Madai Mazito… Mjeshi Amuua Msanii Kinyama

DAR ES SALAAM: DAMU, majeraha na jasho vilionekana mwilini mwa Elius Mathew (28) msanii wa maigizo na mkazi wa Kwalulenge, Yombo Buza, Temeke, Dar es Salaam baada ya kudaiwa kupewa kipigo kikali na mtu aliyedaiwa kuwa ni mwanajeshi hadi baadaye kupoteza maisha; mashuhuda walisema.

 

Inaelezwa kuwa, baada ya kufanyiwa ukatili huo mzito uliotokea Septemba, Mosi mwaka huu, kijana huyo alitembezwa mitaani na mjeshi akiwa kifua wazi huku akionekana mchovu na aliyehitaji msaada wa wasamaria.

 

Video na picha ya tukio iliyonaswa na gazeti hili na kutumika ukurasa wa mbele wa gazeti hili inasherehesha kile walichosema mashuhuda kuwa kijana huyo alifanyiwa ukatili tena mbele ya watu ambao walishindwa kumuokoa na kipigo kwa kile kilichodaiwa: “Kuuingilia ugomvi wa mwanajeshi ni kutokujipenda.”

 

BABA WA MAREHEMU AITWA

Wakati tukio la kijana huyo kupigwa likiendelea, baadhi ya watu waliingiwa na huruma na kulazimika kumpigia simu baba mzazi wa Elius aitwaye Mathew Shengema ambaye aliamua kumtafuta kijana mwingine ili amsindikize eneo la tukio.

 

“Niliona nisiende peke yangu, nikamtafuta afisa wa ustawi wa jamii anayehudumia mtaa wetu, anaitwa Amini Nyamrasa nikampata, ndiyo tukaongozana huko kwenye tukio,” alisema Mathew.

 

WAJARIBU KUMUOKOA…

Aidha, baba huyo alidai kuwa, baada ya kufika walimkuta mjeshi akiendelea kumsulubu mwanaye kwa kumpiga na mkanda huku akimkanyaga na viatu sehemu mbalimbali za mwili wake.

 

“Huyo mwanajeshi namfahamu (anamtaja kwa majina mawili lakini kwa leo weledi unatubana kuyaandika) tulipokuwa tunamuamua hakutaka kutusikia kabisa. “Nikamuuliza kwani mwanangu amefanya kosa gani kubwa? Akasema amemuibia kuku, nikamwambia kama kaiba asimpige ampeleke polisi,” alisema Mathew.

 

MZEE MATHEW AFADHAIKA

“Nilipomtazama mwanangu jinsi alivyokuwa akipigwa na namna alivyokuwa amechakaa na kuchoka nilifadhaika sana nikamshawishi huyo mwanajeshi tukishirikiana na Amini kuwa asijichukulie sheria mkononi anaweza kuua.

“Ndiyo akawa katulia kidogo na kukubali kumpeleka Elius polisi,” alisema mzee Mathew kwa masikitiko.

 

ELIUS AKATALIWA POLISI

Baba wa Elius aliliambia gazeti hili kuwa baada ya mwanaye kufikishwa katika Kituo Kidogo cha Polisi Buza, askari waliokuwa zamu walikataa kumpokea kwa kuwa alikuwa amejeruhiwa huku akivuja damu nyingi na kueleza apelekwe Kituo cha Polisi Chang’ombe.

 

Inaelezwa, walipofika kwenye kituo hicho; mwanajeshi huyo alimkabidhi kijana huyo kituoni hapo na kumfungulia jalada la wizi lenye kumbukumbu namba CHA/RB/8606/019 lililokuwa chini ya mpelelezi Koplo Moses.

DHAMANA YAKATALIWA

Inadaiwa kutokana na kijana huyo kuwa na hali mbaya ya kiafya, baba yake mzazi kwa kushirikiana na ndugu zake waliomba dhamana lakini polisi waliwawekea ngumu. “Kwa kuwa tuhuma yake ni kuiba kuku nikaona niombe dhamana, lengo hasa nimpeleke mwanangu hospitali kwa sababu nilimuona akiwa na hali mbaya kutokana na kipigo alichopewa, lakini polisi wakasema niondoke kituoni niwaachie wafanye kazi zao.

Septemba 2 (mwaka huu) polisi mmoja wa Chang’ombe alinipigia simu na kuniambia kuwa mwanangu amefariki.

 

“Nilishtuka na kuumia sana moyoni, nilipouliza amefia hospitali au hapo kituoni nilipomuacha akiwa na hali mbaya, polisi aliniambia kikubwa kwangu ni kupokea taarifa hiyo ya kifo cha mwanangu. “Nikauliza mwili wake wameuweka wapi? Wakaniambia kuwa upo chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.

 

NDUGU WAGOMEA MAITI

Kutokana na taarifa hiyo ya kifo chenye utata mzee Mathew, ndugu na jamaa zake wamegomea kuchukua mwili wa marehemu hadi pale upelelezi wa kifo utakapofanyika.

 

“Huyo mtuhumiwa wa mauaji ya mwanangu namuona hapa mtaani, anaendelea na maisha yake, sasa huo mwili wa mwanangu nauchukuaje?” alihoji mzee Mathew na kuviomba vyombo vya dola kuchunguza tukio ili haki itendeke.

 

AMINI NAYE ASIMULIA

Naye afisa ustawi wa jamii, Amini ambaye awali alimuokoa na kipigo Elius kabla ya baadaye kufikwa na umauti alisema: “Aliponifuata mzee Mathew na kuniomba nimsindikize mwanaye anapigwa na mwanajeshi nilikubali tukaongozana naye mpaka huko kwenye tukio.

 

“Tukakuta kamvua nguo, kammwagia maji huku akimpiga, askari mwenyewe anafahamika hapa mtaani, nilipomdhibiti asiendelee kumpiga Elius ndiyo akakubali; tukampeleka polisi huyo kijana kwa kutumia gari la mwanajeshi huyo, lakini kusema kweli tayari alikuwa amemfanyia ukatili mkubwa sana.”

 

SHEMEJI AFUNGUKA

Shemeji wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Rose Shengena alielezea jinsi marehemu alivyotoka nyumbani siku hiyo ya tukio. “Elius kabla ya kutoka hapa nyumbani aliniaga kuwa anakwenda Temeke Stereo kwenye mambo yake, nikamuandalia chai akaondoka.

 

“Baada ya muda nikasikia akiwa huko Stereo ndiyo alitekwa na mwanajeshi huyo aliyekuwa amemtuhumu kumuibia kuku wake na kumleta mpaka huku Buza. “Alipomleta huku ndiyo akaanza kumpiga mpaka kumsababishia kifo,” alisema shemeji huyo huku akiangua kilio.

 

KAMANDA ATAFUTWA

Kufuatia sakata hilo mwandishi wetu alimpigia simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Amon Kakwale ili kujua kinachoendelea kufuatia sakata hilo ambapo simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyejitambulisha kwa jina la James Masuo ambaye alisema bosi yuko na wageni kwenye kikao.

 

Alipotafutwa kwa mara nyingine majibu ya msaidizi huyo yalikuwa yaleyale na afande James kusisitiza kuwa bosi wake akimaliza kikao hicho atamwambia kuwepo kwa ujumbe wake wa kutafutwa na mwandishi.

 

Hata hivyo, baadaye alipotafutwa tena kamanda huyo simu yake ilikuwa haipatikani hadi gazeti letu linakwenda mtamboni. Mara kadhaa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekuwa akiwaomba wananchi kushirikiana na jeshi la polisi na pale wanapoona hawatendewi haki wasisite kuwasiliana naye.


Loading...

Toa comment