Mabilionea wasio na huruma 77
WAKILI aliyeshindwa katika kesi ya mirathi ya DK Viola na Vanessa, akishuhudia utajiri mkubwa wa fedha zilizoachwa na wanawake hao hatari zikitua kwa Padri Silvanio na Sista Mariastela, anaamua kwenda kusomea ukachero, lengo likiwa ni kupata ukweli juu ya kilichotokea hadi watawa hao wawe hai wakati alikuwa ametoa fedha ili wauawe na yeye aurithi utajiri mkubwa wa dola bilioni mbili ulioachwa na Dk Viola na Vanessa. Ilimuuma sana kuwashuhudia watawa hao wakitinga mahakamani na kumpokonya tonge mdomoni huku akiamini tayari alishawaua akielezwa walichomewa ndani ya hoteli waliyokuwa wakiishi huko Santa Marta.
Baada ya masomo yake, akaenda Santa Marta kuutafuta ukweli wa nini kilichotokea katika nyumba walimochomewa moto. Ameambiwa siku chache kabla ya nyumba walimokuwemo watawa hao kuchomwa, walikifukia kisima kilichokuwemo ndani ya uzio wa nyumba hiyo lakini kabla ya hapo kuna siku walionwa wakitumbukiza mifuko miwili mikubwa ndani ya kisima hicho.
Askari wanapofukua kisima hicho kwa msaada wa wafungwa, wanaikuta mifuko hiyo ikiwa na mifupa ya binadamu wawili, wanakwenda kuipima vipimo vya DNA kujua ni akina nani. Je, itabainika mifupa hiyo ni ya binadamu gani? Kuna uhusiano gani kati ya kufukiwa kwa binadamu hao kisimani na kupatikana kwa Padri Silvanio na Sista Mariastela wakiwa hai? Au kuna siri gani imejificha nyuma ya pazia?
SONGA NAYO…
ULIKUWA ni mshtuko wa mwaka kwa kila mtu kuanzia Denis Crapton mwenyewe, mapadri, masista, polisi na mahabusu walioshiriki kukifukua kisima! Hakuna aliyetarajia wangekumbana na mifupa ya binadamu chini ya kisima hicho ambacho Padri Silvanio na sista Mariastela walidai mbwa alifia ndani yake na wakaamua kukifukia.
Historia aliyoitoa Katekista Mkongwe wa parokia hiyo Jeremia Gonzales kwa Denis Crapton kuwa aliwashuhudia Padri Silvanio na Sista Mariastela wakidumbukiza kitu usiku ndani ya kisima hicho, ndiyo ilimchanganya zaidi, ikamwondoa kwenye wazo kwamba mifupa waliyoitoa kisimani ilikuwa ni ya Padri Silvanio na Sista Mariastela.
“Haiwezekani mifupa hii ikawa ni ya kwao wakati mimi niliwaona wao wenyewe wakidumbukiza kitu kisimani!” aliongea Jeremia Gonzales.
“Kabisa.”
“Kuna watu waliwaua na kuwadumbukiza kisimani, sijui ni watu gani, pengine ni wale wageni waliowatembelea kabla ya tukio la kuwaka moto nyumba!”
“Inawezekana, waliwaua halafu wakawatupa kisimani, kisha ndipo nyumba ikachomwa moto wao wakiwa wametoroka maana hakuna mabaki ya mwili wa mwanadamu yaliyokutwa kwenye jengo lililoteketea, duniani hakuna moto wa kuunguza mpaka fuvu la kichwa liwe masizi!”
“Lazima walitoroka baada ya kuwaua watu waliowatupa kisimani.”
“Lakini ni akina nani nao waliowaua?”
“Kama nilivyosema inawezekana ni walewale wageni waliowatembelea.”
Denis Crapton alichanganyikiwa kabisa, isingewezekana mifupa ile iwe ni ya Padri Silvanio na Sista Mariastela wakati aliwaona kwa macho yake nchini Tanzania mahakamani na wakatangazwa na mahakama kama warithi wa utajiri wa marehemu Dk. Viola na nduguye Vanessa.
Matumaini yake yote yakabaki kwa kipimo cha DNA, alitaka kifanyike haraka ili aweze kutegua kitendawili kilichokuwa mbele yake, ilimradi Padri Patrick Renamos alishamhakikishia kwamba kama mabaki ya waliokutwa ndani ya kisima yalikuwa ni ya watumishi wa kanisa Katoliki lazima wangejulikana maana kanisa hilo nchini Columbia lilikuwa na utaratibu wa kutunza kumbukumbu za vinasaba vya DNA vya watumishi wote wa kanisa kuanzia mapadri hadi watawa.
“Hapa DNA ni lazima ili kutanzua kitendawili hiki.”
“Hakika!” mkuu wa polisi alijibu.
“Inaweza kufanyika hapa Santa Marta?”
“Hapana ni mpaka Bogota.”
“Duh! Kilometa nyingi za kusafiri.”
“Itabidi iwe hivyo.”
“Kwa hiyo inabidi tuondoke kwenda Bogota mara moja?”
“Haina shida, tupite kwanza kituo cha polisi niandike maelezo kisha niwasiliane na wakubwa.”
“Litakuwa jambo jema.”
Wakaondoka hadi Kituo cha Polisi cha Santa Marta ambako Inspekta Jarmine Lopez alifanya kama alivyokuwa amesema na kuwasiliana na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Bogota kwa njia ya redio, akiwataarifu juu ya kilichotokea kwenye mji wake.
Halikuwa tukio geni hata kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa nchi hiyo, kifo cha watawa wawili kilivuma mno dunia nzima. Kitendo cha kupatikana kwa mifupa iliyohisiwa kuwa ni yao kwenye kisima nyumbani kwao, ilimshtua mkuu wa jeshi la polisi na kumwomba Inspekta Jarmine abaki hukohuko Santa Marta, ingetumwa helikopta kumfuata haraka ili vikachukuliwe vipimo sahihi vya kwenda kuchunguza mabaki hayo.
“Sawa afande, tutasubiri!” alimaliza na kukata simu.
“Vipi?” Denis Crapton akauliza.
“Wanatuma helikopta.”
“Kweli?”
“Kabisa.”
Saa tatu baadaye helikopta ilitua mbele ya uwanja wa mpira uliokuwepo mbele ya kituo cha polisi, askari wanne wakashuka na kutembea hadi ndani ya kituo, nao walipoonyeshwa mabaki walibaki mdomo wazi. Wakachukua vipande vya mifupa na nywele kisha kuweka kwenye viboksi maalum, wakatoka wakifuatana na Denis Crapton, Inspekta Jarmine aliamriwa kubaki.
Helikopta ikaruka tena na kusafiri kwa saa mbili na nusu ndipo ikatua Bogota mbele ya makao makuu ya jeshi la polisi nchini humo, ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu jioni, ofisi nyingi zikiwa tayari zimekwishafungwa. Kilichofanyika ni Denis Crapton kutafuta hoteli ya kulala mpaka siku iliyofuata asubuhi ndipo wakakutana na kupeleka vipimo hivyo kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Columbia.
Alibaki Columbia kwa siku tatu bila majibu kutoka, siku ya nne ndipo akapigiwa simu na polisi akitakiwa afike kituoni kwa ajili ya kupewa taarifa ya majibu ya uchunguzi uliofanyika, Denis aliondoka hotelini bila kupiga mswaki wala kunawa na kwenda moja kwa moja ofisini kwa mkuu wa jeshi la polisi ambako alikaribishwa kwenye chumba cha mkutano na viongozi mbalimbali wa jeshi hilo.
“Kwa sababu wewe ni mpelelezi mwenzetu hatuna budi kukueleza kila kitu juu ya majibu haya.”
“Nina hamu kubwa ya kufahamu.”
“Mifupa iliyotolewa kwenye kisima tumewasiliana na Kanisa Katoliki baada ya majibu kutoka na wamethibitisha kwamba mifupa hiyo ni ya Padri Silvanio na Sista Mariastela!”
“Whaaaaat?” (Niniiii?) Denis Crapton alifoka kwa sauti huku akinyanyuka kitini na kutupa mikono yake huku na kule.
“Ni kweli kabisa, waliuawa na kutupwa kisimani.”
“Siyo kweli.”
“Kwa nini? Unabishana na sayansi?”
“Sibishani na sayansi hata kidogo lakini watu hawa mimi niliwaacha nchini Tanzania, nilikuwa na kesi nao, wakarithishwa utajiri wa dola bilioni mbili ambao nilitakiwa kurithi mimi, wakasababisha niache uanasheria na kwenda kusomea upelelezi ili tu nijue ukweli wa jambo hili, iweje leo eti wawe waliuawa na kutupwa kisimani wakati wako Tanzania wakiishi kitajiri? Huo ni uongo. “Hauhitaji kubishana na sayansi hata kidogo, jambo moja kubwa la kufanya ni kufuatilia huko Tanzania ikiwezekana tukupe barua ambayo utawakabidhi polisi wa kimataifa, Interpol, ukishafika huko, wakamatwe na kuchunguzwa vizuri, pengine kuna jambo lilifanyika ambalo sote hapa hatuwezi kufahamu!”
“Nipeni hiyo barua.” Denis Crapton alisema akionyesha hasira, moyoni mwake alikuwa amedhamiria kwenda kuutafuta ukweli nchini Tanzania kwa kukutana na Padri Silvanio na Sista Mariastela.
Siku iliyofuata asubuhi alikuwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kuelekea Dubai akitokea Bogota, huko alitarajia kuunganisha kwa ndege nyingine ya shirika hilohilo hadi Dar es Salaam, safari ilikuwa ikienda taratibu sana, alitamani awe kwenye jiji hilo na kukutana na Padri Silvanio na Sista Mariastela ili ajue ukweli wao.
JE, nini kilitokea jijini Dar es Salaam baada ya Denis Crapton kufika Hoteli ya Kilimanjaro ambako Padri Silvanio na Sista Mariastela walikuwa wakisaini mkataba wa kuuza mali zao zote ili waondoke nchini humo? Je, atawawahi? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

