Mabilionea Wasio na Huruma 66
JENGO la mahakama limeteketea kwa moto na kuunguza nyaraka muhimu ambazo zilikusanywa kama ushahidi muhimu kwa kesi mbaya ya mauaji ya udunguaji, iliyokuwa ikiwakabili Dk. Viola na pacha wake, injinia Vanessa. Taharuki inatanda kila mahali, jopo la majaji na mawakili wa serikali, waliokuwa wakisikiliza na kuendesha kesi hiyo, wanachanganyikiwa na kushindwa kabisa kujua nini hatima ya sakata hilo, kuungua kwa ushahidi huo, lilikuwa ni pigo kubwa mno kwa kesi nzito kama hiyo.
Macho ya watu wengi duniani kote yalikuwa nchini Tanzania, kujua hatima ya kesi hiyo ambayo ilitingisha kila mahali, kwani watuhumiwa hao walikuwa wameua mamia ya watu duniani, kwa kujivika ngozi ya kondoo kwa wema wa bandia, kumbe ndani wakiwa zaidi ya mbwa mwitu.
Upande wa pili, tayari kundi la wapelelezi wa ndani na wale wa kimataifa, wakiongozwa na Kamishna Mwangomole, wanaamua kufuatilia kwa undani zaidi juu ya tukio la kuungua kwa mahakama hiyo, ambapo kwa juhudi na jitihada kubwa wanafanikiwa kufika mahali ambako aliyekuwa mlinzi wa mahakama, Mzee Ambrose Amlima alikuwa akiishi. Ni ndani ya kibanda kichakavu, kandokando kabisa na Mto Msimbazi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wanamkuta mzee huyo akiwa amekufa na kuning’inia kwa kamba, ikiwa ni ishara ya kujinyonga, pembeni yake wanakuta barua ikielezea mazingira na sababu za mzee huyo kujiua. Hata hivyo, askari hao, wakitumia taaluma ya uchunguzi wa eneo lilipofanyika Tukio la Jinai (Crime Scene Investigation) au CSI, wanapingana na hali hiyo, ambapo barua hiyo kulingana na uzuri wa mwandiko wake, isingewezekana kuandikwa na mzee huyo.
Zoezi la kushughulikia maiti ya Mzee Ambrose, linaendelea na katika hatua za mwisho, ndipo wanagundua barua halali ambayo inawaaminisha moja kwa moja kuwa iliandikwa na marehemu Ambrose muda mfupi kabla ya kifo chake, kutokana na mwandiko ulivyokuwa. Ni barua hiyo ndiyo inawapa mwanga wapelelezi hao, kutokana na vielelezo muhimu walivyovikuta, ambapo mlinzi huyo alikuwa ameandika kila kitu kilichotokea siku ya tukio la kuungua kwa mahakama, ikiwa ni pamoja na namba za usajili za gari TXD 33321 lililofika mahakamani hapo na dereva wake aliyejifanya anaomba msaada wa maji, baada ya gari lake kuzima, ukiwa ni uongo.
Uamuzi unaofikiwa na askari, ni kuuchukua mwili wa marehemu Ambrose na kuupeleka katika Hospitali ya Amana kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu (post – mortem).
Huku nyuma, ndani ya mahabusu, Dk. Viola na pacha wake, Vanessa, wamejawa na furaha isiyo na kifani, muda mwingi walionekana wakitabasamu, wakiiona dunia nzima iko mifukoni mwao, kitendo cha kufanikiwa kuliteketeza jengo la mahakama na kuunguza nyaraka muhimu za ushahidi, tukio hilo likiongozwa na mmoja wa mawakili wao aliyejulikana kwa jina la John Mbwambo, kiliwapa ishara na dalili kubwa ya ushindi dhidi ya kesi yao mbaya ya mauaji. Wakajiona kuwa ni viumbe wenye akili kuliko watu wengine duniani!
Je, nini kitafuata?
SONGA NAYO…
MADAKTARI wa Hospitali ya Amana wakiongozwa na Dk. James Mabula waliufanyia uchunguzi mwili wa mzee Ambrose Amlima na kugundua kuwa mlinzi huyo hakujinyonga, bali shingo yake ilivunjwa na baadaye kutundikwa kwenye kamba ili aonekane kama ni mtu aliyejinyonga mwenyewe.
Picha ya X-ray ya shingo ilionyesha mifupa ya shingo ikiwa imeachana kutokana na shingo yake kukunjwa, mishipa ya damu iliyopo shingoni ilikuwa imepasuka vibaya! Watu waliofanya tukio hilo walikuwa ni wataalam wa mauaji kwani hawakuacha alama yoyote ile mwilini mwake, iliaminika walivaa mipira mikononi wakati wa utekelezaji wa mauaji hayo.
Taarifa hiyo ya madaktari ilipounganishwa na tofauti ya mwandiko kwenye barua ambayo marehemu alidaiwa kuiandika na ule wa kwenye nyaraka mbalimbali zilizopatikana kwenye kampuni ya ulinzi aliyoifanyia kazi, zilikamilisha ushahidi kwamba kuna watu waliofanya mauaji hayo, hao ndiyo ilikuwa ni lazima wapatikane.
“Tutawapataje?” Wapelelezi waliulizana wakiwa ofisini kwao makao makuu ya jeshi la polisi.
“Turudi kwa mama ntilie aliyetuelekeza nyumbani kwa Ambrose, huyo lazima atakuwa angalau na taswira kichwani mwake ya gari lililowaleta wanaume wawili waliokwenda nyumbani kwa Ambrose jioni ya siku ya kifo chake!” Inspekta Masala ambaye sasa alikuwa ni sehemu ya timu ya upelelezi ya jeshi la polisi alisema.
“Ni wazo zuri, basi twendeni!”
Wote wakaondoka ofisini na kuingia kwenye magari, safari ya kuelekea mtaani kwa Ambrose ikaanza, haikuwapa shida kumpata mwanamke huyo ambaye baada ya kujitambulisha kwake kama wapelelezi alikuwa tayari kuwaeleza kila kitu huku machozi yakimbubujika, alidai mzee Ambrose alikuwa mteja wake mkubwa tena asiye na matatizo, aliyelipa madeni yake kwa wakati.
“Kifo chake kimeniumiza sana, alikuwa mtu mwema!”
“Pole sana!”
“Asante. “
“Unaweza kutueleza wale watu waliokuja kukuuliza mahali anapoishi siku moja kabla hajafa walikuwa na gari gani?”
“Sikumbuki rangi yake au aina!”
“Namba?”
“Hiyo niliiangalia, ingawa siwezi kuikumbuka yote, lakini ilianza na TXD!”
“Basi mama komea hapohapo, chukua hii shilingi elfu ishirini utakunywa soda!”
“Nashukuru sana, maelezo yametosha?”
“Kabisa, ukiongezea utakuwa unaharibu.”
“Haya asanteni, wakati wowote mkinihitaji nitakuwa tayari kuwasaidia, kifo cha mzee Ambrose kimeniuma mno, kwa kweli wanadamu hawana wema, wakamuua, wakamnyonga, kisha kumtundika darini aonekane amejinyonga bila ninyi kuniambia kwamba alinyongwa nisingejua, watu wote hapa mtaani wanaamini alijinyonga kwa sababu alichoma jengo la mahakama,” alisema mama huyo huku akikunja zile noti na kuzifunga kwenye kanga yake.
“Siyo hivyo, kuna siri kubwa sana imejificha juu ya mauaji haya, kuna uwezekano mkubwa tukakuhitaji mahakamani kuwatambua wauaji tutakapowakamata, si utazitambua sura zao?”
“Ndiyo!”
“Basi tulia!”
“Asanteni.”
Walichokifanya wapelelezi kwa wiki nzima baada ya kuachana na mwanamke huyo maarufu kwa jina la mama Fatuma, jina lake kamili likiwa ni Aziza Mrisho, ilikuwa ni kufuatilia usajili wa gari lenye namba TXD 33321, kwa msajili wa magari ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), haikuchukua muda mrefu kumpata, alikuwa ni Bw Juma Haji Omari, huyo ndiye aliyeliingiza gari hilo kutoka Japan miaka mitatu iliyopita, anwani yake na maelezo yote ikiwemo namba yake ya simu yalipatikana kwenye faili la gari hilo.
Kilichofanyika ni kumpigia simu, kazi iliyofanyika mara baada ya kutoka ofisi za mamlaka ya mapato, akapatikana na askari wakaomba kukutana naye kwenye Hoteli ya Serena wakijifanya ni wawekezaji wa kampuni ya simu kutoka China iliyokuwa inatafuta kampuni ya kuingia nayo ubia ili waanzishe kampuni tawi lao nchini Tanzania.
“Sawa kabisa, njooni tuonane hapo saa naneeee!” aliongea mwanaume huyo kwa lafudhi ya Kipemba.
“Tutakuwa pale saa saba na nusu tukikusubiri.”
“Jambo jema, inshallah!”
Saa nane kamili alifika na kukutana na askari hao, hakuna kati ya wapelelezi aliyejua wanakutana na mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Dole huko Zanzibar! Wote walipigwa na butwaa alipotoa kitambulisho chake kwa lengo la kuwashawishi wawekezaji, ikabidi kiongozi wa wapelelezi hao aamue kumweleza mheshimiwa ukweli bayana kabla hawajamtia pingu mikononi.
“Mheshimiwa unamiliki gari lenye namba TXD 33321?” Gilbert alimuuliza.
“Ndiyoooo, niliwahi kuimiliki gari hiyo lakini nikaiuza kwa Sheha wa Kianga miaka miwili iliyopita!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Sasa hilo gari limetumika kufanya mauaji na kuchoma jengo la mahakama ambalo umesikia habari zake kupitia vyombo vya habari!”
“Mungu wangu weeee! Walahiii sijui kitu mieeeee, hakyaniiiii tenaaa naweza kumpigia simu Sheha niliyemuuzia akapanda ndege sasa hivi kutoka Unguja ili aje apambane na tatizo lake…”
“Twende kituoni huko ndiko utampigia simu, akija kituoni na kukubali kwamba hilo gari alilinunua kwako wewe utaondoka!”
“Hili sasa limeshakuwa tatizo, mapaparazi wakipata taarifa hizi, hakyanani tena ndiyo nimeshakuwa kwenye ukurasa wa mbele na uchaguzi ndiyo umekaribia, naomba mnisaidie!”
“Twende kituoni kwanza!”
“Kosa langu sikubadilisha jinaaaa!”
Wakatoka hotelini na kuingia kwenye gari na kuendesha hadi makao makuu ya jeshi la polisi idara ya upelelezi ambako mheshimiwa aliwekwa chini ya ulinzi baada ya kumpigia simu sheha Abdallah Juma ili afike Dar es Salaam haraka kwa ndege, hicho ndicho kilifanyika, saa kumi na mbili na nusu jioni sheha Abdallah alifika makao makuu ya polisi kutoa maelezo yake.
“Ni kweli gari hili nililinunua kwa mheshimiwa lakini wiki mbili zilizopita nililiuza kwa wakili mmoja maarufu hapa Dar es Salaam anaitwa Mbwambo!”
Wapelelezi wakaangaliana, jina la Mbwambo ndilo lililokuwa jina la wakili aliyekuwa akiwatetea Dk. Viola na nduguye Vanessa, masikio yao hayakutaka kuamini kwamba wakili huyo ndiye aliyelipua jengo la mahakama na kumuua mlinzi mzee Ambrose Amlima baadaye nyumbani kwake.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia kwenye Gazeti la Championi Jumamosi.