The House of Favourite Newspapers

Madhara ya Uvutaji wa Sigara Mwilini

UVUTAJI wa sigara ni tabia hatarishi inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa mvutaji na watu wa karibu yake wanaovuta moshi anaoutoa. Licha ya elimu kubwa inayotolewa, bado idadi ya wanaovuta sigara inazidi kuongezeka.

Utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba moshi wa sigara, una kemikali nyingi zenye sumu ambazo ni hatari kwa mwili wa binadamu na kwa taarifa yako, uvutaji wa sigara huathiri karibu kila kiungo katika mwili wako, kuanzia mapafu, macho, koo, ini, figo, ubongo na vingine vingi.

Sumu za hatari zaidi zilizopo katika sigara ni pamoja na carbon monoxide, hydrogen cyanide, nitrogen oxide, formaldehyde, benzene na mbaya zaidi, sigara zina kiasi kikubwa cha kemikali za nicotine na phenol zinazotajwa kuwa kichocheo cha mtu kupata aina mbalimbali za saratani.

Uvutaji wa sigara husababisha kuharibika kwa mishipa ya damu ambayo husinyaa na kusababisha damu ipite kwa shida, hivyo kumuweka mvutaji katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo yakiwemo shambulio la moyo, stroke, shinikizo la juu la damu na kadhalika.

Madhara ya uvutaji sigara yanatajwa kuwa makubwa zaidi kwa wenye tabia ya kuvuta sigara muda mfupi baada ya kula. Pia utafiti wa kitaalamu unaonesha kwamba mara tu baada ya kumaliza kula, kiu ya kuvuta sigara huongezeka zaidi, lakini unayajua madhara yake?

Sigara zina nicotine, ambayo ikiingia ndani ya mwili, huzuia mzunguko wa hewa ya oksijen amnayo kwa kawaida baada ya kula, huwa inahitajika sana kwa ajili ya mmeng’enyo wa chakula tumboni. Pia Nicotine hii, ikichanganyikana na tumbaku kwenye damu, huwa chanzo kikubwa cha saratani.

Utafiti unaonesha kwamba kuvuta sigara moja baada ya kula, ni sawa na kuvuta sigara kumi kwa mpigo muda ambao hujatoka kula. Wavutaji sigara wanashauriwa kukaa saa kadhaa baada ya kula ndiyo wavute sigara.

Uvutaji wa sigara husababisha magonjwa ya mapafu, kwani kemikali zilizopo kwenye sigara huharibu vifuko vya hewa (alveoli) vilivyopo kwenye mapafu na kusababisha mapafu yashindwe kuchuja hewa vizuri na hivyo kuufanya mwili ukakosa hewa safi ya Oxygen.

Pia kama mvutaji ana ugonjwa wa pumu, sumu zilizopo kwenye moshi wa sigara husababisha ugonjwa huo uzidi kuchachamaa mwilini na pengine kusababisha kifo cha ghafla

Hatari kubwa zaidi ni kwenye ugonjwa wa saratani, ambapo uvutaji wa sigara unatajwa kusababisha saratani za aina mbalimbali, ikiwemo saratani ya kibofu, saratani ya damu, saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake, saratani ya utumbo, saratani ya koo na nyingine nyingi.

Kwa wanawake, uvutaji wa sigara husababisha matatizo ya kushindwa kupata ujauzito, mimba kutunga nje ya kizazi, mimba kuharibika mara kwa mara, kujifungua watoto njiti na madhara mengine mengi yanayohusu uzazi.

Kwa kutazama athari hizo, ni dhahiri kwamba sasa umegundua madhara ya uvutaji wa sigara. Kuacha kuvuta sigara huwa ni kazi ngumu hasa kwa wale wavutaji waliozoea lakini ukiweka nia, inawezekana. Anza kwa kupunguza idadi ya sigara unazovuta na weka nia ndani ya moyo wako kwamba unataka kuacha, baada ya muda utaweza.

Comments are closed.