The House of Favourite Newspapers

MADRID WABEBA UEFA KWA MARA YA TATU MFULULIZO

MABAO mawili aliyofunga Gareth Bale yaliibeba Real Madrid na kuandika historia ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ‘Uefa’ kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuilaza Liverpool mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa usiku wa kuamkia leo Jumapili kwenye Uwanja wa Olimpiyskiy mjini Kiev, Ukraine.

Pia Real Madrid imeongeza rekodi yake ya kutwaa taji hilo mara nyingi, ambapo sasa imefikisha mara ya 13. Kufuatia mafanikio hayo ya kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo ina maana italihifadhi kombe hilo moja kwa moja na Shirikisho la Soka Bara la Ulaya (UEFA) itabidi iandae kombe jipya.

Bale alianzia kwenye bench lakini kuingia kwake kuliongezea nguvu Real Madrid kwani alipachika mabao mawili yaliyozima ndoto za Liverpool kutwaa taji hilo kwa mara ya sita.

 

Kati ya mabao hayo, moja lilikuwa maridadi na litabakia katika historia ya mashindano hayo wakati jingine lilitokana na makosa ya kipa wa Liverpool, Loris Karius, ambaye alifungisha mabao mawili.

Karius aliizawadia Real Madrid bao la kuongoza mnamo dakika ya 51 baada ya kudaka pasi ya kupenyeza ya kiungo wa Real, Toni Kroos lakini aliamua kuurusha mpira uliomgonga straika wa Real Madrid, Karim Benzema na mpira kujaa wavuni. Benzema alitumia uzoefu kumkabili Karius, ambaye alifanya haraka ya kurusha mpira wakati straika huyo akiwa karibu.

 

Liverpool, ambayo ilipata pigo mapema kwenye mchezo huo baada ya straika
wao, Mohamed Salah kuumia, ilipigana kufa na kupona na kusawazisha dakika nne baadaye kwa bao lililopachikwa na Sadio Mane baada ya kuunganisha mpira wa kichwa wa Dejan Lovren uliotokana na mpira wa kona.

Baada ya hapo ndio yakaja mambo ya Bale, ambaye alifunga bao la pili kwa staili maridadi ya`tik tak’ katika dakika ya 64 na bila shaka ataingia katika orodha ya mastaa waliowahi kufunga mabao makali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Karius aliboronga tena katika dakika ya 83 baada ya kupangulia wavuni shuti la Bale ambalo alipiga umbali wa mita 20 hivi. Liverpool ilipata pigo la mapema kufuatia kuumia na kutoka kwa mfungaji wake tegemeo Salah kwenye mechi ya jana.

 

Hata hivyo, upepo wa mchezo ulibadilika ghafla baada ya Salah kutoka katika dakika ya 29 kufuatia kuumia bega. Salah aliumia mapema katika dakika ya 25 baada ya kuanguka vibaya wakati akigombea mpira na beki wa Real Madrid, Sergio Ramos.

Comments are closed.