The House of Favourite Newspapers

Mabilionea Wasio na Huruma 48

0

spendthriftWAKATI Kamishna Mwangomole, Donald Crish na wapelelezi wengine ambao wametekwa na watekaji wa Dk. Viola na Vanessa kwa lengo la kuuawa kwa kudumbukizwa kwenye mapipa ya tindikali walijua Inspekta Masala amekufa kwa bomu ndani ya gari, mpelelezi huyo hatari anaibuka ndani ya ghala walimowekwa wakiteswa vibaya, hajafika peke yake bali ameongozana na Dk. Viola pamoja na Vanessa.

Risasi zinaunguruma, watekaji wote pamoja na Jinks, kiongozi wao wamepigwa risasi na kuanguka chini, Inspekta Masala anawafungua kamba mateka wote! Dk. Viola na Vanessa wakiwa wamelala chini, kamba mikononi.

Mwangomole na wenzake hawaamini wanachokishuhudia, simu inapigwa na polisi wanawasili na kuwabeba Dk. Viola na Vanessa kuwapeleka Kituo cha Polisi cha Kati, Inspekta Masala akifuatana nao na majeruhi wote wanabebwa kwenye gari la wagonjwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

INSPEKTA Masala alikuwa kwenye maumivu makali lakini alijikaza kiume mpaka wakafika Kituo cha Polisi Kati ambako viongozi wote wa jeshi la polisi walikuwa wamekusanyika wakisubiri kwenye chumba maalum cha mikutano ambamo pia alikuwemo Waziri wa Mambo ya Ndani, hakuna aliyeamini kwamba wawekezaji Jonathan na Andrew ndiyo walioingizwa ndani ya chumba hicho, wakidaiwa ndiyo wauaji Dk. Viola na Vanessa waliokuwa wakisakwa dunia nzima.

“Una uhakika kwamba ni wao?” Waziri wa Mambo ya Ndani aliuliza Dk. Viola na Vanessa wakiwa wameketi mbele yake, mikono yao imefungwa kwa pingu, alikuwa katika hali ya kutokuamini.
“Ni wao!”

“Hawa si ni wazee wa Kijapan? Wewe huwaoni? Unawezaje kusema hawa ni wanawake na tukakuelewa?”
“Aliyewafanyia upasuaji ni bingwa namba moja wa upasuaji wa plastiki duniani, tazama mikono yao ilivyo kama yako na yangu halafu angalia sura zao, hawa ni Waswahili, tena wa hapahapa Tanzania!”

“Ni wanawake?” Mkuu wa Jeshi la Polisi aliuliza.
“Ndiyo.” Inspekta Masala akajibu kwa kujiamini.

“Hebu niitieni askari wa kike wawili wanisaidie kuwapekua.” Mkuu wa Jeshi la Polisi aliamuru na wanawake wawili mmoja akiwa na V tatu na mwingine mbili waliingia na kuwachukua Dk. Viola na Vanessa kwenda nao kwenye chumba cha upekuzi kilichokuwa jirani tu na ukumbi wa mikutano, waliporejea nyuso zao zilikuwa zimejawa tabasamu huku macho yakionyesha mshangao wa wazi, Dk. Viola na Vanessa wakiwa wameinamisha nyuso zao chini kwa aibu.

“Afande ni wanawake wenzetu!”
“You must be kidding!” (Lazima utakuwa unanitania!)
“Siwezi kukutania afande!”
“Hawa ni wanawake?”
“Kabisa.”

“Hebu watupeni kwanza mahabusu.”
Ulikuwa ni mshtuko mkubwa mno, habari ziliposambaa kuwa Dk. Viola na Vanessa walikuwa wamekamatwa nchini Tanzania, jeshi la polisi liliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutoa taarifa hiyo ambayo ilisambazwa kila kona ya dunia kupitia mitandao, televisheni na magazeti.

Watu walifurika kituo cha polisi kutaka kuwaona Dk. Viola na Vanessa, hasa wale ambao ndugu zao waliuawa nao wakati wa zoezi la kuibiwa figo, hata ndugu wa watoto yatima waliokufa katika ndege! Kelele nje ya kituo cha polisi zilikuwa kubwa zikitoka kwa watu zaidi ya elfu mbili waliokusanyika, wakitaka Dk. Viola na Vanessa watolewe nje na kuchomwa moto.

Inspekta Masala akijisikia shujaa, aliyekamilisha kazi, aliamua kuondoka Kituo cha Polisi cha Kati kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kutafuta matibabu ya mwili wake uliokuwa umeumia vibaya kwa moto, alitembea na ulinzi wa polisi kila alikokwenda kwani alikuwa ni mtu muhimu sana kwenye kesi hiyo iliyowakabili mabilionea wauaji, hofu kwamba angeweza kuuawa ilikuwepo.

“Hujaungua sana, bahati nzuri moto haukukuchoma mpaka ngozi ya ndani, hii kwa kitalaam tunaita Superficial Burn, tutakupatia tu dawa za kupaka!”
“Ngozi yangu itarejea kama zamani?”
“Ndiyo.”

“Hiyo ndiyo ilikuwa hofu yangu kubwa.”
“Wala usiwe na wasiwasi.” Daktari alimjibu Inspekta Masala.
Kilichofanyika baada ya hapo ni kupewa dawa za kupaka, zoezi lilipokamilika akaondoka kwenda moja kwa moja chumba cha wagonjwa mahututi ambako Kamishina Mwangomole, Donald Crish na wapelelezi wengine walikuwa wamelazwa baada ya kutolewa chumba cha upasuaji kutibiwa majeraha ya risasi walizopigwa na watekaji.

Alipoingia walifurahi kumwona, alikuwa mkombozi ambaye bila yeye wangetumbukizwa kwenye mapipa ya tindikali kama ilivyokuwa imeamriwa na Dk. Viola na nduguye Vanessa, watu katili wasio na huruma. Baada ya salam, Kamishna Mwangomole na wenzake walikuwa na hamu ya kufahamu jambo moja tu; alijiokoaje kwenye bomu lililolipuka mbele ya macho yao.

“Naweza kusema ni bahati!”
“Huwa siamini sana katika bahati, naamini katika matendo.”
“Ninachokumbuka ni kwamba nilikwenda kisiwani Bongoyo ambako wauaji hao wamewekeza mamilioni ya dola, lengo langu lilikuwa ni kwenda kuwapeleleza kabla wapelelezi kutoka Marekani hawajafika, sababu bosi aliniambia wangefika saa moja jioni, nikafanikiwa kuwafikia na kukaa nao kwenye chumba cha mikutano nikijifanya mteja wa nyumba, nilikuwa nimevalia kofia na miwani, mmojawao sijui ni yupi akaniamuru nivue miwani na kofia, nikagoma kwa sababu nilijua nikivua watanigundua na huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu!”

“Enhe!” Mwangomole akiwa na hamu ya kujua kilichoendelea alimhamasisha Inspekta Masala kuendelea kusimulia.

“Nilipogoma waliwaita watu watatu wakubwa ajabu, ambao walikuja na kunikamata, nakumbuka kuchomwa sindano ambayo sielewi ni ya nini, nikapoteza fahamu kabisa, sikujitambua mpaka nilipozinduka na kujikuta nikiwa ndani ya gari! Nafikiri dawa waliyonichoma ilikuwa inaisha baada ya muda fulani, walijua sitazinduka, bomu lingelipuka nikiwa usingizini.”
“Ulipozinduka?”

“Nikaangalia na kugundua nipo ndani ya gari, mikono yangu imefungwa kwenye kiti cha dereva ile sehemu ya juu ambayo huwa tunaegemeza kichwa, chini yangu katikati ya miguu kuna bomu ambalo tayari lilikuwa limesababisha joto kali ndani ya gari, dalili kuwa muda si mrefu lingelipuka, nikaanza juhudi za kujifungua kutoka kwenye kiti, mpaka nikatumia meno lakini sikuweza, mwisho nikiwa nimeshakata tamaa kabisa nikakumbuka kuwa kile kiegemeo cha kichwa huwa kinang’ooka kwenye kiti, nafikiri waliponifunga hawakulifikiria hilo, nikaanza kutumia kichwa changu, vidole na mdomo mpaka nikafanikiwa kuking’oa kiegemeo na kujikuta nimefungwa lakini nipo huru, nilichofanya ni kufungua mlango na kuruka, bomu likalipuka sekunde chache tu baada ya mimi kuruka, moto ukanifikia kidogo mwilini.”

“Mungu wangu!” Kamishna Mwangomole alitamka maneno hayo akimwangalia Inspekta Masala kwa macho ya huruma huku akimshukuru Mungu kimoyomoyo maana kama angekufa kwenye bomu lile hata yeye asingekuwa hai.

“Nikabingirika ardhini kuelekea bondeni na baadaye kuendelea kukimbia mikono yangu ikiwa imefungwa kuondoka kabisa eneo hilo, nilitaka waendelee kuamini nimekufa ili iwe rahisi sana kwangu kuwakamata!”

“Huwezi kuamini bomu hilo lililipuka mbele ya macho yetu, maana tulikuwa tunakufuatilia kwa kutumia GPS!”
“Ninyi ndiyo mlikuja na gari?”
“Ndiyo!”

“Niliona taa za gari zikiwaka kabla sijaruka!”
“Ndiyo tulikuwa sisi, baada ya pale ndiyo jamaa walituteka na kutupeleka ghalani ulikotukuta!”

“Nilipotoka pale nilipita njia za porini mpaka kituo cha basi cha Goba, hapo nilitafuta mahali pa kupigia simu na mtandao wa intaneti, kwanza nikalipia nusu saa kwenye kompyuta kutafuta namba ya Dk. Viola, bahati nzuri nikaipata kwenye kitabu cha njano ambako kiko mtandaoni, nikampigia na kumpa taarifa juu ya kuwepo kwa wapelelezi kutoka Marekani, akafurahi mno na kunitaka niende kisiwani nikawaelezee vizuri, nikaona huo ndiyo ulikuwa wakati muafaka wa kuwateka.”

“Yes!” (ndiyo!) Kamishna Mwangomole aliendelea kuchochea kama vile alikuwa mzima bila jeraha lolote mwilini.

“Nikakodisha pikipiki iliyonipeleka moja kwa moja hadi hotelini kwangu ambako nilichukua bastola na kuelekea kivukoni walikokuwa wameandaa boti, ambayo ilinibeba na kunipeleka hadi kisiwani ambako nilifanikiwa kuwateka na kuwaamuru wazuie msiwekwe kwenye tindikali na baada ya hapo nikawateka tena ndani ya gari lao, Dk. Viola akiendesha bila mtu yeyote kutambua kilichokuwa kikiendelea na kuwaleta hadi ghalani ambako yalitokea mliyoyashuhudia nikawaokoa, moyo wangu una furaha mno, kuwapata hao watu, wamenitesa kwa muda mrefu! Serikali ya Tanzania haiamini kabisa kwamba hao ni Dk. Viola na Vanessa!”

JE, nini kitaendelea? Hao waliokamatwa ni Dk. Viola na Vanessa kweli au kuna mchezo? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.

Leave A Reply