The House of Favourite Newspapers

Madai: Khashoggi Aliuawa Ndani ya Ubalozi wa Saudia

images-jpg.896247

MWANDISHI wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi,  huenda alirekodi tukio la kifo chake kwenye saa yake aina ya Apple Watch wakati alipoingia katika ubalozi wa Saudia jijini Instabul, Uturuki, siku ya Oktoba 2 mwaka huu, limesema gazeti moja la kila siku la nchini Uturuki.

Matukio ya “kuhojiwa, kuteswa na kuuawa kwake yalikuwa yamerekodiwa na kupelekwa kwenye simu na akaunti yake ya iCloud,” shirika la utangazaji la CNN lilinukuu gazeti binafsi la kila siku la Sabah. Lilisema mazungumzo ya waliohusika katika mauaji hayo yalirekodiwa.  Vyombo vya usalama vinavoongoza uchunguzi, vililipata faili husika lenye sauti ndani ya simu ya Khashoggi ambayo alimwachia mchumba wake, aitwaye Hatice Cengiz.

 

Baada ya kuiona saa hiyo, wauaji wa mwandishi huyo walijaribu kuifungua kwa kutumia majina mbalimbali ya siri wakashindwa hadi walipotumia alama za vidole za Khashoggi ambapo walifuata baadhi ya mafaili husika, liliripoti Sabah.

Hata hivyo, kampuni ya Apple haiorodheshi alama za vidole kama moja ya ufanyaji kazi wa saa za Apple Watch ambapo mwakilishi kutoka kampuni hiyo aliithibitishia CNN kwamba saa hizo hazijumuishi alama hizo.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Abdulaziz bin Saud bin Naif bin Abdulaziz, alikanusha nchi yake kumwua Khashoggi, akisema huo ni uzushi usio na msingi dhidi ya ufalme wa nchi yake.

 

Ijumaa iliyopita, chanzo kimoja kiliiambia CNN kwamba serikali ya Uturuki ina uthibitisho wa sauti na video unaoonyesha Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudia.

 

Ushahidi huo uliotolewa na  chanzo cha intelijensia cha Magharibi kilionyesha kwamba kulikuwa na mapambano ndani ya ubalozi huo ambayo yalisababisha kuuawa kwa mwandishi huyo.

 

Khashoggi, mwandishi wa gazeti la The Washington Post, alikwenda kwenye ubalozi huo kupata hati ambazo zingemwezesha kumwoa mchumba wake  wa Kituruki Hatice Cengiz, lakini tangu siku hiyo hajaonekana.

Comments are closed.