The House of Favourite Newspapers

MACHOZI! KILICHOMPATA MTOTO HUYU LAZIMA ULIE !

MACHOZI! Unajiona una matatizo? Taarifa ikufikie kuwa, humu duniani kuna watu wanateseka zaidi yako na kama ukisikia mikasa yao, lazima ulie, Risasi Mchanganyiko lina mkasa wa kusikitisha.

 

MAUMIVU SIKU 1095

Hicho ndicho kilichompata mtoto Aryan Ally mwenye umri wa miaka mitatu, mkazi wa Mbezi-Beach jijini Dar ambaye yupo kwenye mateso makuu na maumivu aliyodumu nayo yapata miaka mitatu, sawa na siku 1095.

 

Aryan akiwa na umri huo mdogo alipita, amepita na anapita kwenye kipindi kigumu cha maumivu baada ya mwili wake kupooza. Aryan alipooza mara tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo kufuatia kugundulika ana tatizo la moyo.

 

MAMA ARYAN ASIMULIA

“Jamani mwanangu, ee Mungu naomba umsaidie,” ndivyo alivyoanza kusimulia mama wa Aryan, Glory Charles.

 

AZALIWA AKIWA VIZURI

Mama Aryan alisimulia kuwa alimzaa mwanaye huyo akiwa vizuri tu, bila kujua kama ana tatizo lolote. Lakini alipokuwa akimpeleka kliniki kwenye Hospitali ya Lugalo jijini Dar ndipo daktari mmoja akagundua tatizo lake.

 

“Nilimzaa mwanangu akiwa na afya njema kabisa, lakini kuna siku nilimpeleka kliniki, daktari mmoja akagundua kuwa mwanangu akilia mdomo unakuwa mweusi. “Kingine aligundua kucha zinakuwa za bluu ndipo aliponishauri nikamfanyie kipimo cha moyo,” alisimulia mama Aryan.

 

ASHAURIWA KUFANYIWA UPASUAJI

Akiendelea kusimulia, mama huyo alieleza kuwa baada ya kumfanyia kipimo hicho, mwanaye aligundulika kuwa na valvu za moyo ambazo hazipitishi damu vizuri hivyo ikashauriwa kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya kumtengenezea njia nyingine ili iweze kupita vizuri.

 

“Baada ya kuonekana tatizo hilo kwa mwanangu, niliumia sana kwani mtoto wangu wa kwanza alipoteza maisha pia kutokana na tatizo la moyo hivyo walivyoniambia kuhusu Aryan kutakiwa kufanyiwa upasuaji, nilikubali na nikaanza kwenda kliniki Muhimbili.

 

“Siku yake ya kufanyiwa upasuaji ilipofika, alifanyiwa akiwa na umri wa miezi kumi,” alisema mama Aryan. Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji, mtoto wake huyo akiwa bado chumba cha uangalizi maalum (ICU) alipooza. “Baada ya muda alitolewa ICU na kuanza kupatiwa matibabu mengine ili kuona kama anaweza kurudi katika hali yake ya kawaida.

 

“Tofauti na matarajio, bahati mbaya haikuwa hivyo kwani mwanangu alikuwa ameshapooza. “Nilikaa hospitalini hapo, baadaye nilitoka, lakini mtoto alikuwa bado amepooza. “Tukaanza kumfanyia mazoezi katika Hospitali ya CCBRT maana hakuweza tena kukaa wala kusimama kama ilivyokuwa huko nyuma,” alisema mama huyo.

AMETESEKA MIAKA MITATU

Mama Aryan alisema kuwa, hadi sasa, mwanaye ameteseka yapata miaka mitatu mtoto wake kidogo anaanza kuleta matumaini, lakini kuna kifaa anatakiwa akitumie ili kuweza kumsaidia zaidi kinaitwa standing frame au gait trainer ili imsaidie aweze kurudi kwenye hali yake ya zamani kwa sababu bado ni mdogo na kuna uwezekano wa kurudia hali yake.

 

“Ninaamini kabisa mtoto wangu akipata vifaa hivyo atarudi kama zamani maana ninavyompeleka kwenye mazoezi hali yake naona kabisa anapata nafuu na shingo imeshaanza kukaza hivyo ningepata hivyo vifaa ningeshukuru sana,” alieleza mama huyo kwa machungu.

 

KUTOA NI MOYO

Kutoa ni moyo na si utajiri. Kama umeguswa kwa namna moja au nyingine na tatizo la mtoto Aryan, unaweza kumchangia chochote kupitia kwa mama yake huyo ili aweze kununua vifaa hivyo vitakavyomsaidia mtoto wake kurejea tena katika hali yake. Unaweza kuwasiliana na mama yake kwa namba yake ya mkononi 0715795944

Stori: IMELDA MTEMA, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.