The House of Favourite Newspapers

MADHARA YA PENZI LENYE SABABU MBOVU

KARIBUNI jamvini, mahali ambapo tunajadili changamoto na mafanikio ya uhusiano wa kimapenzi na maisha kwa jumla. Tukubaliane wadau kuwa, lengo la kuingia kwenye uhusiano liwe zuri au baya ndilo litakalokupa matokeo, yawe mazuri au mabaya!

Lengo hilo ndilo litakalokupeleka kwenye maisha unayoyataka, yawe ya furaha au machozi kila kukicha. Baada tu ya kukubaliana kuwa na huyo mwenza wako, iwe kwenye ndoa au uhusiano wa kimapenzi kwa sababu zisizo za msingi, siku, miezi au miaka michache, utaanza kuona matokeo.

Kama nilivyoeleza, kama sababu za kuingia kwenu kwenye penzi zilikuwa mbovu, basi tegemea matokeo mabovu. Hakuna tunda bovu ambalo mkulima hutegemea kupata matunda mazuri. Kibovu huzaa kibovu na kizuri huzaa kizuri.

Hapa ndipo ambapo wengi hujikuta kwenye maumivu na machozi ambayo hutokana na msongo, mfadhaiko na muda mwingi kukosa furaha. Matokeo ya hali hii humfanya mmoja wenu au wote kuanza kutafuta kutoshelezwa au kuliwazwa ndipo vinazaliwa vitu kama uzinzi, usaliti na mwisho ni kutengana.

KWA NINI MAPENZI HUFA?

Uhusiano mwingi umekuwa dhaifu kwa sababu ya wahusika kukosa maarifa. Wapenzi wengi hawajui nini cha kufanya ili kuwa na uhusiano imara. Thamani ya penzi inavyochukuliwa siku hizi ni tofauti sana na nyakati za wazazi wetu.

Hii imewafanya wapenzi wengi kujikuta wakiwa kwenye uhusiano au ndoa kwa sababu mbovu hivyo mapenzi kufa baada ya muda mfupi tu. Vitu kama kudhamiria, heshima na uaminifu siyo msingi tena siku hizi. Baadhi ya vijana wa kisasa wanaogopa kuonekana wa kizamani. Mtazamo wao juu ya mapenzi unashikiliwa na ‘social media’ hasa mitandao ya kijamii na teknolojia yake ya simu za mkononi.

Siku hizi kuchukuana na kuanza kuishi pamoja ni jambo la kawaida bila kujua kuwa wanaondoa thamani ya ndoa na kuifanya ya kawaida. Watu kusalitiana siyo jambo la kutisha, mapenzi nje ya uhusiano haishangazi. Katika hali kama hii mtadumu wapi?

Mambo yamebadilika siku hizi. Zamani binti akikutwa bikra wakati anaolewa ilikuwa ni sifa kubwa kwake na familia nzima. Siku hizi binti akikutwa bikra anachekwa na watu kumshangaa wakihisi ana matatizo fulani. Hali kadhalika kwa kijana wa kiume aliyejitunza. Kwa bahati mbaya tunaishi katika jamii ya ajabu isiyoamini katika kujitoa kwa dhati na kudhamiria. Jamii haiamini katika uaminifu na ndiyo maana magomvi yamekuwa mengi pale simu ya mmoja inapoguswa.

Ni mwendo wa kuwindana na kuchunguzana, maadili siyo jambo la kuzingatiwa tena. Wanandoa wengi ni wale wenye majeraha ya mioyoni na walioumizwa. Kwa hiyo hutoka nje ya ndoa zao kutafuta mwingine aliyeumizwa kama wao ili waliwazane ni kawaida sana.

Kwa mujibu wa Mtaalam wa Saikolojia, Dk Chris Mauki, yote kwa yote, ukitazama kwa kina utagundua kuna sababu za msingi zinazoweza kukufanya uingie kwenye uhusiano na usijute;

KWANZA

Kwanza ujue kwamba, penzi au ndoa ni mpango wa Mungu kwa mwanamke na mwanaume kuwa pamoja. Ni nafasi yao wawili kuoneshana mapenzi.

PILI

Lazima ujue kwamba, kuwa kwenu wawili ni nafasi ya kutimiziana mahitaji ya kimwili kupitia tendo la ndoa kwa muda sahihi na mtu sahihi kwa kufuata maadili yote.

TATU

Lazima ujue kwamba, kuwa wawili ni ili kutimiza hamu yenu ya kutengeneza familia yenu.

NNE

Ni lazima ujue kwamba, ni nafasi ya kutumia kwa manufaa kila uwezo na vipawa mlivyo navyo.

Comments are closed.