Maelfu ya watu waandamana kabla ya kuapishwa kwa Trump
Maelfu ya watu wengi wao wanawake waliandamana mjini Washington jana Jumamosi Januari 18, 2025, kulalamika dhidi ya kuapishwa kwa Rais mteule Donald Trump, na kutoa ujumbe wa kulinda haki zote za kiraia na kibinadamu.
Maandamano yaliyopewa jina la “People’s March” yalianza kutoka uwanja wa Franklin na kupita kati kati ya jiji la Washington hadi uwanja mkubwa mbele ya makumbusho ya Lincon.
Waandamanaji walikusanyika pamoja na kusikiliza hotuba kutoka viongozi wa asasi mbali mbali za kiraia kuhusiana na kulinda demokrasia, haki za wanawake hadi haki za uzazi na usawa wa kijinsia na haki za mashoga.
Akizungumza na Sauti ya Amerika, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Popular Democracy, Analilia Mejia, amesema maandamano hayo yana lengo la kuwaleta pamoja wanaharakati na waungaji mkono ili kuwakumbusha masuala muhimu ya demokrasia yanayokabiliwa na kitisho chini ya utawala mpya.
Anasema ujumbe muhimu ni kuhakikisha vita vinaendelea na mageuzi ya kweli yanapatikana baada ya vita vya muda mrefu.
Maandamano ya mwaka huu yakupinga kuapishwa kwa Trump yamekua madogo zaidi kuliko yale yaliyofanyika wakati wa awamu yake ya kwanza 2017, kwa sehemu fulani ni kutokana na vuguvugu la kutetea haki za wanawake Marekani limegawika baada ya Trump kumshinda makamu rais Kamala Harris mwezi Novemba.