The House of Favourite Newspapers

Mabosi Simba Wakutana Kuijadili Yanga

0

BODI ya Wakurugenzi ya Simba imekuwa na vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya klabu hiyo ikiwemo ishu ya meneja na kocha mpya wa makipa wa timu hiyo ikiwa ni pamoja na mchezo wao wa watani wa jadi dhidi ya Yanga utakaochezwa Novemba 7, mwaka huu.

 

Simba hivi karibuni imeamua kuachana na meneja wake, Patrick Rweyemamu na kocha wa makipa, Mwarami Mohammed kutokana na kuhitaji kufanya maboresho ya benchi hilo kutokana na kuona mapungufu yaliyojitokeza.

 

Hivi karibuni, Simba iliwashtua mashabiki wao baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo dhidi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting kwa kufungwa bao 1-0 kila mechi.

Taarifa ambazo Championi Jumamosi imezipata kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, Bodi ya Wakurugenzi chini ya bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ imekuwa ikikutana mara kwa mara ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa katika timu hiyo baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo kabla ya kuwavaa watani wao Yanga ikiwa ni pamoja na kuamua juu ya meneja na kocha mpya wa makipa.

 

“Wakati wowote kuanzia sasa meneja mpya atapatikana pamoja na kocha wa makipa uongozi upo katika mchakato wa kuhakikisha unaziba nafasi hiyo haraka iwezekanavyo ambapo bodi imekuwa ikikutana mara kwa mara kwa lengo la kupata watu sahihi watakaokaa benchi pia kuelekea mechi dhidi ya Yanga.

 

“Lengo kubwa ambalo limefanyika ni kuhitaji kufanya maboresho katika benchi la ufundi ili kuwa imara zaidi na si vinginevyo na mchakato unaendelea kufanyika siku si nyingi atatangazwa meneja mpya,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Katibu wa Simba, Arnold Kashembe aweze kuzungumzia ishu hiyo alisema hawezi kuzungumzia kwa muda huo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao.

Stori: Khadija Mngwai, Dar es Salaam

Leave A Reply