Mabilionea wasio na huruma-60
ILIPOISHIA…
INSPEKTA Masala amefanikiwa kuwaingiza kwenye mkono wa sheria Dk Viola na nduguye Vanessa ili wahukumiwe kwa mauaji ya kikatili waliyoyafanya wakati wakitafuta fedha kwa njia haramu.
Wamewekwa Gereza la Segerea kusubiri hatima yao huku wakitakiwa kueleza ukweli wa kila kitu lakini Dk Viola na Vanessa wamegoma kuongea jambo lolote mpaka pale mwanasheria wao atakapofika ndipo watakuwa tayari kusema chochote.
Mwanasheria wao kutoka Kampuni ya Mbwambo Advocates and Co ambaye wakati wanakamatwa hakuwepo nchini, akiwa Afrika Kusini anapata taarifa hizo kupitia vyombo vya habari anaamua kurejea ili kujua nini kiliwapata wateja wake hao. Anafika moja kwa moja gerezani na kuomba kuonana na wateja wake ambao wanamweleza ukweli wote huku wakimtaka afanye kila kinachowezekana kuhakikisha anawanusuru na adhabu iliyokuwa mbele yao kwa ahadi ya malipo dola milioni mitano.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…
SIKU mbili baadaye Denis Crapton alifika nchini Tanzania na kuingia mkataba na Kampuni ya Uwakili ya Mbwambo Advocates and Co ili kuwatetea Dk Viola na nduguye Vanessa, walielezwa kila kitu wazi, wauaji walikiri kabisa kufanya kila tendo waliloshtakiwa nalo lakini mawakili wao wakitamani utajiri wa dola milioni mia tano, waliwataka wakisimama mahakamani wakanushe makosa yote ya mauaji baada ya hapo ndipo kesi ianze.
Ndivyo ilivyotokea, wiki moja baadaye taratibu za kisheria zilipokamilika, washtakiwa walifikishwa mahakamani mbele ya Jaji Julius Lupondije, aliyekuwa na umaarufu wa kushughulikia kesi ngumu nchini Tanzania zikiwemo za uhaini. Kwenye umri wa miaka arobaini na tano alishajizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa majaji na tasnia nzima ya sheria.
Kama walivyoelekezwa Dk Viola na Vanessa walikanusha mashtaka yote mia tatu ya mauaji, ndipo kesi ikapangwa kuanza kuunguruma baada ya mwezi mmoja mashahidi na ushahidi wote ukishawekwa tayari na upande wa mashtaka. Washtakiwa wakarejeshwa kwenye Gereza la Gontwa kusubiri siku ya kesi iwadie.
Kesi hiyo ilikuwa imevuta hisia za watu wengi mno ndani na nje ya Tanzania sababu watu waliouawa walikuwa si Watanzania peke yao, vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vikiwemo CNN, BBC na Skynews vilikuwepo nchini Tanzania kuripoti kila kilichoendelea, kwa mara ya kwanza jina Tanzania likaonekana kwenye luninga karibu kila siku kesi ya Dk Viola na Vanessa, wanawake katili walioua watu wengi pengine kuliko mwanamke mwingine yeyote katika historia.
Siku ya Septemba 20, ndiyo siku ambayo kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kutoa maelezo yake, mahakama ilikuwa imefurika watu ndani na nje kiasi kwamba kulilazimika kuwekwa vipaza sauti mpaka kwenye miti ili watu waweze kusikiliza vizuri kilichokuwa kikiendelea Mahakama Kuu ya Tanzania.
Nusu ya watu wote waliokuwepo mahakamani walikuwa ni Wazungu, waliofika nchini Tanzania kufuatilia kesi ya ndugu zao, wengine walikuwa wakilia na walikuwa wameshikilia mabango yaliyokuwa yakidai haki kutoka katika mahakama, polisi waliwafuata na kuwaambia wayashushe mabango hayo kwani yalikuwa yakiingilia uhuru wa Mahakama ambayo haikutakiwa kushawishiwa kwa namna yoyote na mtu yeyote kufikia uamuzi fulani.
Saa mbili kamili ving’ora vilisikika, msafara wa magari zaidi ya kumi ya polisi yakiongozwa na pikipiki uliwasili kwenye viwanja vya Mahakama Kuu, watu wakakaa tayari kuwashuhudia Dk Viola na Vanessa wakiingizwa mahakamani, kama kawaida waandishi wa habari nao walikuwepo wakizitafuta picha za watu hao kwa udi na uvumba, pamoja na kuzuiliwa na polisi lakini walitumia haki yao ya kufanya kazi.
Wakashushwa na kuingizwa mahakamani, huku sauti za watu wakipiga kelele na kusema “Murderers, must be excuted!” “Wauaji lazima wauawe” watu walikuwa wakilia hasa walipokumbuka ndugu zao, hapakuwa na mtu hata mmoja kati ya waliokusanyika aliyeonekana kuwahurumia Dk Viola na Vanessa, ambao nyuso zao hazikuonyesha huzuni yoyote, walikuwa wakitabasamu jambo lililowazidishia hasira watu waliofurika mahakamani.
Wakaingizwa kwenye chumba fulani ambako walikutana na wanasheria wao kabla ya kupandishwa kizimbani dakika thelathini na tano baadaye na saa tatu kamili ndipo Jaji aliingia, watu wote wakabaki kimya, ingawa kwikwi za vilio zilikuwa zikiendelea kusikika kwa chini chini.
Jaji akaitaja namba ya kesi na baadaye kuwaita kwa majina washtakiwa, wakaitika na kujitambulisha, wakafuatiwa na mawakili wao ndipo mwendesha mashtaka akaanza kuisoma kesi hiyo na kuieleza mahakama kwamba ushahidi wote ulikuwa umekamilika na kulikuwa na vielelezo sabini na mbili vya kisayansi kuthibitisha kuwa washtakiwa walifanya mauaji yote waliyoshtakiwa nayo, pia alieleza kulikuwa na mashahidi themanini ambao wote wangesimama mahakamani kuthibitisha kuwa Dk Viola na nduguye Vanessa walifanya mauaji hayo ya kutisha.
“Basi ni vizuri muandae vielelezo vyote na mashahidi ili Septemba 30, ambayo ni siku kumi kuanzia sasa, tuanze kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, sijui itatuchukua muda gani, lakini ningependa mashahidi wote wasikilizwe kabla hatujawapa nafasi upande wa utetezi kujitetea!”
“Sawa Mheshimiwa, kila kitu kitakuwa tayari.”
“Basi naiahirisha kesi hii mpaka Septemba 30, saa mbili asubuhi, ahsanteni!”
Dk Viola na Vanessa, wakiwa katika sura zao zilezile za wazee wa Kijapan walifungwa pingu tena na kuondolewa chumba cha mahakama chini ya ulinzi mkali hadi nje ambako walipakiwa kwenye magari tayari kwa kurejeshwa Gereza la Gontwa.
***
“Mshtakiwa namba moja unaweza kuieleza mahakama hii jina lako?”
“Naitwa Jonathan…..”
“Unaweza kuieleza mahakama hii jinsia yako?”
“Mimi?”
“Ndiyo naongea na wewe.” Mwanasheria wa serikali Anganile Hosea, kijana mwenye umri wa miaka thelathini lakini akiwa na shahada mbili za sheria alizozisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na London, Uingereza alimjibu.
“Ni mwanamke!”
“Wewe ni mwanamke?”
“Ndiyo.”
“Umeshawahi kusikia mwanamke mwingine akiitwa kwa jina la Jonathan?”
“Huo ni uamuzi wa mtu.”
“Lakini ujuavyo wewe jina la Jonathan ni la kiume au la kike?”
“La kiume!”
“Ikawaje wewe uwe na jina hilo?”
“Uamuzi tu.”
“Umewahi kuwa na majina mengine katika maisha yako?”
“Pia naitwa Viola.”
“Taaluma yako?”
“Bingwa wa Figo.”
“Unaweza kuieleza mahakama hii wewe ni raia wa nchi gani?”
“Tanzania.”
“Umewahi kuwa na uraia wa nchi nyingine yoyote?”
“Ndiyo.”
“Wapi?”
“Thailand!”
“Unafanana na Mtanzania kwa sura?”
Sauti wakili wa Dk Viola ilisikika akisimama “mheshimiwa Jaji swali lililoulizwa na Mheshimiwa Wakili upande wa mashtaka naliwekea pingamizi.”
“Kwa nini?”
“Liko nje ya utaratibu.”
“Utaratibu upi?”
“Halina umuhimu.” “Mheshimiwa Anganile endelea na swali lako.”
“Nimekuuliza unafanana na Mtanzania kwa sura?”
“Hapana.”
“Unafanana na raia wa wapi?”
“Japan.”
“Umewahi kufanya upasuaji wa kubadilisha sura?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini?”
“Nilikuwa nataka tu kufanana na Wajapan.”
“Ulipofika hapa nchini Tanzania kutoka Thailand ulijitambulisha kuwa wewe ni mwanamke au mwanaume?”
“Mwanaume.”
“Kwa nini ulijitambulisha hivyo wakati wewe ni mwanamke? Nikikuita muongo mzoefu utakataa?”
“Napenda kuonekana mwanaume ili watu waniheshimu, sitakataa.”
“Umewahi kuwa na kituo cha kulea watoto yatima hapa?”
“Ndiyo.”
Je, nini kitaendelea? Dk Viola na nduguye Vanessa watafanikiwa kunusurika na mkono wa sheria? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.