The House of Favourite Newspapers

Madai mazito… AMKATA MKEWE SHINGO AKITUBU“

MUME wangu kama nimekukosea nisamehe,” mwanamke mmoja, Pendo Patrick (30) mkazi wa Kijiji cha Kakola, Kata ya Bulyanhulu, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga amedai kutubu kwa mumewe kabla ya kukatwa na shoka shingoni.  Risasi Mchanganyiko liliambiwa hivi karibuni na kutafakari sababu za mwanamke huyo kujeruhiwa huko vibaya na kuziona zina makengeza ingawa yeye anamtuhumu mumewe aitwaye Paul Matogolo (36) kuwa ndiye aliyemfanyia ukatili huo, kutokana na kukasirishwa na hatua yake ya kununua kiwanja.

“Tumekuwa tukiishi maisha ya nyumba za kupanga; mimi jambo hilo limekuwa likiniumiza sana. Nikaamua kuanza kutafuta fedha kimyakimya ili niweze kununua kiwanja na kweli nikafanikiwa, lakini nilipomwambia mume wangu kuwa nimenunua kiwanja na kumshauri tuanze mkakati wa kujenga akakasirika.

“Nilimweleza namna nilivyopata fedha za kununua kiwanja lakini hakuniamini,” alisema Pendo na kuacha maswali iweje mume huyo akamsirike mkewe kununua kiwanja cha familia?

PENDO ANAENDELEA KUSIMULIA

Aidha, Pendo aliendelea kusimulia kuwa, kilichochochea hasira za mumewe juu ya hatua yake ya kununua kiwanja ni madai ya Matogolo kuchekwa na wanaume wenzake kijiweni kwamba anaishi maisha ya ‘Marioo’ yaani kulelewa na mwanamke. “Aliniambia kitendo changu cha kununua kiwanja bila kumshikirisha kimemdhalilisha kwa wenzake na akasema atanikomesha ili aibu imtoke.

“Nikamwambia, mume wangu kiwanja hicho si changu ni cha familia tuanze kukijenga, hakunielewa, kila siku ukawa ugomvi,” alisema Pendo akirejea mazungumzo kati yake na mumewe ambaye ametoweka na hivyo kulifanya gazeti hili lisipate uhakika wa maelezo hayo na kuyaacha kuwa ni tuhuma dhidi ya mwanamke huyo kwa mumewe ambazo hazijathibitishwa.

SIKU YA TUKIO ILIVYOKUWA

Akisimulia siku ya mkasa ambayo (tarehe haikumbuki) lakini ni mwishoni mwa mwezi uliopita, Pendo alisema kwamba majira ya saa mbili usiku wakati akitoka nyumbani kwake kuelekea kwenye duka la dawa analofanyia kazi alishangaa kumuona mtu aliyemtaja kuwa ni mumewe akitokea kichochoroni. “Nilimuona ana shoka mkononi, akanisogelea, nikamsalimia lakini hakuitika, nilipomuuliza kuna nini akaniambia ananiua, nikajaribu kumuomba msamaha ili kumtuliza hasira lakini hakunisikiliza.

“Ghafla akanikata shingoni na shoka, nikaanguka na kupoteza fahamu, kilichoendelea sikukifahamu tena,” alidai Pendo akizidisha tuhuma kuwa aliyemkata shoka siku ya tukio alikuwa ni mumewe jambo ambalo halijathibitishwa kwa sababu mtuhumiwa hajapatikana na vyombo vya usalama vinaendelea kufanya upelelezi na kumsaka Matogolo.

Aidha, Pendo aliongeza kuwa baada ya kukatwa shingoni na kuanza kuvuja damu nyingi, mtuhumiwa wake aliamini ameshamuua, hivyo kuamua kutoweka kusikojulikana na kumuacha yeye chini ambapo baadaye alipata msaada wa wasamaria waliomchukua na kumkimbiza katika Kituo cha Polisi Bugarama ambako alipatiwa Fomu Nambari 3 ya Polisi (PF3) kwa ajili ya matibabu.

“Baada ya hapo walinikimbiza Hospitali ya Bugarama ambako kwa kweli nawashukuru mno madaktari walinihudumia vizuri na kufanikiwa kuokoa maisha yangu. “Sina cha kuwalipa, ila nikikaa nikifikiria watoto wangu wangekuwa wapi kama mimi ningekufa na baba yao kama hivyo kakimbia?” alihoji Pendo kwa huzuni na kutokwa machozi, kisha kumshukuru Mungu.

HALI YA PENDO YAENDELEA VIZURI

Akizungumza na mwandishi wetu kuhusu hali yake baada ya kujeruhiwa huko, Pendo alisema kuwa kwa sasa anaendelea vizuri kutokana na matibabu bora anayopata. “Angalia hii picha (Pendo anamwonesha mwandishi wetu picha yenye jeraha kubwa shingoni aliyopigwa siku ya tukio) unadhani kama si uhodari wa madaktari na mkono wa Mungu ningepona?

“Nilishonwa nyuzi nyingi sana na jeraha lilikuwa kubwa, nilipopata nafuu na watu kunionesha sikuamini kama nimepona,” alisema Pendo huku akimuonesha mwandishi picha mbalimbali za tukio lake tangu siku ya kwanza hadi alivyo hivi sasa ambazo chache zimetumika ukurasa wa mbele wa gazeti hili.

AOMBA ULINZI WA POLISI

Kutokana na mtuhumiwa kutokutiwa nguvuni, mwanamke huyo mwenye watoto wawili, ameliomba jeshi la polisi kuzidisha uchunguzi na kulinda usalama wake kwa vile mtuhumiwa anaweza kurejea na kumfanyia unyama mwingine.

“Naishi kwa wasiwasi, angekuwa amekamatwa ingekuwa nafuu lakini kwa kuwa kakimbia naona kama anaweza kurudi kunimalizia endapo atasikia kuwa siku hiyo sikufa,” alisema Pendo. Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao alisema tukio hilo halijamfikia na kuahidi kulifuatilia kwa karibu.

MAUAJI YA WANANDOA TISHIO

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mauaji hasa wanawake yatokanayo na migogoro ya wanandoa nchini yamekuwa yakiongezeka jambo ambalo limekuwa likizua hofu. Ongezeko hilo la mauaji limekuwa likiwaibua baadhi ya watetezi wa wanawake na jamii kwa jumla na kutoa hoja ya kufanyika kwa makongamano ya kitaifa yenye lengo la kuzungumzia tatizo hili la mauaji na kulipatia ufumbuzi.

Hivi karibuni mwanamke mwingine Naomi Marijani mkazi wa Kigamboni, Dar alidaiwa kuuawa na mumewe kisha mwili wake kuchomwa moto kwa magunia mawili ya mkaa, tukio ambalo limegusa hisia za watu wengi.

Comments are closed.