The House of Favourite Newspapers

Madai ya Uchawi: Esma Aanika Siri Nzito ya Mobeto

DADA wa staa wa Afro Pop ndani na nje ya Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Esma Khan amerusha bomu lingine kwa mwanamitindo Hamisa Mobeto kwamba ndiye chanzo cha sakata lao la mambo ya kurogana kufika yalipofikia.

 

Akizungumza na Ijumaa Wikienda kwenye mahojiano maalum kuhusiana na sakata hilo, Esma alisema amekuwa akizushiwa lawama na matusi kwamba ndiye aliyevujisha ishu hiyo jambo ambalo si kweli.

 

Alisema anayestahili lawama ni Mobeto kwani angekubaliana na alichokifanya tangu mwanzo wala sakata hilo lisingefika mbali kama ilivyotokea kwani hata wao kama familia hawakutaka yafike yalipofikia mpaka hivi sasa.

 

“Unajua kama sisi tungekuwa wabaya, basi tungeweka kila kitu kwenye mitandao, lakini kutokana na watu hawaelewi, wanatutukana na kutusema vibaya kwa sababu tu hawajui ukweli wa hili jambo,” alisema Esma.

 

Mwanamama huyo alizidi kuweka wazi kuwa anawashangaa watu kuwaona wao kama wakosefu na labda hawampendi Hamisa, lakini siyo kweli ni kwa sababu tu mwanamitindo huyo anatengeneza sura ya huruma kwa watu.

 

“Watu wanaweza kusema mama yangu ana matatizo, lakini siyo, kwa sababu hata huyo mganga hakuwa anamjua, bali ni ndugu wa huyo mganga ndiye anafahamiana na mama na kwa vile aliona ni watu ambao wanakuwa pamoja kwenye vitu mbalimbali ndiyo akamwambia huyo ndugu yake na mama akayapata,” alisema Esma.

 

Esma alisisitiza kuwa sauti zilizosikika ni za wahusika wenyewe wala hakuna cha kutengeneza na ni bora wangenyamaza kwa sababu baada ya kusikika ile sauti, upande wa pili wa Mobeto walituma watu wakaanza kumtukana yule mganga.

 

“Najua kabisa ukweli wao wanafahamu, lakini wanapenda kupindisha mambo na hayo yaliyosikika ni madogo mno, yapo mengine na tuna ushahidi wa kutosha hivyo na sisi tukiamua tutalipua bomu muda wowote,” alisema Esma.

Esma na mama yake ndiyo wanaotuhumiwa kuvujisha sauti ya Mobeto akimuomba mganga wa jadi amsaidie ili aolewe na Diamond na kupendwa na mama yake.

STORI: Imelda Mtema, DAR

Huyu Ndiye Mshindi wa Miss Tanzania 2018

Comments are closed.