The House of Favourite Newspapers

MADAI YA KUTELEKEZA WATOTO WAWILI, MUME AMGEUZIA KIBAO MKE

WAKATI kasheshe la wanaume kutelekeza wanawake na watoto waliozaa nao likiendelea kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, mwanaume mmoja mkazi wa Mtaa wa Bukondamoyo Kata ya Mhungula wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga aliyefahamika kwa jina la Hussein Rashidi (26), amemgeuzia kibao mkewe, Aisha Osika aliyezaa naye watoto wawili, Uwazi limedokezwa.

 

Madai ya awali yaliyolifikia gazeti hili yalieleza kwamba, Rashidi alitelekeza familia yake ya watoto wawili hivyo mkewe kuchukua hatua ya kufikisha malalamiko yake katika Shirika la Kutetea Haki za Binadamu mkoani Shinyanga (Shihabi).

Habari hizo zilieleza kuwa, Osika alikuwa akimlalamikia mumewe huyo wa ndoa kwamba, tangu apate mwanamke mwingine, amekuwa hatunzi familia yake kwa kutoa matumizi kwa ajili ya watoto wake na kila akiulizwa matumizi ya watoto hujibu kwa kifupi; ‘vyuma vimekaza’.

 

Osita alilieleza shirika hilo kuwa, hali hiyo ilianza tangu wakiwa mkoani Tabora walipoanzia maisha kabla ya kufika Kahama na kuanza maisha upya.

Alisema kuwa, Rashidi alimtelekeza mara tu baada ya kufika Kahama ambapo alimpangishia chumba kimoja anachoishi na wanaye hao wawili hadi sasa.

Alisimulia: “Tangu mume wangu anitelekeze, ninaishi na watoto wawili, mmoja ana umri wa miaka mitatu na mwingine ana miezi miwili.

 

“Matumizi anayotoa kwa siku ni shilingi 2,000 na wakati huo ndani hakuna mchele, mkaa, mafuta, maharage, unga, sukari ya uji kwa watoto pamoja na sabuni.”

Hata hivyo, Osita alisema kuwa, alichukua uamuzi wa kumshtaki mumewe huyo kwa kuwa kila anachomueleza hasikilizwi.

Baada ya kusikiliza maelezo ya Osita ndipo Rashidi akatoa utetezi wake uliowachekesha sana wasikilizaji wa sakata hilo huku akimgeuzia kibao mkewe huyo.

 

Kwanza, Rashidi alikiri kumtelekeza Osita, lakini alidai kuwa, hakumtelekeza na watoto wawili bali ni mmoja tu hivyo kuibua sintofahamu kwa wasikilizaji waliotaka kujua kivipi?

Rashidi alidai kwamba, hakutarajia kumpata mtoto huyo mdogo kwa sababu alipatikana wakati wakiwa safarini mkoani Tabora walipokwenda kumuangalia mtoto wao mkubwa.

 

Alijitetea na kuibua vicheko: “Mara baada ya kufika Tabora, mamamkwe wangu alitupisha kwenye kitanda chake tulale kwa kuwa muda ulikuwa umeenda. Hapo ndipo mimba ilipopatikana bila mimi kukusudia kwani nilishamuacha na kuoa mke mwingine.”

Rashidi aliongeza kuwa, amekuwa akimhudumia Osita kila siku na amekuwa akimpatia shilingi 2,000 hadi 2,500 kutokana na hali ngumu ya maisha na akaahidi kuongeza matumizi kutoka shilingi 2,000 hadi shilingi 4,000 ifikapo mwezi wa tano kutokana na mwezi huu wa nne kwake kuwa mgumu.

 

Kwa upande wake, mwanasheria wa shirika hilo, Hawa Saidi alisema kuwa, wanandoa hao walishafika ofisini kwao kulalamika na kutaka wao kuachana na kugawana mali.

Alisema wawili hao walikubaliana mwanamke achukue godoro, vyombo vya ndani, redio, meza na kuondoka zake.

 

Mwanasheria huyo alisema kuwa, kama walifikia hatua ya kushitakiana kwa mara nyingine, kisa mwanaume kutotoa matumizi ya watoto, mwanaume alitakiwa kutoa mahitaji yale ya muhimu kama vile unga, mchele, sabuni, maharage, mafuta ya kupaka ya watoto hali ambayo itasaidia kupunguza malalamiko.

 

Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mengi kwenye jamii juu ya watoto kutelekezwa hivyo ni wakati wa watu kubadilika ili kumaliza tatizo hilo linalokua kwa kasi kila kukicha.

STORI: SHABAN NJIA, SHINYANGA

Comments are closed.