Maendeleo ya mtoto na ukuaji wake-2

baby-psa2Naendelea na mada hii ambayo nimeianza wiki iliyopita.
Mtoto apewe fursa ya kucheza peke yake au na wenzake, apewe uhuru wa kucheza katika eneo kubwa na salama, apatiwe vitu vya kuchezea kama midoli, vigari, nk, apewe pia muda wa kucheza na wakubwa hasa na baba au mama au wengine ambao wapo karibu na mtoto bila kuwepo madhara.

Mtoto abadilishiwe mara kwa mara vifaa vya kuchezea na aongezewe tofautitofauti kwani husaidia kujenga akili ya mtoto kwa kasi. Vilevile mtoto afundishwe michezo mbalimbali.

MICHEZO YA WATOTO
Michezo ya watoto inasaidia kujenga afya na akili ya mtoto, pia inampa stadi za maisha. Mtoto ajifunze aina tofauti za michezo akiwa nyumbani au shuleni au katika vituo maalum vya michezo ya watoto. Kuna aina nne za michezo ya watoto;

‘Physical play’; Hii ni michezo ya viungo kwa ujumla, hufanya mwili uwe mwepesi na nguvu, misuli ya mwili wa mtoto hujengeka na kumfanya aonekane mwenye afya na nguvu.

Michezo hii ni kuruka, kukimbia, kupanda kwenye vifaa maalum kama ngazi au miti na kuogelea au kucheza mpira.

Manipulative play; Hii ni aina ya michezo inayomfanya mtoto atumie mikono na macho yake, mtoto hujifunza maumbo, rangi na aina ya vitu mbalimbali na kuvitambua.
Mtoto aachiwe achezee vitu vya asili kama mchanga, udongo, tope, maji na vitu ambavyo siyo hatari ili afurahi na kumjenga kiakili.

Creative play; Hii ni michezo ya ubunifu inayomjenga mtoto kiakili na kuwa mwerevu, mfano upakaji wa rangi, uchoraji, kutengeneza maumbo kwa kutumia karatasi, ushonaji, kuchezea goroli na vitu vingine vidogo vidogo.

Imaginative play; Hii inahusiana na mavazi na mazingira kwa ujumla kwa kuigiza kama baba kwa mtoto wa kiume na mama kwa mtoto wa kike, kuigiza kama mwalimu, daktari, fundi, askari, mtangazaji, dereva au katika sifa yoyote, mfano mchungaji, padri au shehe.

KUJIFUNZA LUGHA KWA MTOTO
Mtoto anaweza kujifunza lugha yoyote kirahisi toka kwa mzazi iwe Kingoni, Kichaga, Kimakonde, Kisukuma, Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, n.k. Tena mtoto ni mwepesi zaidi ikiwa mzazi muda mwingi atatumia kuongea naye au kuimba kwa lugha unayotaka mwanao aijue.

Iwapo mtoto ataanza kuongea lugha hiyo akikosea usimcheke, muone kama amepatia na endelea kuongea naye na atajisikia mwenye furaha.

MAENDELEO YA MTOTO KUFUATANA NA UMRI
Katika umri wa mwezi mmoja mtoto tunategemea anaweza kunyanyua kichwa akiwa amelala kitandani, anakuangalia unapoongea naye na mara nyingi hutabasamu.

Katika umri wa miezi mitatu hadi sita mtoto anaweza kugeuza kichwa upande wowote, anaweza kufuatilia kitu au mtu kwa macho na kuchezea vitu kwa mikono.

Umri wa miezi sita hadi tisa tunategemea mtoto anaweza kukaa chini mwenyewe bila kushikiliwa, anakuwa mwoga kwa vitu, watu au tukio la hatari kwake na akikasirika hulia kwa sauti kubwa.

Miezi tisa hadi kumi na mbili, tunategemea mtoto anaanza kusimama, anaelewa maneno machache na anaweza kuyatumia.

Umri wa miezi kumi na mbili hadi miezi kumi na nane tunategemea mtoto anaanza kutembea na kuchezea vitu mbalimbali vya ndani na hata kuviharibu.
Katika umri wa miaka miwili mtoto anakimbia huku na kule, anazungumza maneno mengi na kuyaunganisha.

Katika umri wa miaka mitatu, mtoto anacheza kwa bidii, anapanda juu ya vitu, anakimbia, anakuwa mjanja, anaongea sana na kuuliza sana maswali, hupenda kujua watu na vitu mbalimbali, anapenda asikilizwe yeye tu anapoongea na wakati mwingine huingilia mazungumzo ya wakubwa.

USHAURI
Kama mtoto yupo kinyume cha maelezo yote tuliyoyatoa, basi atakuwa na matatizo kwa hiyo muone daktari wa watoto katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi wa kina.


Loading...

Toa comment