The House of Favourite Newspapers

MAFANIKIO YA KITUO CHA UWEKEZAJI KIPINDI CHA JPM

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeeleza mafanikio kiliyopata kuanzia Novemba, 2015 hadi Septemba, 2019 katika kipindi cha utawala wa Rais Dk John Pombe Magufuli. Katika kipindi hicho, TIC kimepata mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake. Mafanikio hayo yanatokana na jitihada na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyojikita katika kutekeleza mikakati ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.

Baadhi ya mafanikio hayo ni uboreshaji wa mfumo wa huduma za mahali pamoja katika kituo cha uwekezaji, ambapo taasisi zinazofanya kazi zimeongezeka kutoka nne hadi 11 na uboreshaji wa utoaji huduma kwa vibali vya kazi, cheti cha uwekezaji na ukaazi.

Mafanikio mengine ni pamoja na kuandikishwa kwa baadhi ya miradi mikubwa kama KEDA (Twyford) katika Kijiji cha Pingo, Chalinze mkoani Pwani. Pia kumekuwa na ongezeko la Watanzania kuwekeza kwenye sekta ya usafirishaji wa malighafi zinazohitajika na viwanda pamoja na kusafirisha bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivi kwenda
kwenye mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi kama vile Kenya, Burundi, Congo
na Zambia.

Kutokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga misingi imara ya mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, Serikali imefanikiwa kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali za uchumi.  Uwekezaji huo umeweza kuleta manufaa makubwa kwa Serikali pamoja na wananchi kiujumla.

 

Na Neema Adrian

Comments are closed.