MADEREVA wa kampuni ya Dangote Cement inayomilikiwa na mfanyabiashara tajiri Afrika, Aliko Dangote, ambao ni Hussein Hassan na Juma Mtambo na Sadick, ambao wote ni raia wa Tanzania, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Kisutu leo wakikabiliwa na kosa la kusafirisha isipo halali raia 40 wa Ethiopia waliokuwa wanakwenda Afrika Kusini wakipitia Tanzania.
Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay, alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano ambayo ni kuingia nchini kinyume na sheria ikidaiwa Septemba 25 mwaka huu walikutwa maeneo ya Mbagala-Kongowe, wakiishi bila kuwa na kibali.
Kosa jingine ni usafirishaji usio halali linalowakabili madereva Watanzania waliowasafirisha ambapo inadaiwa Septemba 20 mwaka huu, maeneo ya Mbagala, Kongowe, na Mtoni Mtongani walikutwa wakisafirisha Waethiopiahao kwa kutumia gari ambalo ni mali ya Dangote Cement kuelekea Afrika Kusini.
Baada ya kusomewa makosa hayo, raia wa Ethiopia walikiri kosa ambapo Watanzania walikana na Wakili Mlay alisema upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.
Hakimu Nongwa alisema washtakiwa waliokana makosa wanaweza kupata dhamana kwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waaminifu ambapo washtakiwa waliokiri kosa walitakiwa kusomewa maelezo ya awali. Kesi iliahirishwa hadi Oktoba10 na 11 mwaka huu.
NA DENIS MTIMA/GPL