MADAKTARI WAKWAA SKENDO

HUJAFA hujaumbika ni msemo wa Kiswahili wenye tafsiri ya maisha ya kiumbe na maumbile yake halisi aliyoumbwa na Mwenyezi Mungu na baadaye kuishi duniani kwa kadiri Mungu alivyomkadiria maisha yake. Unaweza kuzaliwa ukiwa na viungo kamili vya mwili wako, lakini kutokana na mazingira ya maisha yanayotokana na tabia za kimaumbile, viungo vya mwili wa binadamu vinaweza kubadilika na kuwa katika taswira nyingine tofauti na awali ambayo umezaliwa nayo.

MADAKTARI WAKWAA SKENDO

Hicho ndicho anachokutana nacho mwanamama Valentine Winjislaus (pichani), mkazi wa Tabata-Kinyerezi jijini Dar, baada ya madaktari kukwaa skendo nzito ya kudaiwa kumfanyia kitu mbaya wakati akijifungua. Mama huyo yupo kwenye mateso na maumivu makali mno baada ya kidonda chake cha upasuaji kutofunga kwa madai ya kukosewa zaidi ya mara mbili. Madaktari hao wa hospitali maarufu ya Serikali jijini Dar (jina la hospitali linahifadhiwa kwa sasa hadi baadaye kwa sababu za kisheria) walidaiwa kutenda kosa hilo kutokana na uzembe.

MUME ACHACHAMAA

Akizungumza na Gazeti la Risasi Jumamosi kwa masikitiko makubwa, mume wa Valentine, Samson Kuyava alichachamaa vikali mno na kusema kuwa mkewe huyo yuko kwenye mateso kiasi ambacho anashindwa afanye nini kwa sasa baada ya kuhangaika bila mafanikio.

AJIFUNGUA KWA UPASUAJI

Akisimulia kisa na mkasa huo, mwanaume huyo alisema kuwa, ilikuwa mwezi Februari, mwaka huu ambapo alimpeleka Valentine kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kujifungua. Kuyava alisema mkewe huyo alikuwa akijifungua mtoto wao wa tatu kwa njia ya upasuaji ndipo alipopatwa na majanga mazito yaliyomfanya kupita kwenye bonde la mauti.
MSIKIE MUMEWE “Baada ya upasuaji huo ambao ulikuwa ni mara ya kwanza kwa mke wangu kujifungua kwa njia hiyo (operesheni), tulimshukuru Mungu kwani mtoto wetu alitoka salama salimini na baada ya pale tukarejea nyumbani,” alisema Kuyava.

VITU VYASAHAULIKA TUMBONI

Kuyava alizidi kusimulia kuwa, baada ya kuruhusiwa kisha wakarejea nyumbani, muda mfupi baadaye mkewe alianza kulalamika tumbo linamuuma na kwamba anakata roho huku akitapika kila anachokula, jambo
lililowaogopesha. Alisema ilibidi warudi kwenye hospitali hiyo ambapo waliambiwa kuwa kuna vitu vilisahaulika tumboni hivyo wakamfanyia upasuaji mwingine wa pili, kidonda kikiwa bado kibichi na kutoa vitu hivyo vilivyosahaulika kitaalam. “Kwa kweli nilisikia huruma sana kutokana na maumivu ya mke wangu huku akiwa na mtoto mdogo,” alisema Kuyava.

UPASUAJI WA TATU

Kuyava alieleza kuwa, baada ya upasuaji huo, Valentine alirudi tena nyumbani wakiamini mambo yataenda sawa, lakini baada ya muda, tumbo la mkewe lilivimba mno na kuwa kubwa kiasi cha kutaka kupasuka huku akihisi maumivu makali kiasi cha kushindwa kunyonyesha mtoto wao mchanga na hofu kutanda kuwa huenda anakata roho.

“Tuliporudi tena kwenye hospitali ileile walitupa rufaa, tukaenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Kuyava. Alisema kuwa, baada ya kufika Muhimbili, mkewe huyo alifanyiwa vipimo ambapo ilibainika kuwa alipofanyiwa upasuaji wa pili, wakati wa  ushonaji, madaktari walishonea na utumbo.

Alisema baada ya hapo mkewe alifanyiwa upasuaji mwingine na kukata sehemu ya utumbo iliyoshonewa na kumtoboa pembeni mwa ubavu kwa sababu njia ya mkojo iliziba wakati wakiushonea utumbo huo. “Ukisikia mateso aliyopata mke wangu ni mazito maana hata mtoto hakuweza kunyonyesha tena, ilibidi kumtafutia maziwa ya kopo ambayo ni gharama kubwa.

“Mke wangu ilibidi awekewe mipira kwa ajili ya kupitisha haja ndogo na kila mpira mmoja ni shilingi elfu 25. “Kwa wiki moja inatakiwa mipira zaidi ya mitatu, kwa kweli nimechanganyikiwa kabisa
ukizingatia kipato changu nacho ni changamoto kubwa,” alisema Kuyava akilengwalengwa na machozi.

BADO MSHONO HAUJAPONA Baba huyo aliweka wazi kuwa, hata baada ya kufanyiwa upasuaji, bado kidonda hicho hakikukauka, badala yake kinazidi kumuuma mkewe na ameteseka kwa kipindi chote cha miezi mitano.
MALALAMIKO YAKE Baba huyo anakwenda mbele zaidi na kusema kuwa, kila alipokuwa akijaribu kwenda kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo amekuwa akiambiwa aandike barua ya malalamiko au aende makahamani huko ndiko atakapopata haki yake. “Kinachoniuma ni namna ninavyojibiwa wakati jambo lipo wazi kabisa kwamba madaktari walifanya uzembe kwa mke wangu.

KUMBE HANA KIZAZI “Nasema ni uzembe kwa sababu hata madaktari wa Muhimbili walisema kulikuwa na uzembe. “Isitoshe madaktari wa Muhimbili walithibitisha kuwa madaktari hao wakati wanamfanyia operesheni ya pili walimtoa kizazi hivyo mke wangu kwa sasa hana kizazi,” aliendelea kusema Kuyava na kuongeza; “Hadi sasa mke wangu amefanyiwa operesheni nne na bado hajapona.
SAKATA LATINGA KWA WAZIRI UMMY

“Nilipewa namba ya Waziri Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto), niliwasiliana naye, akanipa pole na kuahidi kulifuatilia suala la mke wangu, lakini mpaka sasa naona kimya tu,” alisema Kuyava akionesha SMS ya Waziri Ummy.

OMBI KWA WATANZANIA Kuyava aliwaomba Watanzania wanaoguswa na tatizo la mkewe wanaweza kuwasiliana naye kwa namba 0716 789 830 kwa ajili ya msaada wa kisheria, hali na mali.RISASI JUMAMOSI MZIGONI Gazeti la Risasi Jumamosi liliingia mzigoni kusikia upande wa pili wa hospitali hiyo ambapo jitihada ziligonga mwamba.
MGANGA MKUU WA MKOA Hata hivyo, jitihada hizo hazikuishia hapo kwani gazeti hili lilimtafuta Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar, Dk Yudas Ndungile ambaye alisema suala hilo halikuwa limemfikia mikononi mwake. “Hilo halijanifikia, lakini pia sijapata takwimu za matukio ya aina hiyo. Naomba nilifuatilie ili niwe na majibu kamili,” alisema Dk Ndungile.
KUTOKA KWA MHARIRI Gazeti hili linaahidi kulifuatilia sakata hili hadi kujua hatma yake itakuwaje hivyo endelea kufuatilia.
MADAKTARI


Loading...

Toa comment