walivaa nguo za mikono mifupi au kaptura wakiogopa ngozi za mikono na miguu yao kuonekana mbele za watu.
***
“Yes I have photos in my album at home!” (Ndiyo ninazo picha hizo kwenye albamu yangu nyumbani!)
“Are you sure?” (Una uhakika?)
“Yes, do you doubt?” (Ndiyo, una mashaka?)

“No!” (Hapana) Inspekta Masala aliitikia kumwondoa wasiwasi mtu huyo ingawa kweli alikuwa na mashaka kama kilichokuwa kikisemwa ni ukweli usije kuwa ni mpango wa kumwingiza matatizoni.
“Do you need them?” (Unazihitaji?)
“Yes, I can pay you anything to have those photos!” (Ndiyo, naweza kulipa chochote ili kuzipata picha hizo.)
“I don’t need money!” (Sihitaji fedha.)
“What do you need?” (Unahitaji nini?)
“I need you!” (Nakuhitaji wewe)

“What do you mean?” (Unamaanisha nini?)
“You are not a little kid, you know what I mean!” (Wewe siyo mtoto mdogo, unajua ninachomaanisha!)
“Do you mean you want to exchange those photos with sex?” (Unamaanisha unataka tubadilishane picha hizo na ngono?)

“Absolutely!” (Haswa!)
“Me? Having sex with a transsexual? Never!” (Mimi? Nifanye ngono na mtu aliyebadilisha jinsia? Kamwe haiwezekani!)
“Ha, ha, ha, ha! Then you don’t need the photos!” (Ha, ha, ha, ha! Basi picha huzihitaji!)
“I need them, but not in exchange for sex, tell me any amount of money, I will pay!” (Nazihitaji lakini si kwa kubadilishana na ngono, niambie kiasi chochote cha fedha nitalipa!)
“I did not choose to be a transsexual because I am poor, I am very rich, I did it because I needed it!” (Sikuchagua kubadilisha jinsi kwa sababu ni maskini, mimi ni tajiri, nilifanya hivyo tu kwa sababu nilihitaji!”

“So?” (Kwa hiyo?) Inspekta Masala aliuliza akiwa katika mshangao bado, ni kweli alizihitaji sana hizo picha lakini hakuwa tayari kufanya ngono na mwanaume huyo aliyebadilisha jinsia.
“After the funeral come with me to my house, after a wonder sex, I will give them to you!” (Baada ya mazishi twende nyumbani kwangu, baada ya ngono safi, nitakupatia hizo picha!)

Inspekta Masala alibaki kimya kama dakika tano bila kuongea chochote akitafakari juu ya kazi aliyokuwa nayo ya kuwasaka Dk. Viola na nduguye Vanessa, kwa miaka mingi alikuwa ameteseka akiwa amepoteza maisha ya wapelelezi wenzake wanne, lakini sasa mbele yake alikuwepo mtu mwenye picha za watu aliokuwa akiwasaka ambao kwa kuwafahamu sura zao tu angejua walipo na angekwenda moja kwa moja na kuwakamata, fikra hizo zilimfikisha mahali akajikuta anaamua kuachana na msimamo wake.
“I am ready!” (Niko tayari!)

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi.

Leave A Reply