Mabilionea Wasio na Huruma 42

WAGENI wiwili kutoka nchini Thailand, bwana Hui na Chu, waliokuja Tanzania kwa lengo la uwekezaji, tayari wameingia nchini Tanzania na kupokewa na Waziri wa Utalii na Biashara wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Jamhuri Azimio na Katibu Mkuu wake, Teofil Ezekia na viongozi mbalimbali ambao wamewapeleka ikulu kwa lengo la kuonana na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongea kisha kupata chakula cha mchana, ishara kwamba walikuwa wamekubalika.

Ndani ya ikulu umefanyika mkutano mfupi, waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wamefurika kutaka kuchukua picha na kuuliza maswali kutoka kwa watu hao waliojiita wawekezaji, jambo ambalo mpaka mwisho limekwenda sawia.

Chakula kinaandaliwa na wageni hao wanakula pamoja na rais wa nchi, kisha kusindikizwa na magari maalum kuelekea Serena Hoteli ambako wangepumzika wakisubiri jioni ya siku hiyo kula tena chakula na wafanyabiashara, viongozi mbalimbali ili watambuane zaidi.

Wanasindikizwa mpaka Serena Hoteli na kupokewa na taratibu zote kufanyika kisha kupelekwa mpaka katika moja ya vyumba vilivyokuwa hotelini hapo ili wapumzike, ni huko ndiko wanaanza kufikiria mchezo mzima namna walivyotoroka nchini Thailand na kurejea Tanzania kwa mwamvuli wa wawekezaji huku wakiwa katika sura tofauti kabisa, wanacheka na kujiona washindi, lakini ghafla mlango wa chumba chao unagongwa na wote wanashtuka.

Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

WAZIRI wa Utalii na Biashara wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jamhuri Azimio na Katibu Mkuu wake, Teofil Ezekia ambao walilazimika kuongoza msafara kuwasindikiza wageni wao hotelini baada tu ya kumaliza zoezi hilo, waliingia ndani ya magari yao na kurejea ikulu ili kuanza mchakato wa kuhakikisa dhifa iliyokuwa imeandaliwa na rais siku hiyo kwa ajili ya kuwakaribisha wageni, inakwenda kwa mpangilio uliotakiwa.

“Tanzania imepata bahati kubwa sana,” aliongea Waziri.

“Kweli kabisa mheshimiwa, kwanza wawekezaji wenyewe kwa inavyoonekana hawana makuu kabisa, ni watu wa kawaida, mimi huwa napenda mtu akiwa na fedha asijionyeshe.”

“Kama ilivyo kwa bwana Hui na Chu.”

“Eeeh! Tunatakiwa tusimamie kila hatua mpaka mwisho ili wasije wakaona kama wametupa fedha zao.”

“Hilo ni jambo la muhimu, naona mpaka rais mwenyewe amefurahi ajabu.”

“Sana, mpaka kuandaa dhifa ni ishara ya kuonyesha kwamba amekubali si kitu kidogo.”

“Mimi mwenyewe nimefurahi mno, uwekezaji wao utachangia pato la taifa letu lakini pia hata wapinzani wetu wataona ni jinsi gani serikali yetu inavyochangia kuhakikisha uchumi wetu unakua.”

“Ha! Ha! Haa, kiongozi wapinzani mara nyingi huangalia zaidi makosa na si mazuri.”

“Hilo kwangu si tatizo, hakujawahi kuwa na wapinzani wakasifia bila kutoa dosari, ila mimi naamini sana katika utendaji wa kazi zangu.”

“Vizuri mheshimiwa, naweza kuuliza swali?”

“Uliza tu.”

“Ulifanya nini kuwapata wawekezaji hawa?”

“Haikuwa kazi ngumu sana japo ilikuwa na changamoto kidogo lakini mwisho niliweza kuwashawishi na kukubali ili waje hapa nyumbani kuwekeza, ndipo wakaniambia kuwa walikihitaji Kisiwa cha Bongoyo, lakini pia mimi kama waziri ninalo jukumu la kuhakikisha natafuta wawekezaji ninaoamini wanaweza kuleta mabadiliko, kwa ufupi tu hicho ndicho kilichotokea .”

“Duh!” Katibu mkuu aliguna.

Yalikuwa ni maongezi ya waziri na katibu wake wakiwa ndani ya gari kurejea ikulu kwa ajili ya maandalizi ya sherehe iliyokuwa mbele yao.

Dakika tano tu tayari gari lilikuwa likiegesha kwenye ngome ya ikulu, waziri na katibu wake huku wakiwa wenye nyuso za tabasamu, wakateremka na kutembea kwenda kuungana na wenzao ambao waliwaacha hapo wakiendelea na taratibu zote za dhifa ya kitaifa iliyokuwa imeandaliwa na rais.

Mambo yalikuwa mengi na yote yalitakiwa kufanyika kwa wakati muafaka ili kwenda sawasawa na muda ambao ulipangwa, katibu muhtasi naye alikuwa kwenye simu akifanya mawasiliano na mashirika, makampuni, viongozi wa dini na wafanyabiashara kuwapa taarifa juu ya mwaliko huo.

Siku hiyo ikulu ilikuwa ikiwaka moto, ulinzi ukiimarishwa kwa hali ya juu ili tu kuhakikisha pasingekuwepo jambo baya lolote ambalo lingetokea kwa wageni hao muhimu waliokuwa wamekuja Tanzania kuwekeza, chakula na vinywaji vingi viliandaliwa, yote hiyo ikiwa ni kukamilisha ujio wa bwana Chu na Hui, wawekezaji muhimu kutoka nchini Thailand.

Wageni na watu mbalimbali walikuwa wamepata mwaliko ili tu kuongea na kutambulishwa ujio wa wawekezaji wawili matajiri ambao walitaka kuipeleka Tanzania mbele zaidi katika ukuaji wa kiuchumi. Kamati maalum iliyokuwa imeteuliwa ilihakikisha mambo yote yanakaa sawa, haikuwepo kasoro yoyote iliyoonekana.

Saa kumi na mbili na nusu juu ya alama, mambo yote yalishakamilika na baadhi ya wageni wachache walishaanza kuwasili, wao pia wakionyesha kufurahia mwaliko waliokuwa wameupata, walionekana katika makundi makundi wakiongea mambo fulani kisha kuachia vicheko na kugonganisha glasi zilizokuwa mikononi mwao.

“Sasa naona kila kitu kimekaa sawa kabisa, wageni wetu wameanza kuingia.”

“Rais?”

“Huyu hana tatizo, yuko tayari ni sisi kutoa tamko juu ya wageni wetu ambao wako hotelini kwamba ni muda gani wangewasili,” waziri aliongea kwa kujiamini.

Muda mfupi tu sauti ikasikika kwa mshereheshaji wa shughuli akiongea na kuwakaribisha wageni wote akiwataka kujisikia wapo nyumbani, pia akitoa pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri pamoja na waziri mhusika kwani walikuwa wamefanya kazi kubwa ambayo ilionekana ingeleta matunda bora muda mchache ujao. Magari mengi ya kifahari yaliyobeba watu ndani, yaliendelea kumiminika katika viwanja vya ikulu jioni hiyo.

***

“Ngo! Ngo! Ngo!” ulikuwa ni mlango wa chumba cha bwana Chu na Hui ukigongwa kwa nguvu, jambo lililokatisha maongezi yao na kufanya wabaki kimya kwa muda huku wakitazamana. Jasho jembamba likaonekana kutiririka miilini mwao, hofu ya ajabu ikafunika mioyo yao wasijue ni kitu gani cha kufanya.

“Nani?” bwana Hui aliyekuwa amejilaza kitandani akanyanyuka haraka na kuketi kisha kuuliza kwa kunong’ona.

“Sijui.” Chu akajibu naye pia akionekana kuwa katika wasiwasi, hawakuwa na majibu ya mtu aliyegonga mlango wakati huo kwani walifahamu wazi kwamba kama muda wa kuelekea ikulu ulikuwa umefika, ni lazima mtu aliyekuja kuwachukua angefika kwanza mapokezi kisha kujitambulisha nao kupigiwa simu wakielezwa juu ya ujio huo.

“Tufanye nini sasa?”

“Hakuna kufungua kwanza mpaka tujue ni akina nani,” ndivyo walivyojiambia na kubaki ndani ya chumba wakiwa kimya kabisa.

Mlango ukaendelea kugongwa na waliposikiliza vizuri walisikia hatua za watu wakitembea huku na kule na muda mfupi kurejea tena karibu na mlango kuendelea kugonga, jambo lililozidi kuwatia wasiwasi zaidi.

Wakiwa ndani ya chumba, waliendelea kushikilia msimamo wao wa kutofungua mlango na kusubiri kuona nini kingetokea. Wakasogelea dirisha lililokuwa chumbani hapo na kuchungulia upande wa nje.

“Turuke,” bwana Hui alisema akimzama mwenzake ambaye alionekana kukata tamaa kabisa.

“Kwa umbali huu hatutafika chini tukiwa hai.”

“Kipi bora kwetu, kuruka na kuanguka tukakamatwa tukiwa wafu au kukamatwa, binafsi siko tayari.”

Bila kujiuliza mara mbili wote wakalisogelea dirisha kisha kutupa macho yao chini ambako wangefikia baada tu ya kuruka, hawakuwa na uhakika kama wangenusurika.

JE, nini kitaendelea? Watafikia uamuzi wa kuruka kwa kuhofia kukamatwa na watu wanaogonga mlango? Je, ni akina nani hao? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

JIUNGE NA MICHEZO KIGANJANI TUMA NENO SPORTS KWENDA NAMBA 15778CHAMPIONI


Loading...

Toa comment