Mafunzo ya Usalama Barabarani kwa Wanafunzi yahitimishwa, Washindi Wapewa Zawadi
‘VIA CREATIVE’, program ya usalama barabarani inayolenga kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule za msingi, imeadhimishwa kwa kuwazawadia washiriki kwenye tafrija iliyofanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii.
Tukio hilo la kuhitimisha mafunzo na kutoa zawadi limefanyika katika Ofisi Kuu za Total Energies, likivuta umakini wa wadau mbalimbali na kuhudhuriwa na Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Usalama Barabarani nchini Tanzania, ACP Michael Deleli, kama mgeni rasmi.
‘VIA CREATIVE’, programu inayolenga kuwaelimisha vijana kuhusu usalama barabarani, imewashirikisha wanafunzi wa shule za msingi katika mafunzo yanayowapa nafasi ya kutoa mawazo yao kupitia uchoraji wa picha.
Picha hizi zinawasilisha ujumbe muhimu wa kuzuia ajali za barabarani kwa wanafunzi wenzao na jamii kwa ujumla.
Mpango huu umewezekana kupitia ushirikiano kati ya Total Energies Foundation, Total Energies Marketing Tanzania Limited, East African Crude Oil Pipeline (EACOP), na Nafasi Art Space, mshirika aliyetoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi kupitia sanaa, michezo, na muziki.
Akitoa hotuba yake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Total Energies Marketing Tanzania Limited, Bw. Ellon Kamau alisema, “Tunajivunia sana leo wanafunzi wetu wanatunukiwa kwa sanaa kubwa waliyoitengeneza na ujumbe waliouwasilisha kuhusu usalama barabarani.
Tunaamini wanafunzi hawa sasa ni mabalozi wazuri wa usalama barabarani na watawaelimisha wanafunzi wenzao kuwa makini barabarani na kufuata sheria na taratibu zote za usalama barabarani.”
Hii ni toleo la pili la programu ya VIA Creative; toleo la kwanza lilifanyika mwaka 2022 kwa ushirikiano na Nafasi Art Space na lilifanikiwa kuwafikia zaidi ya wanafunzi elfu kumi katika shule 51 za msingi hapa Dar es Salaam.
Mwaka huu, VIA CREATIVE ilishirikiana kwa ukaribu na Idara ya Polisi ya Usalama Barabarani, kutoa mafunzo kwa walimu 90, wasanii 12, na kuelimisha wanafunzi zaidi ya 6000 katika shule 29 jijini Dar es Salaam na shule 20 Bagamoyo.
Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Usalama Barabarani nchini Tanzania, ACP Michael Deleli, alipongeza juhudi zilizofanywa na Total Energies kwa kushirikiana na EACOP na Nafasi Art Space katika kutoa mafunzo na stadi za usalama barabarani kwa wanafunzi.
Alisema, “Tunashukuru kushirikiana vyema na wadau binafsi kama nyinyi katika kuwaelimisha wanafunzi wa shule za msingi, ambao kwa kiasi kikubwa ndio waathirika wa ajali za barabarani, katika kutoa elimu ya usalama barabarani. Mmeonyesha ubunifu mkubwa wa kutumia sanaa, muziki, na ngoma, kitu ambacho kitabakia akilini mwa wanafunzi hawa.”
Kilele cha tukio hilo kilihusisha utoaji wa tuzo kwa shule tatu zilizoibuka washindi katika mashindano haya. Shule iliyoshika nafasi ya kwanza ilikuwa ni Shule ya Msingi Makuburi, wakijishindia zawadi ya Tshs 200,000/-.
Shule ya Msingi Mji Mwema ilishika nafasi ya pili, wakipokea zawadi ya Tshs 150,000/-, wakati Shule ya Msingi Kizuiani ilichukua nafasi ya tatu, na zawadi ya Tshs 100,000/-. Kila shule iliyoshinda ilipokea kikombe, vyeti, na vifaa vya uchoraji kama ishara ya shukrani kwa juhudi zao za kukuza usalama barabarani.
VIA CREATIVE inaendelea kujitolea kujenga utamaduni wa usalama miongoni mwa kizazi kipya na inatoa shukrani kwa washirika wote, washiriki, na wafadhili wote waliochangia kwa mafanikio ya program hii ya kuelimisha.