The House of Favourite Newspapers

MADENTI WAINGIZWA GESTI MCHANA

HIVI wazazi wawafiche wapi watoto wao wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao kimasomo? Jibu la swali hili ni gumu kutokana na ripoti kamili ya hivi karibuni ya Ijumaa kuonesha jinsi madenti wa kike wanavyoingizwa gesti jijini Dar kufanyiwa ufuska na wanaume wakware hata nyakati za masomo.  

 

Takwimu za Idara ya Watoto katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka huu inaonesha kuwa watoto 27 kati ya 100 hupata ujauzito katika umri mdogo. Wazazi au walezi wengi wamekuwa wakijiuliza ni wakati gani watoto wao wa kike wa shule za msingi na sekondari hushiriki ngono hatarishi? Ijumaa limechunguza na kubaini yafuatayo;

 

Shule kukosa mabweni, ukosefu wa maadili, vishawishi vya mafataki, wanafunzi kuishi mbali na shule na uwepo wa mila potofu ni miongoni mwa mambo yanayochochea wanafunzi wengi wa kike kujihusisha na ngono za utotoni. Aidha, kuhusu muda gani wanaotumia wanafunzi wa kike kufanya ngono, hasa jijini Dar, kwa mujibu wa uchunguzi wetu, ni nyakati za mchana ambapo wasichana hao hupata ruhusu kutoka kwa wazazi wao kwenda shule au kwenye masomo ya ziada maarufu kama tuition.

SINTOFAHAMU YA WAZAZI WENGI

Kwa muda mrefu kumekuwepo na masikitiko haya miongoni mwa wazazi: “Mwanangu nimemlea vyema, hapa nyumbani haruhusiwi kutoka ovyo kwenda kuzurura.

“Akitoka hapa anapanda gari, anakwenda shule, anarudi jioni; akifika ni kupumzika na baadaye kusaidia kazi za nyumbani usiku unaingia tunalala. “Leo ninapoambiwa mwanangu ni mjamzito ninachanganyikiwa, najiuliza amejifunzia wapi haya mambo na muda gani anautumia kuyafanya,” Mwanahamisi Hussein, mkazi wa Mikocheni jijini Dar aliliambia Ijumaa siku chache zilizopita baada ya kubaini kuwa mwanaye anayesoma kidato cha tatu (shule kapuni) amepata ujauzito.

 

MHARIRI MKUU  IJUMAA AITISHA MJADALA

Mara kadhaa, kwa lengo la kutafuta majibu yanayosaidia jamii kuondoa changamoto zilizopo, Timu ya Ijumaa imekuwa ikifanyia uchunguzi sintofahamu nyingi ambapo zamu hii ilikuwa ni kuangalia ni nyakati gani wanafunzi hujihusisha na vitendo vya ngono.

MHARIRI MKUU: Ndugu zangu nimewaita, nataka tubadilishane mawazo, nadhani mtakuwa mnafahamu kuhusu baadhi ya wanafunzi wa kike kukatiza masomo kutokana na ujauzito.

WAANDISHI: Tunafahamu kiongozi.

 

MHARIRI MKUU: Kwa fikra za kawaida mnadhani ni wakati gani hasa hapa Dar wanafunzi hawa wanafanya vitendo vya ngono maana ukiangalia muda mwingi wasichana hawa wanautumia kwenye masuala ya masomo; halafu mara nyingi mchana wanakuwa na sare za shule, mnadhani kuna mwanaume anaweza kumchukua mwanafunzi wa kike akiwa na sare, tena mchana na kumwingiza gesti au nyumbani kwake?

WAANDISHI: Inawezekana kabisaaa.

MHARIRI MKUU: Jambo hili ni gumu kwa mazingira yetu maana gesti haziruhusiwi kuingiza wanafunzi…

MWANDISHI: Zipo nyingi tu zinaruhusu mkuu, wala si za kutafuta.

MHARIRI MKUU: Kama gesti hizi zipo nadhani iwe ndiyo assignment ya leo, tuchunguze. Maana wazazi wengi hasa hawa wa geti kali hawafahamu watoto wao wanafanya hayo mambo saa ngapi?

 

UCHUNGUZI KAMILI WAANZA

Mara baada ya kumalizika kwa majadiliano hayo ya kazi ambayo ndiyo msingi mkubwa wa mafanikio ya vyombo vyetu vya habari, waandishi kadhaa waliingia kazini kupeleleza uwepo wa gesti na hoteli ambazo zinaruhusu mtu kungia na mwanafunzi, tena akiwa kwenye mavazi ya shule.

 

Siku ya kwanza ambayo ilikuwa ni Oktoba 19, mwaka huu, timu ya wachunguzi wawili wa kike aliyekuwa amevalia sare za shule ya sekondari na begi la kuwekea madaftari iliingia kazini kwa kuzipitia hoteli kubwa mbili zilizopo Kariakoo (majina yanafichwa) ambazo gharama za kukodi chumba ni kubwa na matokeo yalikuwa hivi; “Vipi nafasi zipo?”

Shushushu wetu wa kiume alimuuliza mhudumu wa mapokezi katika hoteli ya kwanza huku akiwa ameambatana na shushushu wetu wa kike aliyekuwa amevaa sare za shule.

MHUDUMU: Nafasi zipo.

SHUSHUSHU: Okey…shilingi ngapi?

MHUDUMU: Vipo vya laki moja na ishirini na vya shilingi elfu sabini.

SHUSHUSHU: Nipatie cha elfu sabini. Alisema shushushu wetu huku akitoa fedha za kulipia chumba hicho, tukio ambalo lilikuwa likirekodiwa na vifaa kazi.

 

MHUDUMU: Nani anataka chumba hicho?

SHUSHUSHU: Mimi, kwani vipi?

MHUDUMU: Na huyu mwanafunzi ni nani wako?

SHUSHUSHU: Ni mdogo wangu.

MHUDUMU: Chumba utapata, lakini huyu hutaruhusiwa kuingia naye chumbani, kama ni mazungumzo tuna maeneo yetu ya kuzungumzia.

 

Mara baada ya majibu hayo ya mhudumu yaliyoonesha umakini katika kazi, mashushushu wetu walijaribu kumuonesha mfanyakazi huyo wa hoteli kuwa hakuna tatizo baina yao, lakini waligomewa na kuwafanya waondoke huku mpango wao ukiwa umefeli. Hata hivyo, walipokwenda hoteli nyingine ambayo iko eneo la Kariakoo, Mnazi-Mmoja, nako uchunguzi wao uligonga mwamba na hivyo kulazimika kurejea ofisini wakiwa wamefanya kazi nzuri, lakini isiyokuwa na matokeo yaliyotakiwa.

 

UCHUNGUZI WAHAMIA GESTI

Oktoba 21, mwaka huu, uchunguzi uliendelea kwenye nyumba za kulala wageni zilizopo maeneo ya Buguruni- Sokoni, Manzese, Mabibo, Magomeni, Ubungo na Temeke eneo la Sokota ambapo zoezi lilikwenda vizuri kwani miongoni mwa gesti sita zilizofanyiwa uchunguzi katika maeneo hayo, tatu zilikubali shushushu wetu wa kiume kuingia gesti na shushushu wa kike, mbili zilitaka dau la kukodi chumba liongezeke na kwamba wateja walitakiwa kupewe chumba maalum huku gesti moja mhudumu wake akigeuka mbogo kwa kupelekewa mwanafunzi katika biashara yake.

 

“Kaka hii ni biashara, naomba uiheshimu, ulipokuja kulipa chumba mimi sikujua kama unaleta mwanafunzi, tangu lini mwanafunzi anaingizwa gesti? “Nakuomba… nakuomba ujiheshimu, ukiona hivi usidhani nashindwa kukuitia Polisi, naweza; lakini sipendi kukuharibia siku yako, kwa heshima yako ondoka,” alifoka mhudumu wa gesti moja iliyopo Ubungo eneo la Shekilango na kuwafanya mashushushu wetu waondoke eneo hilo wakiwa wameshalipia shilingi elfu 20.

GESTI NYINGINE MBILI ZANASWA

Oktoba 24, mwaka huu, majira ya saa 5:00 asubuhi, zoezi la uchunguzi liliendelea ambapo timu ya mashushushu wetu, wakiwa na gari dogo walikwenda eneo la Sinza karibu na baa maarufu ya Hongera ambapo walifanikiwa kuingia kwa kupokewa kwa bashasha na mlinzi.

 

“Vyumba vipo karibuni sana,” mhudumu wa gesti hiyo ambayo jina lake linaanza na herufi M na kushia na T alionesha furaha kupata wateja huku akipuuzia kuwa mteja mmoja alikuwa na sare za shule na kwamba Serikali hairuhusu msichana wa aina hiyo kuingia gesti.

 

Aidha, baada ya mapokezi hayo mema, shushushu wetu wa kiume alilipia chumba cha shilingi elfu 20 na kwenda kuoneshwa huku akiambatana na mwanafunzi huyo feki. “Hodi,” mhudumu aligonga tena mlango wa chumba alichowapa mashushushu wetu, alipofunguliwa alikabidhi taulo, sabuni ya kuongea kisha kuondoka. Ikumbukwe kuwa tukio hilo lilichukuliwa picha laivu ambazo baadhi zimetumika kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti hili.

 

Baada ya dakika zisizozidi kumi, mashushushu wetu waliwasiliana na wenzao waliokuwa nje kuwa wanatoka na kwamba walitakiwa kupigwa picha wakati wakitoka kwenye gesti hiyo. Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, mashushushu wetu walikwenda kwenye gesti nyingine iliyopo eneo hilo ng’ambo ya Barabara ya Shekilango kwa upande wa Mwenge ambapo nako walikubaliwa, lakini waliishia kuingia ndani kisha kutoka kwa kisingizio cha bei kuwashinda.

 

MUDA WA HATARI KWA WANAFUNZI

Mbali na uchunguzi wa kuzibaini gesti zinazoruhusu wanafunzi wa kike kuingia kufanya uchafu, kilichoangaliwa ilikuwa ni suala la muda gani wasichana huutumia kujihusisha na ngono.

 

Ilibainika kwamba, baadhi wa wanafunzi wa kike hutoroka shule nyakati za masomo na kwenda kwa wanaume ambako huenda kwenye gesti zisizotii masharti ya biashara ambako huruhusiwa kuingia ndani huku wakiwa wamevaa sare. Wapo baadhi ya wasichana ambao hutumia fursa ya ruhusa kutoka kwa wazazi wao kwenda kujisomea kwa wenzao au kwenda kwenye masomo ya ziada ambako huko hubadili nia na kwenda kufanya maasi yanayowaletea mimba na kukatizwa kwa ndoto za masomo.

 

WAZAZI KAENI CHONJO

Kufuatia uchunguzi huu, Dawati la Ijumaa linawaomba wazazi kupitia kwa makini habari hii na kuwa chonjo na watoto wao wa kike, vinginevyo watajikuta wanawalelea watoto mafataki ambao watawatumia na kuwaharibia masomo kama si kuwaambukiza magonjwa

Stori: Waandishi Wetu, Ijumaa

Comments are closed.