The House of Favourite Newspapers

Macron: Nani anaamini Urusi ya leo itaishia tu Ukraine?


Rais Emmanuel Macron amewakumbusha viongozi wenzake kwamba “hatma ya Ulaya haiwezi kuamuliwa na Washington au Moscow” na kuwatanabahisha kuwa enzi ya unyonge iliyoshuhudiwa tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin mwaka 1989 imefikia mwisho.

Amekumbusha kuwa hivi sasa Urusi inatumia asilimia 40 ya bajeti yake ya taifa kwenye shughuli za kijeshi ikiwa na mipango ya kulitanua jeshi lake lifikie wapiganaji 300,000 mwaka 2030, kuunda vifaru 3,000 na ndege 100 za kivita. “Nani anaamini kuwa Urusi ya leo itaishia tu Ukraine?” ameuliza kiongozi huyo wa Ufaransa.

Macron pia amegusia wasiwasi wa kusambaratika kwa ushirika wa nchi za magharibi tangu kurejea Trump madarakani akisema anaamini “Washington itaendelea kubakia upande” wa marafiki zake wa miaka mingi lakini ni sharti Ulaya ijiandie iwapo imani hiyo haitokuwa ya kweli.
Kiongozi huyo amemtahadharisha Trump kuwa amani ya Ukraine “haipaswi kufikiwa” bila kupima taathira zake na kwamba usitishaji mapigano haufai kuwa legelege.

Pia Macron amerejea ahadi yake ya kutumwa vikosi vya nchi za Ulaya kwenda kusimamia makubaliano yoyote ya amani yatakayofikiwa kati ya Urusi na Ukraine ili kuhakikisha Urusi haitamvamia tena jirani yake huyo.

Vilevile ametangaza kwamba Wakuu wa Majeshi wa nchi za Ulaya watakutana wiki ijayo mjini Paris kujadili namna ya kuisaidia Ukraine pindi mkataba wa amani utakapopatikana.