MADAI MAZITO MUME ACHOMA NYUMBA KUPOZA HASIRA!

MWANAUME mmoja aliyefamika kwa jina la ‘Mlawa’ mkazi wa Kizani, Gezaulole jijini Dar amedaiwa kuchoma nyumba yake na kupoza hasira alizokuwa nazo.  Kwa mujibu wa mashuhuda, jamaa huyo anadaiwa kufanya tukio hilo kutokana na kuwa na ugomvi na mkewe Zubeda Maarufu aliyezaa naye watoto watatu. “Alikuwa na ugomvi na mkewe, aliondoka hapa na kwenda kuishi na mwanamke mwingine sasa ndio hivi juzi tukashangaa amekuja kuchoma nyumba,” alidai shuhuda aliyeomba hifadhi ya jina.

Akizungumza na Uwazi, mke huyo wa Mlawa, alisema kuwa siku ya tukio yeye na wanawe walikuwa wamehamia kwa jirani yao baada ya mumewe huyo kufanya jaribio la awali la kuchoma moto kisha kushindwa. “Kabla ya tukio hilo alikuja siku ya Jumatano akamwaga petroli huku akidai kuwa anawasha nyumba moto lakini bahati nzuri tuliwahi kumuona na majirani wakanisaidia akaondoka,” alisema mke huyo wa Mlawa na kuongeza:

“Siku ya Ijumaa ndipo alipokuja tena mida ya saa tatu usiku mimi nikiwa kwa jirani yangu maana kutokana na tishio alilolifanya Jumatano la kumwaga mafuta ya petroli nikawa naogopa kulala ndani, kwanza alichukua jiwe na kuanza kupasua vioo vya madirisha, nikashtuka.

“Nilipochungulia nyumbani kwangu nikamuona mume wangu akipasua vioo madirisha, nikaamsha majirani, tukampigia simu mwenyekiti wa mtaa, akaja kuzungumza naye akandoka. “Baada ya nusu saa alirudi akaingia chumbani ambako walikuwa wakilala watoto akawasha moto nyumba ikaanza kuwaka.

“Ikabidi mwenyekiti aje tena pamoja na majirani wakanisaidia kutoa vitu tulifanikiwa kutoa vya sebuleni tu lakini vya chumbani viliungua na yeye akakimbia. “Kwa kweli sijamuelewa mume wangu nini kimempata mpaka anachukua maamuzi hayo kwa kuwa tumetoka naye mbali. Tumeanza kulala chini baadaye tukafungua biashara wote tukiamka saa kumi za usiku tukitafuta hela, tukajaliwa kujenga nyumba na kununua viwanja viwili pamoja na gari sasa leo anakuja kuchoma nyumba wakati hapa mimi naishi na wanaye!” alidai Zubeda.

Akisimulia historia ya maisha yake, mke huyo alisema mumewe aliondoka nyumbani hapo miaka kadhaa iliyopita na kwenda kuishi na mwanamke mwingine ambaye alizaa naye watoto wawili na akawa analeta tu matumizi ya watoto.

“Alikuwa haishi hapa, ana mwanamke mwingine ambaye amezaa naye watoto wawili alikuwa tu ananunua chakula na matumizi na kutuletea anaendelea na maisha yake huko aliko hadi alipokuja juzi kufanya tukio hili,” alisema na kuongeza: “Kuna kipindi tuligombana nikiwa na watoto wawili akaja kuniomba msamaha akisema yaishe tulee watoto, nikamkubalia nikashika ujauzito mwingine kwa kuwa sikujua kuwa atanigeuka tena na kuendeleza ugomvi kama hivi.

“Nilipoona anaendeleza ugomvi (hakuutaja kwa undani) nikaenda Kituo cha Polisi cha Dege kupeleka malalamiko yangu niliambiwa hili suala ni la dawati kwa hivyo niende Kituo cha Polisi Kigamboni sasa kabla sijaenda ndio mume wangu akawasha nyumba moto,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Mtaa wa Kizani, alisema kuwa awali siku ya tukio alifuatwa na Zubeda ambaye ni mke wa Mlawa kulete malalamiko yake. “Nilifuatwa na Zubeda nyumbani kwangu ilikuwa mida ya saa mbili usiku kutela malalamiko yake dhidi ya mumewe kwa kuwa ilikuwa usiku nikamwambia aende mimi nitakwenda kesho.

“Lakini roho yangu ilisita ikabidi niamke niende nyumbani kwake nikamkuta John anamwaga petroli na mkewe anahangaika kutoa vitu, nikamwambia Mlawa acha kufanya unachotaka kufanya akaniambia nimuache amalize hasira zake. “Ikabidi nimpigie kamanda wa ulinzi shirikishi akaja lakini yule bwana alifanikiwa kukimbia kabla hajachoma moto. Basi baada ya muda sisi tukaondoka pale.

“Ilipita kama dakika 45 hivi yule bwana kumbe alirudi na kuwasha moto nyumba nikapigiwa simu tena, niliporudi nikamkuta nyumba inawaka ikabidi tuanze kuuzima moto na majirani nao wakatoka kutusaidia lakini yule bwana alikimbia. Kesho yake polisi walikuja kuangalia kuendelea na taratibu zao za kuhakikisha wanamtia nguvuni mtuhumiwa,” alisema mwenyekiti.


Loading...

Toa comment