The House of Favourite Newspapers

Mabilionea wasio na huruma 60

0

us-dollarsILIPOISHIA…
Ushahidi wa kuwatia hatiani Dk Viola na nduguye Vanessa kwa mauaji ya mtungo waliyoyafanya umetolewa mahakamani na mashahidi wachache tu na inaonekana wazi kabisa hawana namna ya kukikwepa kitanzi.

Mawakili wao, John Mbwambo na Denis Crapton ambao wameahidiwa dola za Kimarekani milioni mia tano kama wangefanikiwa kuwaokoa wateja wao na kifo wanafikiria juu ya nini cha kufanya, wamegundua kabisa hakuna njia halali ya kuweza kuwakomboa Dk Viola na Vanessa ili wajipatie dau hilo nono.

Sasa wameanza kupanga mpango wa kufanya ufisadi ili tu wapoteze vielelezo na kuwahonga fedha nyingi watumishi wa mahakama, Dk Viola na Vanessa wamebariki mpango huo na wamewapa kadi yao ya benki ili wachukue fedha kwenye akaunti yao kutekeleza zoezi hilo.

Lengo ni kupoteza vielelezo vyote vilivyotolewa mahakamani, mawakili wameamua kulichoma jengo la mahakama ili kuviteketeza vielelezo hivyo, ni tendo baya na kinyume cha taaluma yao lakini hivyo ndivyo mambo wakati mwingine hufanyika katika baadhi ya mahakama ili kutafuta ushindi wa kesi.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO….
SONGA NAYO…

Hakuna mtu aliyeamini, watu walipomiminika mahakamani asubuhi hiyo na kukuta jengo la mahakama kuu likiwa limeteketea kwa moto, walinzi walidai ulianzia kwenye chumba cha kuhifadhia vielelezo na watalaam wa moto walipofika walidai ilikuwa ni shoti ya umeme! Uongozi wote wa mahakama ulipagawa kwani kulikuwa na vielelezo muhimu mno vya kesi za wauaji ambao dunia nzima ilikuwa ikiwafuatilia!
“Mungu wangu tutafanya nini?” Jaji Kabengwe Lupilia alisema akiwa ameweka mikono kichwani.

Kila mtu mahakamani alionekana kuchanganyikiwa, fikra zote zilikuwa juu ya vielelezo muhimu vya kesi, ambavyo kwa hakika bila kuwepo kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa Dk Viola na Vanessa kuachiwa huru baada ya mahakama kushindwa kuthibitisha kosa lao.

Huo ndiyo ulikuwa wasiwasi wa wanasheria wote wa upande wa mashtaka ingawa upande wa utetezi walipofika mahakamani na kukuta jengo la mahakama limebaki gofu sababu ya moto walionyesha furaha ya waziwazi.

Kikao kilifanyika haraka iwezekanavyo ndani ya jengo la makao mkuu ya jeshi la polisi idara ya upelelezi, aliyeongoza kikao hicho alikuwa ni Kamishina Mwangomole, tayari alisharuhusiwa kutoka hospitali baada ya jeraha la risasi alilopigwa na watekaji akiwa njiani kutokea Goba pamoja na wapelelezi kutoka Marekani waliotumwa kuja kumsaidia Inspekta Masala.

“Nawaelezeni wazi, tukio hili siyo bure, lazima Dk Viola na Vanessa wako nyuma yake, wana uwezo wa kufanya chochote hata kama wako mahabusu, wale wanawake ni hatari!”

“Inawezekana afande.” Alijibu msaidizi wake.
“Siyo inawezekana huo ni ukweli, ninyi fanyeni kila kinachowezekana kupeleleza ili tuujue ukweli na kama kweli wanahusika, ushahidi ukusanywe na waongezewe kosa jingine kwenye kesi zao, safari hii hawawezi kunusurika.”

“Sawa afande!”
Kikundi cha wapelelezi kumi kiliundwa wote wakiwa na elimu ya kutosha pamoja na uzoefu wa mambo ya upelelezi wa eneo la tukio au kwa Kiingereza iliitwa Crime Scene Investigation (CSI), Kamishina Mwangomole alijiridhisha kabisa kuwa timu aliyoiunda ilikuwa na uwezo wa kufanya upelelezi na kupata jibu kabla ya Agosti 26, siku ambayo kesi ya mauaji iliyowakabili Dk Viola na Vanessa ilitarajiwa kurejea mahakamani.
“Muda mrefu sana huo mkuu!”
“Basi nendeni mkafanye kazi.”
“Sawa.”

Wiki moja tu baadaye taarifa ilikuwa mezani, upelelezi ulishakamilika na Kamishina Mwangomole akaitisha tena kikao ofisini kwake ili kupokea taarifa ya upelelezi uliokamilika, idadi ya vigogo watano, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani walikuwepo kusikiliza ripoti hiyo ambayo kila mtu alikuwa akiisubiri na ilidaiwa kulikuwa na shinikizo la mataifa makubwa ambayo watu wake walikufa kwenye ajali ya ndege kutaka haki itendeke.

“Haya tuelezeni!”
“Kazi imekamilika, tulikuta galoni mbili ambazo baada ya kuzichunguza tuligundua zilikuwa na harufu ya petrol, pia kulikuwa na kamba ndefu iliyoungua ambayo ilitokea barabarani.”
“Mh! Endelea.”

“Jengo la mahakama lilichomwa, aliyelichoma alitanguliza galoni za petrol ambazo ndani yake alidumbukiza kamba ya katani ambayo alishailowanisha na petrol kabla na yeye aliiwasha kamba hiyo kwa moto akiwa umbali wa mita mia, moto ukakimbia ukiifuta kamba na ulipoifikia galoni, petrol ikalipuka na nyumba kuwaka na galoni hizo zilitegwa kabisa kwenye stoo ya kutunzia vielelezo, maana yake ni kwamba mtu aliyewasha moto huo alikuwa na lengo la kuteketeza vielelezo!”

“Hilo halina ubishi, hawa lazima ni Dk Viola na nduguye, shida ni jinsi ya kuwaunganisha kwenye kosa hili!” Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamishina Amran Juma alisema.

“Kweli kabisa afande, lakini mmekwishachunguza ni mlinzi gani alikuwepo usiku hule?”
“Anaitwa mzee Ambrose Amlima, bado hatujamfuata nyumbani kwake!”
“Huyo lazima atakuwa anafahamu ni nani aliyezitega galoni hizo, haiwezekani mtu aje atege galoni kwenye jengo la mahakama bila yeye kumuona!”
“Kabisa afande, tutamfutilia leo!”
“Fanyeni hivyo mara moja!”
***
Kwenye chumba maalum ndani ya gereza, Dk Viola na Vanessa waliketi na wanasheria wao, wakiongea kwa sauti ya kunong’ona na kupewa taarifa juu ya kilichotokea, tabasamu zilifunika nyuso zao, dalili ya kwamba hatimaye wangeweza kuachiwa huru ilionekana dhahiri, kwani bila vielelezo kuthibitisha kwamba wao ndio waliofanya mauaji, haikuwa rahisi kuwatia hatiani, mwisho wa siku wangekuja kuachiwa huru.

“Hongereni sana, sikutegemea ingekuwa kazi rahisi kiasi hicho!”
“Haikuwa rahisi, bali ngumu, hatukutaka kumtumia mtu yeyote kwa hofu kwamba siri ingeweza kuvuja, badala yake mimi mwenyewe nilifanya hiyo kazi ya kwenda kutega galoni za petrol na kulipua jengo.”
“Duh!”

“Uliwezaje?”
“Fedha haishindwi kitu.”
“Aliyekusaidia hakujua unachokwenda kufanya?”
“Hakuelewa.”
“Ulifanya nini?”

“Nilinunua galoni zangu mbili za petrol na kamba ambayo niliimwagia petrol na kupima umbali wa mita mia moja, usiku nikaenda karibu na jengo la mahakama ambako nilimkuta mlinzi na kumpa shilingi elfu ishirini nikimwambia gari yangu ilikuwa inachemsha, aniruhusu nichote maji karibu na jengo la mahakama, mzee yule wala hakuwa na shaka yoyote na mimi wala hakunitambua kwa jinsi nilivyokuwa nimevaa, akaniruhusu.”

“Halafu kikafuatia nini?”
“Nikachukua galoni mbili, moja tupu na nyingine ikiwa na petrol, kisha nikatembea mpaka kwenye bomba ambalo liko ukutani kwenye jengo la mahakama lenye stoo ya kuhifadhia vielelezo, nikaiacha galoni yenye petrol na kuchota maji ambayo nilikwenda nayo mpaka kwenye gari, ikayamwaga chini kisha kuchukua galoni ya pili yenye petrol, safari hii ilichukua pia kamba iliyolowanishwa ambayo nilikwenda kuidumbukiza kwenye galoni kisha nikachota maji na kurejea mpaka kwenye gari ambako nilichukua kiberiti na kuiwasha kamba kisha mimi nikaondoka, mbele kidogo tu nilisikia mlipuko, jengo lilikuwa likiwaka moto.”
“Umefanya kazi nzuri!”

“Hawana tena vielelezo, hakika tutashinda kesi, ziandaeni tu hizo dola milioni mia tano, tunataka kutajirika.”
“Sisi hatuna tatizo, ili mradi tu tutoke hapa.”

“Tarehe 26 mwezi wa nane tutasikiliza wanasema nini mahakamani, lakini lililopo hivi sasa ni kukanusha tu ili walete vielelezo vya kuthibitisha mliua, mtu mwingine ambaye hatakiwi kabisa kuwa hai ni mlinzi, maana yule anaweza kutoa ushahidi wa mtu aliyekuja usiku, huwezi kujua pengine alinitambua!”
“Anastahili kufa.”
***
Kazi waliyokuwa nayo polisi wa upelelezi baada ya kutoka kwenye kikao ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa Ambrose Amlima, mzee aliyekuwa zamu siku ya tukio. Aliishi maeneo ya Mburahati karibu kabisa na Kigogo Bondeni, iliwachukua siku tatu kamili kupata mahali alipoishi maana hata kazini kwake kwenye Kampuni ya Ulinzi ya Goha Security hawakujua alikoishi.

Aliishi kwenye kibanda kidogo kilichoezekwa kwa madebe, kikiwa kando kabisa ya mto Msimbazi, mahali ambako hakuna mtu mwingine aliishi! Palikuwa ni bondeni mno, mara kadhaa alishanusurika kufa kwa mafuriko usiku akiwa amelala. Aliyewasaidia kufika kwenye kibanda hicho alikuwa ni mamantilie aliyemuuzia mzee Ambrose chakula kila siku jioni.

“Alipita hapa majuzi akiwa amechanganyikiwa kabisa, akidai kuna matatizo yametokea kazini kwake, lakini jana saa moja usiku kuna watu wengine wawili walikuja wanamuulizia nikawaelekeza, nyoosheni tu moja kwa moja na njia hiyo hadi bondeni, nyumba ya mwisho kabisa ndiyo yake!”

Askari walifanya kama walivyoelekezwa, hawakuwa na sababu ya kuwa na hofu kwani ilikuwa ni saa kumi na nusu za jioni hivyo walitembea kwa kasi mpaka wakafika mbele ya kibanda hicho na kuanza kubisha hodi, hakuna aliyewaitikia, wakabisha tena na tena lakini hali iliendelea kuwa kimya, mwisho wakafikia uamuzi wa kusukuma mlango, ulikuwa wazi! Jambo ambalo hawakulitegemea na walipofika tu sebuleni wote walishtuka, mzee Ambrose alikuwa akining’inia darini, kamba shingoni.
“Masikini amejinyonga!”

“Mh! Kajinyonga mweyewe huyu?” aliuliza askari mwingine.
“Hata mimi nina shaka, hii hapa ni barua, bila shaka kaacha mwenyewe!”
Wakainama na kuanza kuisoma bila kuigusa maana hawakutaka kuharibu ushahidi, iliandikwa kwa mwandiko mzuri kabisa ambao haukulingana na umri wa mzee Ambrose;

Nimeamua kujiua, kosa nililolifanya ni kubwa mno, hasira ilinifanya nichome jengo la mahakama, bora niondoke duniani kuepuka aibu na mateso ya gerezani!

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika gazeti la Championi Jumatano.

Leave A Reply