The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma 46

0

6095921-Avarice-businessman-with-money-man-or-devil-holding-dollars-in-display-of-greed-in-hell-fire-A-Deadl-Stock-PhotoINSPEKTA Masala ametua nchini Tanzania kuwafuatilia Dk Viola na Vanessa, mabilionea wasio na huruma, waliojipatia utajiri wao kwa kuua watu wengi! Dunia inawatafuta watu hao kwa udi na uvumba lakini wamejificha jijini Dar es Salaam kama wawekezaji wakiwa wamebadilisha sura na majina yao, hivi sasa wanaonekana ni wazee wa Kijapan wakitumia majina ya Jonathan Magafu na Andrew Kisanji!

Kwa muonekano wao si rahisi kuamini kwamba ni wanawake, bali wazee wa Kijapan wanaoheshimika kama wawekezaji maarufu nchini Tanzania na serikali inawaheshimu bila kuelewa ni wauaji hatari! Inspekta Masala amefikia kwenye Hoteli ya New Africa na kupanga chumba namba 215, kichwani mwake anatafakari jinsi ya kuifanya kazi iliyo mbele.Je, nini kitafuata?SONGA NAYO…

KILA kitu kilikuwa bayana kuwa Inspekta Masala alikuwa mita chache tu kuwafikia watu hatari aliowatafuta kwa muda mrefu bila mafanikio, moyoni mwake alikiri Dk Viola na Vanessa walikuwa ni watu machachari waliozijua mbinu za kujificha kuliko wahalifu wote aliowahi kufanya kazi ya kuwasaka, hata hivyo ujanja wao ulikuwa umefika mwisho kwani saa chache tu kuanzia muda huo, sababu alishajua mahali walipo na majina waliyotumia, angewatia mkononi mwake na huo ndiyo ungekuwa mwisho wa stori.

“Yaani Serikali ya Tanzania imeshindwa kabisa kufahamu kwamba hao kina Jonathan Magafu na Andrew Kisanji, wenye sura za Kijapani waliochukua uraia wa Tanzania walikuwa ndiyo Dk Viola na Vanessa? Siku nikiwawakilisha kwao hawataamini kwamba watu waliowakaribisha kama wawekezaji, walikuwa ni wauaji hatari walioua Watanzania wengi pamoja na watu wa mataifa mbalimbali, itakuwa mshtuko wa maisha!” aliwaza Inspekta Masala.

Muda huohuo akachukua kompyuta yake mpakato na kwenda kwenye Mtandao wa Google ambako aliandika majina ya Vanessa na Dk Viola kisha kubonyeza sehemu iliyoandikwa picha, zikatokea picha zao wakiwa na viongozi mbalimbali wa serikali na pia majengo mbalimbali ya mradi wa mji mpya wa Dar es Salaam uliokuwepo kwenye Kisiwa cha Bongoyo, mitandao yote ilijaa sifa zao, bila mtu kuelewa kwamba watu hao ndiyo waliodondosha ndege na kuua watu wote waliokuwemo ndani yake ili tu walipwe fidia ya bima ya dola milioni mia sita na ishirini.

Fikra hizo zilimpa Inspekta Masala hasira, hasa alipofikiria wapelelezi wake waliouawa na watu hao katika Jiji la Bangkok, hata yeye mwenyewe asingetoroshwa lazima angeuawa, hiyo ilimfanya awe na hamu kubwa wa kuwakamata haraka iwezekanavyo na kama ingebidi angewaua na kuwasilisha maiti zao mbele ya waliomtuma kazi.
“They have to die, it won’t be easy to catch them!”(Lazima wafe, haitakuwa rahisi kuwakamata!) aliwaza Inspekta Masala.

Mara moja alichukua kitabu chake kidogo cha kumbukumbu na kuanza kuchora ramani ya ambacho angekifanya mpaka kuwakamata, alielewa wazi kabisa zoezi hilo lilitakiwa lifanyike kwa umakini wa hali ya juu, kosa moja dogo tu lingesababisha Dk Viola na mwenzake kufahamu kwamba alikuwepo katika Jiji la Dar es Salaam akitumia jina la Profesa Abdulkarim Rahim, kufahamika tu hivyo kungemaanisha kifo, asingeweza kuukwepa mkono wao kwa jinsi walivyokuwa na ushawishi mkubwa nchini Tanzania.
“Nitajifanya mteja wa kununua moja ya nyumba zao, kama nikifanikiwa tu kuwa nao karibu nitawateka na baadaye kuwapigia simu polisi wa Tanzania ambao sina uhakika kabisa kama wanaweza kunisaidia, kikubwa itabidi niombe msaada haraka sana kutoka Washington, wafike hapa watu wenye uwezo wa kunisaidia!” aliwaza Inspekta Masala akichora kwenye karatasi yake jinsi ambavyo angetekeleza zoezi la kuwakamata.

Kitu cha kwanza alichokifanya ni kupiga simu kwa Mkurugenzi Msaidizi wa CIA bwana John Captain akimtaarifu juu ya mafanikio aliyoyapata tangu aingie nchini Tanzania, kwamba alishajua mahali Dk Viola na nduguye Vanessa walipokuwa, wakitumia majina ya bandia waliyoyapata baada ya kupewa uraia wa Tanzania.
“Kweli?”
“Kabisa.”

“Wapo?”
“Wapo ni wawekezaji hapa Dar es Salaam.”
“Sasa tukusaidieje?”

“Nahitaji watu wengine kama kumi hivi, wafike hapa ili tuweze kuwakamata kwa urahisi maana wanaushawishi mkubwa mno, tukitumia jeshi la polisi la hapa hatutafanikiwa, hivyo basi naomba mnitumie wasaidizi wenye uwezo, ikiwezekana niombe kitu!”
“Kitu gani?”

“Kuna uwezekano wa kupata ndege binafsi ambayo watakuja nayo mpaka hapa, ili tukishawakamata tu ni kuwapakia moja kwa moja na kusafiri nao kuja Washington, huo utakuwa ni ushindi mkubwa!”

“Hilo linawezekana na litafanyika mara moja.”
“Basi nakuomba ufanye hivyo mkuu kabla mambo hayajaharibika, maana hawa jamaa wakishtuka tu kidogo, nitakuwa marehemu!”
“Wanaondoka hapa mara moja baada ya kukata simu na watakuwa hapo Dar es Salaam saa ishirini na nne kuanzia sasa.”
“Saa moja na nusu kesho.”
“Ndiyo.”

“Basi mimi kesho asubuhi nitakwenda huko kisiwani angalau nianze utaratibu wa mwanzo wa kukutana nao kama mteja wa nyumba!”
“Una uhakika hawatakukumbuka?”

“Nitajibadilisha vya kutosha, nikivaa kofia na miwani pamoja na kubandika mustachi juu ya mdomo wangu, haitakuwa rahisi kwao kunikumbuka hata kama wamewahi kuona picha yangu!”
“Kuwa makini lakini.”
“Nitafanya hivyo.”

Simu ikakatwa, Inspekta Masala akabaki amejilaza kitandani akitafakari juu ya kazi iliyokuwa mbele, maneno ya bosi wake kwamba “una uhakika hawatakukumbuka?” yalisumbua ubongo wake, hata hivyo akajipa moyo na kusema haikuwa rahisi kwake kutambulika kirahisi akivaa kama alivyopanga, hakupata usingizi kabisa mpaka asubuhi kulipokucha na kufanya kitu kimoja tu; kujiandaa kwa ajili ya kuondoka kwenda kisiwani Bongoyo kichwani mwake akijua lazima jioni ya siku hiyo ndege ingefika ikiwa na wasaidizi wengine.

Haikuwa kazi ngumu kwake kufika kisiwani Bongoyo, teksi ilimfikisha hadi kivukoni saa mbili na nusu asubuhi akapanda boti iliyompeleka moja kwa moja. Ilikuwa ni siku ya Jumapili, watu wengi walikuwa wakienda kisiwani huko kupumzika na kula mwisho wao wa wiki, ndani ya boti alikuwa kimya peke yake akijiuliza maswali mengi na kutafuta majibu, mengine aliyapata na mengine yaliendelea kuwa maswali mpaka anashuka kwenye boti na kushangazwa na uzuri wa kisiwa.

“Walipata fedha za haramu lakini wanawake hawa walizitumia kufanya jambo la maana, hii ni kama Dubai au Hongkong ya Afrika, pamoja na hayo haihalalishi kile walichokifanya, lazima niwafikishe mbele ya sheria, waliua watu wengi mno!” aliwaza Inspekta Masala akipitapita mitaani, haikuwa rahisi hata kidogo kumtambua kwa jinsi alivyojibadilisha.

“Samahani dada,” alimwambia binti mmoja aliyekuwa akipishana naye.
“Ndiyo kaka.”
“Unafahamu ofisini kwa matajiri wa kisiwa hiki?”
“Unamaanisha Jonathan na Andrew, wale Wajapan?”
“Ndiyo.”

“Nenda mbele kama mita mia mbili hivi, utakutana na barabara inayoitwa Frank Mbilinyi, kata kulia, kisha tembea kama mita hamsini utakuta jengo lao kubwa la vioo tupu, hapo ndipo ofisini kwao.”
“Ahsante sana.”

Inspekta Masala huku akisikia wimbi dogo la hofu, kiunoni mwake akiwa hana bastola yake sababu siku hiyo hakuwa na mpango wa kumteka mtu yeyote, zaidi ya kujifunza jinsi ya kuwafikia na kuwakamata wabaya wake, alitembea akifuata maelekezo aliyopewa mpaka akafika mbele ya jengo la mahakama, refu la vioo na kuzama ndani hadi mapokezi.

“Naweza kuwaona mzee Jonathan Magafu na Andrew Kisanji?”
“Wewe ni nani?” aliulizwa swali na Inspekta akatoa kitambulisho chake kilichomtambulisha kwa jina la Profesa Abdulkarimu Rahim, mtaalam wa mambo ya mazingira kutoka Marekani.
“Yaani kwa ulivyovaa hiyo kanzu mtu hawezi kuamini umetoka Marekani na unaongea Kiswahili kizuri.”
“Mimi ni Mbongo ila nimeishi Marekani kwa muda mrefu na huko ndiko ninakofanya kazi.”

“Karibu sana, shida yako?”
“Nataka kununua nyumba.”
“Watafurahi sana kukuona maana wanatafuta wateja wa nyumba zao.”
“Basi mimi ni mmoja wao.”
“Subiri nimpigie Katibu Muhtasi wao!” aliongea dada huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Suzana.

Dakika tano baadaye baada ya maongezi kwenye simu, alikata simu na kunyanyuka kitini akimwomba Profesa Abdulkarim amfuate, wote wawili wakatembea mpaka kwenye lifti ambako waliingia na Suzana akabonyeza kitufe namba 14, kuonyesha kwamba lifti ilitakiwa itii amri ya kuwapeleka ghorofa namba hiyo kulikokuwa na ofisi za Dk Viola na Vanessa ambao kwa Tanzania walijulikana kama Jonathan na Andrew, wazee wa Kijapan.

Kadri lifti ilivyozidi kupanda juu ndivyo jasho jembamba lilivyozidi kumtoka Inspekta Masala mgongoni, kwa mara ya kwanza tangu afanye kazi ya upelelezi, alihisi hofu ikimgubika.
“Ningejua ningechukua bastola yangu maana hapa hawana hata mashine za kukagua, hivi ilivyo ni kama najipeleka kwenye mdomo wa Mamba!” aliwaza.
Walipofika ghorofa ya kumi na nne walishuka na kuingia ofisini kwa Jonathan na Andrew, Katibu Muhtasi alikuwa akiwasubiri, mara moja akawaongoza kuingia chumba cha mkutano ambako Inspekta Masala aliachwa peke yake akiwasubiri wenyeji Jonathan na Andrew ili wajadiliane kuuziana nyumba. Haukupita muda mrefu sana, mlango ukafunguliwa na wakaingia wazee wawili wa Kijapan.
“Karibu sana, tumeambiwa unataka kununua nyumba?”
“Ndiyo.”

“Sura yako siyo ngeni, ni kama tumewahi kukutana?”
“Hapana, mimi ni mara ya kwanza kufika hapa.”
“Una kitambulisho?”
“Hapana nina kadi tu.”
“Hebu.”

Inspekta Masala akachomoa kadi moja na kumkabidhi Jonathan, akaanza kuisoma kwa sauti ya juu huku akionyesha wasiwasi wa wazi kabisa, mwisho alipomaliza kuisoma kadi hiyo alimwomba Inspekta Masala atoe kofi na miwani ili waongee vizuri, Inspekta akasita, maana kufanya hivyo kulikuwa ni kuhatarisha maisha yake.
“Vua bwana!” Jonathan aliamuru.

JE, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

Leave A Reply