The House of Favourite Newspapers

Mabingwa Ndiyo Kwanza Tumeanza

0

“MABINGWA ndiyo tumeanza sasa!” Hiyo ni kauli ambayo ilitawala katika Dimba la Jamhuri, Dodoma kutoka kwa mashabiki wa Simba baada ya timu hiyo kupata ushindi wake wa kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

Simba walianza kwa mwendo wa kuchechemea kwa kudondosha pointi mbili mbele ya Biashara United kwa kutoka suluhu, lakini jana walirudisha tabasamu na hali ya kutamba kwa mashabiki wao baada ya kushinda bao 1-0 mbele ya Dodoma Jiji kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

 

Straika Meddie Kagere ndiye ambaye aliirejesha timu hiyo kwenye reli ya ushindi kwa kufunga bao pekee ikiwa ni baada ya kupita mechi tatu bila ladha ya ushindi. Kagere alifunga bao hilo dakika ya 69 akitumia pasi ya Chris Mugalu, aliyetoa pasi akiwa nje ya 18 na Kagere alipachika bao hilo kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 likamshinda mlinda mlango wa Dodoma Jiji, Hussein Masalanga.

 

Kagere alipewa kadi ya njano kutokana na kuvua jezi wakati akishangilia bao hilo.

 

Katika mchezo wa jana, Gomes hakuwa na namna kwa kuwa alifanya mabadiliko ya lazima mara tatu baada ya nyota wake, Kennedy Juma kuumia baada ya kupigwa kiwiko na mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Anwar Jabir. Nafasi yake ilichukuliwa na beki Inonga Baka. Tukio hilo lilisababisha Anwar aonyeshwe kadi nyekundu dakika ya 44 na mwamuzi Joseph Akamba.

 

Kocha huyo kwa mara nyingine tena alilazimika kumtoa Pape Sakho kutokana na kuumia na kumuingiza Rally Bwalya pia Taddeo Lwanga akatolewa baada ya kuchezewa faulo na Salmin Hoza ambaye alionyeshwa kadi ya njano. Aliingia Meddie Kagere badala yake. Duncan Nyoni naye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Yusuph Mhilu.

 

Kwa matokeo hayo, Simba kwa sasa wanafikisha pointi nne ambazo zinawapa nafasi ya kurejea kwenye nafasi ya kutetea ubingwa wao ambao waliutwaa msimu uliopita. Jitihada za Simba kusaka ushindi zilijibu kipindi cha pili baada ya Gomes kuwatumia nyota wake wa kazi katika safu ya ushambuliaji John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu.

 

Washambuliaji hao walikuwa na moto msimu uliopita ambapo Mugalu alifunga mabao 15, Kagere alitupia mabao 13 na Bocco mabao 16.

 

Dodoma Jiji walikwama kutumia nafasi ambazo walizitengeneza kupitia kwa Cleophance Mkandala pamoja na Seif Karihe ambao walikuwa ni mwiba kwa mchezo wa jana.

 

Katika mchezo mwingine, uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma, Biashara United ilikutana na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ruvu Shooting kwa bao lililofungwa na Rashid Juma dakika ya 47.

ISSA LIPONDA, Dodoma

Leave A Reply