The House of Favourite Newspapers

Mafia Simba Aichambua Yanga

0

JOTO la mtanange wa watani wa jadi Simba na Yanga limeanza kushika kasi baada ya mtathimini ubora wa Simba, Culvin Mavhunga kuanza kuwasoma wapinzani wao Yanga kwenye mchezo ambao Yanga ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Azam.

 

Simba na Yanga zitakutana Mei 8, ambapo mchezo wa kwanza uliopigwa Novemba 7 mwaka jana, ulimalizika kwa timu hizo kutoa sare ya bao 1-1 bao la Yanga likifungwa na Michael Sarpong huku lile la Simba likifungwa na Joash Onyango.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, Mavhunga ambaye alikuwa miongoni mwa mashuhuda waliojitokeza kwenye dimba la Mkapa kutazama mchezo kati ya Azam na Yanga akionekana kuwa amekwenda kufanya kazi maalum, alisema: “Yanga ni timu kubwa lakini haichezi kama timu kubwa kwenye baadhi ya mechi zao wamekuwa hawana muunganiko mzuri kwenye maeneo mengi.

 

“Wamekuwa na mawasiliano hafifu hasa kwenye eneo la kiungo na eneo la ushambuliaji jambo ambalo limesababisha wanafanya makosa mengi ya kiufundi.“Kwenye eneo la ulinzi wamekuwa bora kwa baadhi ya mechi licha ya kuruhusu mabao ya aina moja kwenye mechi tatu za mwisho ambazo wamecheza.”

 

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Mei 8 kwenye dimba la Mkapa jijini Dar, huku Simba wakiwa na mwenendo bora wakifanikiwa kuwashusha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara Yanga ambao wameongoza kwa kipindi kirefu.

 

Kabla ya mechi ya Simba ya jana dhidi ya Dodoma Jiji, Simba walikuwa kileleni na pointi 58 huku Yanga wakifuata na 57 na Azam wakiwa na 54.

Stori: Hussein Msoleka na Marco Mzumbe

Leave A Reply