The House of Favourite Newspapers

MACHO YOTE SASA NYUMBA

0
Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo (kulia) akimkabidhi funguo Mshindi wa Nyumba, Nelly Mwangosi.

WAKATI siku za kuchezeshwa kwa droo kubwa katika Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili zikikatika kwa kasi, macho yote ya wasomaji wa magazeti ya Global Publishers yameelekezwa kwenye zawadi hiyo kubwa ya nyumba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu kutoka sehemu mbalimbali nchini, wasomaji kutoka mikoa ya Mwanza, Ruvuma, Mbeya, Lindi na Arusha, walisema baada ya kutopata zawadi yoyote katika droo tano zilizochezeshwa, macho yao sasa ni kwenye zawadi hiyo ya nyumba.

 

 

Shigongo akimkabidhi hati ya nyumba Mshindi wa Nyumba, Nelly Mwangosi.

“Yaani kama mimi ninapiga simu kutoka hapa Lindi, akili yangu ni juu ya nyumba tu, nimejitahidi nikakata kuponi nyingi na hata sasa ninaendelea kupata kwa kila nakala inayotoka, nadhani hii ni nafasi yangu kuibuka mshindi,” alisema Stanslaus Mapinga, wakati akiulizia kama kuna utaratibu mpya juu ya bahati nasibu hiyo inayoendeshwa na Global Publishers inayochapisha Magazeti ya Championi, Uwazi, Ijumaa Wikienda, Risasi, Amani na Ijumaa.

Msomaji mwingine kutoka Mwanza, Shitindi Kemis, amesema hakuna mtu aliyekata kuponi za bahati nasibu ya shinda nyumba ambaye hafikirii kuhusu zawadi hiyo kubwa ambayo ina thamani ya mamilioni ya shilingi.

 

“Ninachoweza kukuambia ni kwamba hakuna mtu mwenye kuponi ambaye hafikirii kuhusu hiyo nyumba. Hivi ni nani asiwazie nyumba ya mamilioni ya shilingi kuipata kwa shilingi mia tano tu? Kwa kweli mimi binafsi naona hili zoezi linachelewa, bora huu mchezo uishe tu tuwaze vitu vingine maana akili yote inatembea nyumba, nyumba,” alisema Kemis.

Nelly, mama wa watoto wawili ambaye ni mkazi wa Iringa, alibahatika kuibuka mshindi katika droo ya Shinda Nyumba iliyochezeshwa Juni, mwaka jana lakini kwa kuwa ni mjasiriamali huko Iringa anakoishi, aliamua kuipangisha nyumba hiyo na fedha anazopata, zinamsaidia kulipia ada za watoto wake wawili, mmoja akiwa kidato cha pili na mwingine akisoma chekechea.

Ofisa Usambazaji wa Global Publishers, Jimmy Haroub (kushoto) akiwaelekeza wasomaji jinsi ya kujaza kuponi za shinda nyumba.

Ofisa Masoko wa Global Publishers, Yohana Mkanda, alisema jana kuwa huu ni wakati muafaka wa wasomaji wote waliokata kuponi zao kuziwasilisha kwa mawakala wao nchi nzima.

“Nyumba siyo kitu kidogo, kila mtu angetamani kumiliki nyumba jijini Dar es Salaam, sasa hii ni fursa adimu ambayo haikulazimu kuwa na mamilioni ya kujenga au kununua, ni kiasi cha kwenda kwa muuza magazeti yeyote, popote alipo Tanzania na kujipatia mojawapo ya magazeti yetu ili ujiweke katika nafasi nzuri ya kuwa mmoja wa wamiliki wa nyumba bora nchini,” alisema Mkanda.

Nyumba hiyo ambayo kama ile ya kwanza imejengwa Dar es Salaam, itakuwa ni ya kisasa ikiwa na samani zote ndani yake, kiasi cha kumfanya mshindi kuingia na begi lake tu ili kuanza maisha. Bahati Nasibu hii ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili imedhaminiwa na Kampuni ya Premier Bet.

Leave A Reply