The House of Favourite Newspapers

MADAI MAZITO BOSI AFANYA UKATILI RPC

MBEYA : Ni ukatili mzito! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya watu wanne akiwemo bosi mmoja kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa madai ya kumjeruhi kwa kumchoma visu vya moto mfanyakazi wake aitwaye Godfrey. 

 

Imedaiwa kuwa bosi wa mfanyakazi huyo ndiye aliyeongoza ukatili huo ambapo inadaiwa walianza kumfungia ndani ya chumba kisha kumchoma moto sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia visu na mapanga vilivyowekwa kwenye moto mkali Machi 22 mwaka huu.

 

Kama hiyo haitoshi, inadaiwa baada ya kufanya unyama huo, watu hao walimpaka pilipili na chumvi katika majeraha na kumsababishia maumivu makali kijana Godfrey, mkazi wa Mtaa wa Sokomatola, Kata ya Maendeleo jijini Mbeya. Mwenyekiti wa Mtaa, Boniphace Siame alisema tukio hilo lilitokea siku hiyo ya Machi 22, saa 11 alfajiri nyumbani kwa mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Adam, mkazi wa Sokomatola.

Siame alisema alipata taarifa saa moja asubuhi na kwenda kwenye tukio, alipofika alimkuta majeruhi katika hali mbaya akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili na amefungiwa katika chumba huku akiwa amefunikwa na blanketi.

 

“Kutokana na hali ya mgonjwa kuwa tete nilimwamuru bosi wa kijana huyo ambaye ni mfanyabiashara maarufu mtaani hapo kumpeleka mgonjwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na mimi kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kati Mbeya,” alisema Siame.

 

Akaongeza: “Baada ya kutoa taarifa Polisi walimkamata mfanyabiashara huyo na wenzake watatu wanaodaiwa kushirikiana kumtesa kijana huyo wakimtuhumu kujihusisha na vitendo vya wizi.” Jumbe Hassan Mapunda ni mjumbe wa mtaa huo alisema walifuatilia maendeleo ya afya ya mgonjwa lakini walishangaa kuona baadhi ya ndugu wa watuhumiwa wakimhudumia mgonjwa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Maendeleo, Modest Shiyo alisema alishangazwa na ukatili uliofanywa na mfanyabiashara huyo na kuliomba Jeshi la Polisi kufuatilia kwa karibu ili kuona haki inatendeka.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Watuhumiwa wa unyama huo tunawashikilia,” alisema Kamanda Matei na kuongeza kuwa uchunguzi wa suala hilo unaendelea.

‘MAHAKAMA’ Yamuhukumu BOCCO Kukosa PENALTI – SIMBA VS TP Mazembe

Comments are closed.