The House of Favourite Newspapers

Mafanikio ya Keisha: Amber Lulu, Gigy, Nandy Someni Hii!

Khadija Shabani Taya ‘Keisha’

PONGEZI ziende kwa Khadija Shabani Taya ‘Keisha’, ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa (NEC), kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni hatua kubwa kwake na dhahiri hatua hii inaonesha wazi anazidi kuchuma matunda kutokana na mapambano yake kwenye ulimwengu wa siasa.

Kinachonivutia zaidi kutoka kwake ni kauli aliyowahi kuisema kwamba, anajikubali ni mlemavu wa ngozi, anajipenda, anajiheshimu na kujiamini, zaidi siku zote atapigania amani na haki ambayo wanastahili kuipata walemavu kama yeye!

Ni miongoni mwa wanamuziki wenye mchango mkubwa kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva, amekuwepo kwenye kabla ya wakali wengi unaowafahamu na amedumu kwenye gemu kuliko wakongwe wengi pengine unaowapenda.

Miongoni mwa ngoma kali zilizomtambulisha vyema kwenye gemu ni pamoja na Wimbo wa Uvumilivu aliofanya na Squeezer, Hamu aliofanya na Marlow pamoja na Nalia aliomshirikisha mkali wa michano toka pande za Rock City (Mwanza), Fareed Kubanda ‘Fiq Q.’

Unapomzungumzia Keisha, bila shaka utamzungumzia sambamba na wanamuziki wengine wakongwe wa kike akiwemo Lady Jay Dee, Vick Kamata, Dataz, Pauline Nzongo, Ray C na wengine waliokuwa wanakimbiza wakati huo. Lakini pia sifa zake hizi hazitasahaulika kwenye gemu la muziki wa Kibongo!

Malkia wa TipTop Connection

Keisha ana mchango mkubwa kwenye Kundi la TipTop Connection. Zaidi ni mwanamke wa pekee ‘malkia’ aliyeanza nalo tangu linastawi enzi zile linaogozwa na Abdul Bonge (marehemu) mpaka utawala wa Babu Tale.

Miongoni mwa kazi nzuri alizofanya kundini hapo aliweka mchango mkubwa kwenye Wimbo wa Tunapanda.

Wanamuziki akiwemo Kassim Mganga, Spack, Dogo Janja na wengine wengi walimkuta kundini hapo akikinukisha, kamwe Keisha hawezi kukosea kuita maskani ya TipTop, pale Manzese kwamba ni nyumbani kwake.

Ni kiunganishi cha muziki

Keisha akitoka kwenye kizazi cha kina Pauline Nzongo, Zey B, Vick Kamata na wengine wengi wa miaka hiyo ya mwanzoni au katikati mwa mwaka 2000, ameweza kuunganisha muziki kutoka kizazi hicho na kizazi cha sasa.

Aliweza kufanya kazi kali na mwanamuziki Diamond Platnumz kupitia Wimbo wa Nimechoka ambao hakika ulikuwa ‘hit song’ wakati unatoka!

Ni mkali wa ngoma za mahaba

Mwanamama huyu mwenye watoto watatu ni mkali kwenye suala zima la nyimbo za mahaba. Ingawa ngoma zake nyingi amekuwa akilia kulizwa na mapenzi lakini zina ujumbe mzuri katika ulimwengu huo kwa wanaoumizwa, kuteswa na mapenzi na hata wanaopenda kwa dhati.

Kumbuka nyimbo zake za Nalia, Nimechoka, Uvumilivu, Hamu aliofanya na Marlow, Huruma aliomshirikisha Bushoke na nyingine nyingi. Hakika utakubaliana nami kwamba yupo vizuri kwenye upande wa nyimbo za mahaba.

Si mtu wa skendo

Inawezekana kuna wanamuziki wakawa wanajiuliza inawezekana kweli kuwa maarufu bila kuwa na skendo! Keisha ana majibu ya swali hilo. Hilo ni jambo linalowezekana kabisa, kama yeye ameweza kudumu kwenye gemu na kupata heshima aliyonayo bila kuwa na skendo za ‘kipuuzi’ kama walizonazo wanamuziki wengi wa kike kwa sasa, basi kila mmoja anaweza.

Katika hili wanamuziki kama Lulu Diva, Amber Lulu, Gigy Money, Shilole, Nandy na wengine wengi wanatengeneza kiki kiasi cha kuvuka maadili wanaweza kujifunza kutoka kwake.

Kwamba muziki unategemea zaidi kazi nzuri na si kiki. Ni kweli unaweza kupushi muziki kwa kiki. Lakini kumbuka kiki inapita, kama muziki siyo mzuri basi, kiki ikiondoka na muziki wako unaondoka.

Lakini jambo lingine ambao kina Nandy inabidi wajifunze kwa Keisha, pengine kufika kwake mbali katika ulimwengu wa siasa, pamoja na sifa nyingine nyingi alizonazo, kujiheshimu na kulinda utamaduni wa Kitanzania vimezidi kumuongezea nafasi ya kuchana mawingu.

Ana elimu

Wakati fulani Keisha alipopotea kwenye gemu, aliulizwa na vyombo vya habari yakiwemo Magazeti ya Global Publishers juu ya nini kimempoteza. Unajua alijibu nini? Kwamba ni masomo. Keisha alisema yupo ‘busy’ na masomo na alikuwa akimalizia ‘bachelor’ katika kozi ya’ Procurement & Supplies Management’ katika Chuo cha Biashara cha CBE (Collage Of Business Education).

BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.