The House of Favourite Newspapers

Mabilionea Wasio na Huruma 55

0

INSPEKTA Masala ameomba msaada wa makomandoo kutoka Washington DC ili wamsaidie kwenye zoezi la kuwakamata Dk Viola na Vanessa, wauaji wanaosakwa dunia nzima lakini wamejificha nchini Tanzania wakiwa wawekezaji na kubadilisha majina. Ameahidiwa na bosi wake kwamba makomandoo wangefika siku iliyofuata saa moja na nusu jioni.

Katika muda huo Inspekta Masala ameamua kwenda kisiwani Bongoyo kuitafuta ofisi ya Dk Viola na Vanessa akijifanya mteja wa nyumba, alichokifanya ni kuvaa kofia kichwani pamoja na miwani kwa lengo la kujibadilisha lakini akiwa chumba cha mkutano na Dk Viola na Vanessa, mabilionea wasio na huruma, mmoja wao anamtaka avue kofia lakini Inspekta Masala amegoma kwa sababu kufanya hivyo ni kujiingiza katika hatari kama watamgundua.

Alipogoma, Jonathan anabonyeza kitufe na wanaingia watu watatu wenye miili ya kukata na shoka na kumvua Inspekta Masala kofia na miwani, haikuwa siri tena Dk Viola na Vanessa wakamtambua. Walichofanya ni kuagiza achomwe sindano ya usingizi haraka na aendelee kuchomwa kila baada ya saa nne, ili giza likiingia wamchukue kwenda kumuua ndani ya gari huko Goba wakiwa wametega bomu miguuni mwake.

Wamefika msituni Goba, Inspekta Masala akiwa bado yu usingizini, kinachofanyika hapo ni kutega bomu lilipuke baada ya saa moja, zoezi hilo lilipokamilika wote waliondoka bila kujulikana, wakiwa ndani ya gari masikio yao yote yalikuwa walikotokea wakisikiliza mlipuko.

Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

JONATHAN ama Dk Viola na Andrew ama Vanessa na vijana wao wa kazi,           waliondoka eneo la tukio wakijisikia washindi, hapakuwa na namna Inspekta Masala angeweza kujiokoa, mikono yake ikiwa imefungwa kwenye kiti cha gari kwa kutumia tai, lazima baada ya saa moja bomu lingelipuka na angebaki vipande vipande bila uwezo wa kutambulika.

Kwa Dk Viola na Vanessa ilikuwa ni furaha mno kwani mtu huyo aliwakosesha usingizi, kifo chake kilimaanisha kuendelea na maisha ya kutanua nchini Tanzania ambako waliheshimika kama wawekezaji, hakuna mtu kwa jinsi walivyoona angeweza kugundua kwamba ni wao ndiyo wauaji namba moja duniani waliokuwa wakisakwa kwa gharama yoyote, mtu pekee aliyebaki akijua siri hiyo alikuwa ni Inspekta Masala ambaye ndani ya muda mfupi tu angekuwa kuzimu.

Gari lao lilishasafiri dakika arobaini na tano nzima, zikawa zimebaki dakika kumi na tano tu kabla bomu halijalipuka, Jonathan ama Dk Viola aliyekuwa akiendesha gari hilo alikanyaga breki na kupunguza mwendo akionekana kushtuka kama vile amekumbuka kitu.

 “Mlikumbuka kumchoma sindano ya Valium ya saa kumi na moja na nusu?”

“Aaah!”

“Vipi mbona umeshtuka?”

“Tulisahau bosi.”

“Mungu wangu! Hatazinduka yule?” Andrew ama Vanessa aliuliza kwa mshangao.

“Inaisha mwilini baada ya muda gani?”

“Saa nne!”

“Hiyo inamaana kuanzia saa kumi na moja na nusu hatakuwa na dawa mwilini, lazima atazinduka!” Jonathan aliongea akionyesha masikitiko.

“Tufanye nini? Turudi?”

“Hakuna saba…” hakuimalizia sentensi yake wakasikia mlipuko wa bomu nyuma yao.

“Tayari! Kwisha kazi yake!” Andrew ama Vanessa alitamka maneno hayo akishangilia.

Kwa mlipuko huo wakawa na imani kabisa Inspekta Masala alikuwa ni marehemu, tena kifo kibaya kupindukia, bila kupoteza wakati wakaamua kuendelea na safari yao kuelekea Mbezi Beach ambako waliingia Barabara ya Bagamoyo kurejea jiji la zamani la Dar e Salaam ambako wangepanda boti kuwarejesha kisiwani Bongoyo kulikokuwa na jiji jipya la Dar ambalo wengi waliliita Dar es Salaam New City.

***

Joto lilikuwa kali mno ndani ya gari, hilo ndilo lililomzindua Inspekta Masala kutoka usingizini, mwili wake wote ulikuwa umelowa jasho. Alishangaa kujikuta amefungwa mikono yake yote miwili kwenye kiegesheo cha kichwa cha kiti cha dereva, kwanza alijiuliza ni wapi alipokuwa bila kupata majibu, alipovuta vizuri kumbukumbu zake alichokikumbuka kwa haraka ni kuwemo ndani ya chumba cha mikutano ofisini kwa Dk Viola na Vanessa.

“Kwa nini wamenileta hapa?” aliwaza huku akisikia joto kali sana kwenye miguu ambako kulionekana kutoa kitu kama mvuke, akainamisha uso wake kuangalia chini, kwa msaada wa mbalamwezi  macho yake yalikutana ana kwa ana na bomu likiwa katikati ya miguu.

Moja kwa moja akaelewa ni kwa nini alikuwa pale, aliletwa kuuawa, Mungu alikuwa amemzindua usingizini na sasa alikuwa na wajibu wa kujiokoa asife. Alipojaribu kuvuta mikono yake alishindwa, ilikuwa imekazwa mno kwenye kiti, hakukata tamaa akaendelea kuvuta kwa muda bila mafanikio, macho yake yalipotua kwenye saa ilimweleza ilikuwa tayari saa mbili kamili usiku.

Alichokifanya ni kuendelea kujivuta na hata kuiuma kwa meno tai aliyofungwa nayo kwenye kiti ili apate kujiokoa lakini haikuwezekana, mwili ukachoka, akaanza kuhisi nguvu zinapungua sababu ya joto lililokuwemo ndani ya gari. Moyoni akaamini hapakuwa tena na namna ya kujiokoa, hivyo akaanza kusali akimwomba Mungu amwokoe mwenyewe kwa uwezo wake na kama isingewezekana hilo kutokea basi amsamehe dhambi zake zote na kumpokea kwenye ufalme wake, akimalizia sala hiyo ilikuwa tayari ni saa mbili na dakika ishirini na tano, macho yake yakaona mwanga wa gari likikaribia eneo hilo, hakuwa na wazo jingine zaidi ya kuamini Mungu amejibu maombi yake.

***
Ndege iliyowabeba makomandoo kutoka Marekani ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam saa moja na nusu kama ilivyopangwa na baadaye kusimama kabisa, kila mtu akabeba mzigo wake na kuanza kushuka hadi chini ambako walipokelewa na wapelelezi wa CID na Interpol waliokuwa na taarifa juu ya ujio wao.

“My name is John Mwangomole, Deputy Director of Criminal Investigation here, welcome to Tanzania!”(Naitwa John Mwangomole, ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Karibuni Tanzania!)

“Thank you so much, I am Donald Crish, these are my colleagues, like you were told, we are here to join our fellow in hunting two chronic criminals; Dr Viola and Vanessa!”(Ahsante sana, naitwa Donald Crish, hawa ni wenzangu, kama ambavyo uliambiwa na wakubwa zangu, tuko hapa kuungana na mwenzetu kuwasaka wahalifu sugu; Dk Viola na Vanessa!)

“We will be more than read to assist you, though I think Dr Viola and Vanessa are not within our borders!”(Tutakuwa tayari kuwasaidia kwa lolote, ingawa nafikiri Dk Viola na Vanessa hawapo ndani ya mipaka yetu!)

“They are here sir!”(Wako hapa mkubwa!)

“Really?”(Kweli?)

“Yeah!”(kweli!)

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai alikataa kabisa kwamba Dk Viola na Vanessa walikuwepo nchini Tanzania, hata hivyo akawa tayari kuwasaidia katika kukamilisha kazi iliyowaleta akishirikiana na Interpol. Kilichofanyika hapo ni Donald Crish kupiga simu ya Inspekta Masala kama walivyoagizwa na bosi wao, ikaita tu bila kupokelewa, jambo ambalo halikuwa kawaida kabisa. Aliendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu bila mafanikio, hatimaye akaamua kutaarifu viongozi wake Washington DC ambao walimwambia watumie mtambo wa GPS kuhakikisha wanamfikia Inspekta Masala kwani alionekana kuwa kwenye matatizo.

Mtambo wa GPS ulitumia minara ya simu, ilikuwa ni kazi rahisi kufahamu mahali mtu alipokuwa kwa kuangalia namba ya mnara wa simu alioutumia kuwasiliana, wakiwa ndani ya jumba la wasafiri, kwa pamoja waliwasha mashine ya GPS na kuanza kuangalia kwa umakini, simu ya Inspekta Masala ilikuwa hewani kwenye mnara namba 112236, uliopo eneo la Goba.

“Let’s go after him!”(Hebu tumfuatilieni!) aliongea Donald na kuingiza namba ya mnara huo kwenye mashine ya GPS ambayo ilianza kuwaelekeza barabara zote za kupitia kuelekea Goba, wakitumia maneno kama “Upo saa nzima kutoka mahali unapokwenda, baadaye ikawa nusu saa, hatimaye dakika kumi na mwisho dakika tatu, hii ilifika wakiwa katikati ya pori la Goba, mbele yao wakaliona gari aina ya Vitz ya rangi nyeupe, wakasimama kwa mshangao.

“Anaweza kuwa yumo ndani?”

“Kabisa!”

“Sasa kwa nini amekuja hapa?”

“Hata sijui.”

“Wawili twende kwenye gari wengine mtulinde kama kutakuwa na watekaji!” Donald Crish alisema.

Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai akajitokeza ili yeye na Donald watembee kuelekea kwenye gari, hawakwenda umbali mrefu sana kabla hawajasikia mlipuko wa ajabu, kila mtu akaanguka chini na kulala kifudifudi akijaribu kuokoa maisha yake.

Je, nini kitaendelea? Inspekta Masala amekufa? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply