The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma 47

0

100-dollar-billKWA kutumia taaluma zao, Dk Viola na Vanessa wakiwa na tamaa ya utajiri, walifanya dhambi kubwa ya kuua watu ili tu wapate fedha, Dk Viola aliwafanyia watu upasuaji usio wa lazima na kuwaibia figo zao ambazo aliziuza kwa matajiri waliokuwa na matatizo makubwa waliohitaji figo za kupandikizwa.

Akiwa Mhandisi wa Ndege wa Shirika la Brito Africa Airline nchini Uingereza, Vanessa alishirikiana na nduguye wakawapakia watoto yatima 62 kwenye ndege ya shirika hilo ambao Viola aliwalea kwenye kituo chake cha kulea watoto yatima kwa lengo la kuwasafirisha kwenda nchini Uingereza, watoto hao na abiria wengine wengi walikufa kwenye ajali ya ndege ambayo Vanessa aliisababisha, lengo likiwa ni kujipatia malipo ya bima ya watoto wote 62.

Kabla ya ajali hiyo kutokea, Dk Viola alikuwa amewawekea bima watoto wote 62 na yeye kujitaja kama mrithi wa malipo yao ikiwa ajali yoyote ingewapata, vifo vya watoto hao katika ndege vilimfanya Dk Viola alipwe dola za Kimarekani milioni 640, huo ulikuwa ni utajiri mkubwa, alipochanganya na fedha alizokusanya kabla, alifikia daraja la ubilionea wa dola.

Uchunguzi wa ajali hiyo ulianza kufanyika, walipogundua kuna ufuatiliaji, wakiwa nchini Tanzania, Dk Viola na Vanessa waliamua kukimbilia Bangkok, Thailand ambako walibadilisha sura zao na kufanana na wazee wa Kijapan, ndipo wakarejea Tanzania kama wawekezaji na kununua Kisiwa cha Bongoyo ambako walijenga mji wa kisasa, hakuna mtu yeyote nchini Tanzania aliyewatilia shaka.

Kazi yao ikawa ni kuua wapelelezi wote waliowafuatilia, akawa amebaki mmoja ambaye ni Inspekta Masala, naye wamemkamata na kumweka ndani ya gari huko Goba nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam na kutega bomu ambalo lililipuka baada ya saa moja.

Wapelelezi zaidi aliowaomba Inspekta Masala kutoka Washington DC, wamefika eneo la tukio wakiwa na baadhi ya wapelelezi wa Tanzania wakiongozwa na DCI Msaidizi Kamishna Mwangomole na kushuhudia gari likilipuka, wakajua Inspekta Masala amekufa.

Mbele kidogo baada ya kuondoka eneo hilo, gari yao ilikuta kizuizi, wakashushwa na kutekwa! Waliowateka ni vijana wa Dk Viola na nduguye Vanessa ambao wamepewa maelekezo ya kuwapeleka ghalani ambako watawadumbukiza kwenye mapipa ya tindikali.Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

MPELELEZI Donald Crish, Kamishna Mwangomole pamoja na vijana wote walikuwa wamerundikwa na kulaliana ndani ya gari aina ya Land Cruiser Pickup chini ya ulinzi mkali, SMG zikiwa zimewalenga na wakati mwingine kugusa vichwa vyao huku wakitishiwa kwamba yeyote ambaye angeleta vurugu, kichwa chake kingesambaratishwa kwa risasi.

“Whoever will make noise, for sure he will be dead in second!” (Yeyote atakayepiga kelele atakuwa amekufa ndani ya sekunde!) ilikuwa ni sauti ya Jinks, kiongozi wa vijana wa Dk Viola na Vanessa, alionekana kabisa ni mtu asiyekuwa na huruma.

Safari iliendelea kuelekea mjini, magari yakipita maeneo ya Mbezi, Mwenge, Sayansi, Victoria, Morocco moja kwa moja hadi yakafika Posta Mpya na baadaye Kivukoni ambako boti ilikuwepo kuwasubiri. Mwangomole na wapelelezi wake wote wakiwemo Wamarekani walikuwa kimya, kila mmoja akijiona mjinga kwa jinsi walivyokamatwa kirahisi.

Gari liliingizwa kwenye boti iliyokuwa imewekwa tayari ikiwasubiri na safari kuelekea kisiwani Bongoyo ikaanza tena kwa kasi, walipofika upande wa pili gari liliendeshwa na kwenda moja kwa moja hadi ghalani ambako walikuwa wameelekezwa kuwapeleka mateka wao, milango ikafunguliwa na wakashushwa na kuingizwa ndani wakiwa chini ya ulinzi, mikono imefungwa na pia macho yamezibwa kwa vitambaa vyeusi.

“Sit down! Sit down! (Kaeni chini! Kaeni chini!) Jinks alitamka maneno hayo na wote wakajibwaga chini kama mizigo.

Haraka Jinks akachukua simu yake na kubonyeza namba kadhaa kisha kuanza kuongea na mtu ambaye kila mmoja alifahamu kwamba ni bosi wake kwa jinsi alivyoongea kwa unyenyekevu akipokea maelekezo.

“Ndiyo bosi…tumekwishafika…tupe maelekezo tu…ahaa…kama ni mateso basi watapata ya kutosha…wakilainika ndiyo tutakupigia ili utupe maelekezo ya kuwatumbukiza!” alimaliza na kukata simu.

Akatangaza kwa wenzake wote aliokuwa nao kwamba kilichofuata sasa kilikuwa ni kipindi cha mateso, kamba mikononi na miguuni zikaongezwa, wakawa hawana namna kabisa ya kujinasua! Mbao, mawe na mijeledi ikasogezwa karibu, kazi ya kuwachapa mfululizo ikaanza huku wakilia kama watoto na kulazimishwa waeleze kila kitu juu ya walichokuwa wakifuatilia.

Hakuna aliyefungua mdomo wake kusema lolote, mateso yakaongezeka, ikiwa ni pamoja na kupigwa risasi za miguu kila mmoja lakini bado hawakutamka chochote, mwisho wakiwa taaban kabisa, sakafu yote imetapakaa damu, wakisubiri kufa na mara kadhaa wakiwa wamekwishaomba wenyewe bora wadumbukizwe kwenye mapipa ya tindikali kama Jinks alivyowatishia, simu ya mwanaume huyo katili iliita, akaipokea.

“Ndiyo bosi…wamelainika kabisa…tupe maelekezo tuwadumbukize, maana wao wenyewe wanataka hivyo…ahaa! Basi tunawasubirini mfike!” alimaliza Jinks na kukata simu.

Dakika ishirini baadaye mlango ulipigwa teke, watu wawili wenye mikono ya kiafrika na sura za kizee za Kijapan wakasukumwa na kuanguka sakafuni mbele ya Jinks, akiwa katika mshangao risasi nyingi zilisikika wa kwanza kuanguka chini akiwa amepigwa risasi ya kichwa akiwa Jinks ndipo wakafuatia wenzake aliokuwa nao katika zoezi la utekaji na utesaji.

Kamishna Mwangomole, Donald Crish na wenzao walikuwa wamelala sakafuni wakiwa taaban bila kuelewa kilichoendelea, mara wakashangaa kuhisi mtu akiwafungua kamba mikononi na baadaye vitambaa machoni mwao, walipoangalia mbele kila mmoja kwa wakati wake walikutana na sura ya mwanaume aliyeungua usoni na mikononi.

“Wewe ni nani?” Kamshina Mwangomole alimuuliza mwanaume huyo.
“Inspekta Masala!”

“Inspekta Masala? Si umekufa kwenye mlipuko wa bomu?”
“Sikufa, roho ya paka, ndiyo maana nimeungua kiasi chote hiki.”
“Mh!”

“Na hawa umewatoa wapi?”
“Ofisini kwao, walifikiri wamenimaliza, ambacho hawakufahamu ni kwamba walikuwa wanapambana na mnyama mwenye akili nyingi kuliko nyoka, mwisho wao umefika!”
“Hebu tueleze ulivyojiokoa?”

“Siyo muhimu kwa sasa, lazima kwanza mpate matibabu, kisha hawa wajinga wafikishwe mbele ya sheria, wamenitesa mimi na dunia nzima kwa muda mrefu, hakika huu ni wakati wa dunia kupigwa na butwaa, kwa muda mrefu Watanzania waliwaona kwamba ni wawekezaji kumbe ni wauaji, hawa wazee wawili ndiyo Dk Viola na Vanessa, hawa ni wanawake wala siyo wanaume, tazameni mikono yao ilivyo tofauti na sura zao, aibu!” aliongea Inspekta Masala akionekana kuwa kwenye maumivu makali, mkononi akiwa ameshika bastola huku akiwaangalia Dk Viola na Vanessa sakafuni, wakiwa wamefungwa mikono yao kwa nyuma kwa kutumia kamba.

Alichokifanya Inspekta Masala ni kumwomba Kamishna Mwongomole ambaye alijitambulisha kwake ili apige simu polisi, gari la wagonjwa lifike mara moja na kuwachukua kuwapeleka hospitalini, jambo hilo lilitekelezwa, nusu saa baadaye ving’ora vilisikika nje ya ghala hilo, idadi kubwa ya askari wakavamia ndani ambako walipigwa na mshangao kwa kuwakuta mzee Jonathan na Andrew kama walivyowafahamu wakiwa wamelala sakafuni.

“Hawa si ni wawekezaji wetu?” mmoja wa askari aliuliza.
“Wee Koplo acha ujinga, beba wagonjwa peleka kwenye gari, haya mambo mengine hayakuhusu,” Inspekta Masala alifoka.

Majeruhi wote walibebwa na kupelekwa kwenye gari la wagonjwa lililokuwa nje kwa ajili ya kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, huku nyuma Dk Viola na nduguye Vanessa wakipigwa pingu kisha kupandishwa kwenye gari la polisi, Inspekta Masala naye akapanda gari jingine la polisi, chini ya ulinzi mkali wakaondolewa eneo hilo hadi Kivukoni ambako magari yote yalipakiwa ndani ya boti na safari kuelekea Kituo cha Polisi Kati ikaanza.

Je, nini kitaendelea? Inspekta Masala alinusurikaje kwenye mlipuko wa bomu hatimaye kwenda kuwaokoa wenzake? Nini kitawapata Dk Viola na Vanessa? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

Leave A Reply