Madai Mazito Msanii Amuua Mwenzake Wakigombania Maiki

DAR ES SALAAM: Madai mazito; ndivyo unavyoweza kusema baada ya msanii wa Bongo Fleva aliyetajwa kwa jina moja la Daud kudaiwa kumuua mwenzake aliyejulikana kwa jina la Yusuph Kasanda (20) ambaye walikuwa wakigombea maiki maeneo ya Salasala Mwisho wa Lami jijini Dar es Salaam, walikokuwa wamekwenda kwenye sherehe.

 

Akizungumza kwa uchungu mama wa marehemu Lucy Mwanyika alisema kuwa alipokea taarifa za kifo cha mtoto wake kwa masikitiko makubwa lakini hana cha kufanya zaidi ya kumuachia Mungu.

 

“Nilipata taarifa za msiba siku ya Jumatatu saa nane usiku nikiwa Mbeya kuwa kijana wangu amefariki dunia kwa kuchomwa kisu, ikabidi nianze safari ya kuja Dar.

“Nilifika hapa Jumanne saa 11 asubuhi, niliuliza kwa nini mwanangu wamemchoma kisu nikaambiwa alikuwa na wenzake kwenye sherehe ndiyo kukataokea kutoelewana na wenzake ambao walikuwa wakibishana kutokana na tuzo alizopata baada ya kushuka jukwaani akiwa na maiki ndipo mmoja wao alitaka yeye ndiyo aimbe, vurugu ikaanzia hapo,” alisema.

 

Baada ya mama huyo kueleza anachokifahamu Risasi liliongea na mlezi wa marehemu Yusuph aliyejitambulisha kwa jina la Salma Rajabu ambaye amesikitishwa na jambo hilo kwani ni mtoto aliyemlea katika maadili mazuri.

 

“Yusuph ni mtoto niliyemlea tangu akiwa na miaka miwili, nakumbuka siku ya tukio wakati tupo mezani tunakula, ilipofika saa mbili na nusu akaniambia mama mimi naenda Mwisho wa Lami kuna sherehe, basi nikamruhusu aende ila nikamwambia awahi kurudi.

 

“Akaniambia sawa nitawahi kurudi nataka tu nikaimbe ili nipate hela kidogo za kwenda kuangalia mpira basi akaondoka, ilipofika saa nne usiku nikapigiwa simu na mama yangu kuwa mwanangu amefariki dunia kwa kuchomwa kisu.

“Nilichanganyikiwa sana, nikauliza kwa nini wamemuua, nikaambiwa kwamba wakati sherehe inaendelea walipanda vijana wadogowadogo kwanza kuimba ndiyo na yeye baadaye akapanda na alipomaliza akapewa tuzo mbili kisha akashuka jukwaani ambapo wenzie walianza kumzonga.

 

“Baada ya hapo akatoka nje na wenzie ambapo alikaa chini ya mti na kujipumzisha; muda kidogo walifika vijana wawili wakamshika mikono miwili kwa nyuma na baadaye wakamtoboa tumboni na sime, kisha wakakimbia,” alisema mama huyo.

 

Gazeti hili halikuishia hapo liliongea na bibi wa Marehemu Bi Kasanda ambaye naye alisema kuwa alipopata taarifa kesho yake alienda hospitali na kukuta mjukuu wake ameshauawa.

 

“Nilipata taarifa usiku kutoka kwa mjukuu wangu nilichanganyikiwa na kukata simu, baadaye walikuja vijana ambao ni marafiki zake wakanitajia jina la mtu aliyefanya tukio hilo la kinyama,” alisema bibi huyo.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilimahewa, Richard Njela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa, uchunguzi bado unaendelea hivyo watawabaini waliofanya tukio hilo na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria.

 

“Nilikuwa namfahamu kijana Yusuph alikuwa ni mwema sana na alikuwa ni mchapakazi tumesikitishwa kwa kweli,” alisema mwenyekiti huyo.


Loading...

Toa comment