MADAI MAZITO ASKARI WAUA RAIA KWA MAPANGA

ASKARI wa Maliasili eneo la Kola, Kisarawe Mkoani Pwani, wameangushiwa madai mazito ya kumuua raia mmoja aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Yusuph (37) kwa kumkata mapanga huku mwingine aitwaye John Mwaluko akijeruhiwa vibaya. 

 

Tukio hilo lilitokea Mei 14, mwaka huu ambapo inadaiwa kuwa, rai hao walikuwa eneo la maliasili wakichoma mkaa ndipo askari hao walipowavamia na kuwapa kibano kilichosababisha mauaji. Akizungumzia tukio hilo, majeruhi John alisema kuwa, siku hiyo kutokana na hali ngumu kimaisha waliingia kwenye eneo hilo na kukata miti kwa ajili ya kujitafutia riziki kupitia kuchoma mkaa na ndipo walipokutwa na masaibu hayo.

 

“Tulikuwa watatu tunaendelea na shughuli za kukata mkaa kwa ajili ya kijikimu kimaisha, tulienda kwenye sehemu ya kupumzikia ambayo ndio huwa tunatumia kupikia na kuhifadhi vifaa vyetu, ilipofika mida ya saa tano walikuja watu wakiwa na virungu na mapanga, ikabidi sisi tusikimbie.

 

“Mwenzetu mmoja (mdogo wa marehemu) alifanikiwa kuwakwepa lakini mimi na mwenzangu aliyefariki walitukamata na kutuambia tuwatoe na ‘kitu kidogo’, sisi tukawaambia hatuna kitu.

 

“Wakaanza kutupiga na panga za ubapa, baadaye wakageuza kwenye makali, wakatukata kwenye miguu na kuanza kutukanyaga mwilini. “Walienda sehemu tuliyokuwa tumehifadhi vitu vyetu wakavichukua vyote. Baada ya kuona tuko hoi, wakaondoka huku wakimuacha mwenzangu damu zinamvuja sana kwa sababu walimkata eneo la mshipa mkubwa mguuni.

 

“Tukawa tunagalagala tu pale chini, kwa kuwa tulikuwa tumeumia hatukuweza kupeana msaada ila mwenzangu damu ilivuja sana, ilikuwa inatoka kama bomba, mara nikamuona amezidiwa. “Kwa bahati nzuri yule mwenzetu aliyekuwa amekimbia alirudi mida ya saa kumi na moja jioni akaja na pikipiki akatuchukua. Kwa kuwa mimi nilikuwa na nafuu nikakaa nyuma, mwenzangu nikampakata tukafungwa mpira na kuanza safari ya kuondoka eneo hilo.

 

“Tukiwa njiani mwenzangu alikata roho, mimi sikumwambia dereva wa pikipiki, nilihisi angeogopa. “Tulipofika ofisi ya Mtendaji ya Kifuru, tuliwekwa pale mimi nikiwa na maumivu makali na mwenzangu alishapoteza maisha, ndipo mtendaji akasema anawasubiri polisi waje wanipeleke hospitali na kuchukua mwili.

 

“Lakini yule dereva akasema ni bora aniwahishe mimi hospitali, ndipo aliponichukua na kunipeleka, tulipokuwa tunaelekea hospitali, tuliliona gari la polisi mwenzangu akalisimamisha na polisi wakatuuliza kama wagonjwa waliokuwa wanawafuata ni sisi, tukawajibu ndiyo, wakanichukua na kunipeleka Hospitali ya Kisarawe ila tukawaambia kuwa maiti ipo kwenye ofisi ya Mtendaji.

 

“Baada ya hapo waliufuata mwili na kuuleta katika chumba cha kuhifadhia maiti hapohapo Hospitali ya Kisarawe,”alimalizia kusema majeruhi huyo. Baba mzazi wa marehemu, Yusuph Paul alisema alipata taarifa kutoka kwa rafiki yake aitwaye Nyang’asa akimwambia kuwa mwanaye ameuawa na askari wa wanyama pori. “Nilikuwa nyumbani kwangu maeneo ya Chanika, akaja rafiki yangu na kuniambia mwanangu ameuawa.

 

“Ikabidi mimi na ndugu zangu tuende huko Kisarawe ili tuweze kujua nini kimempata mwanangu, tulipofika pale tulionana na wahusika wakatuambia kuwa ni kweli waliwatuma hao askari wao lakini hawakuwaambia kuwa waue, waliwaambia wawakamate watu ambao wapo huko kwenye msitu.

 

“Hata hivyo walionesha busara kwa kushirikiana na sisi kwa hali na mali kwenye mazishi ya mpendwa wetu tukijua wamekiri kosa na watakuwa na sisi kwenye kipidi hiki kigumu. “Baadaye wakawa wanatuchengachenga huku baadhi ya maafisa wakisema hawana uhakika kama waliofanya tukio hilo ni askari wao.

 

“Kwa kweli tuko kwenye wakati mgumu sana. Huyu marehemu ameacha mke na watoto wadogo sana ambao wanahitaji matunzo, mimi mwenyewe nimeshazeeka, nilikuwa namtegemea huyo huyo marehemu, nitafanyaje miye? Naomba serikali inisaidie ili niweze kupata haki kwa hiki kilichotokea,” alisema baba huyo kwa masikitiko.

 

NDUGU WACHARUKA

Uwazi ambalo lilifanikiwa kufika msibani lilifanikiwa kuongea na baadhi ya ndugu wa marehemu ambao walisema kuwa, hawakubali kilichotokea kipite hivi hivi bila haki kutendeka.

 

“Huyu marehemu ni kaka yangu kabisa, kifo chake kimeniuma sana ila nitapambana mpaka haki ipatikane. Hakuna kosa kubwa walilofanya kwani walikuwa wakijitafutia riziki, na kama walikuwa wamefanya kosa, si wangewapeleka kwenye vyombo vya sheria kuliko kuua.

 

“Namuomba Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani atusaidie ili wale waliohusika kwenye tukio hili wachukuliwe hatua stahili,” alisema ndugu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Jackson. Uwazi lilifanikiwa kumpata Kamanda wa Mkoa wa Pwani, ACP Nyigesa Wankyo ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanawashikilia askari wawili wa wengine wawili wanaendelea kuwatafuta.


Loading...

Toa comment