The House of Favourite Newspapers

MAGONJWA MA-4 HATARI KWA MAMA MJAMZITO

UJAUZITO mara nyingi huchangia mabadiliko mbalimbali ya mwili tangu mwezi wa kwanza hadi wa tisa mwanamke anapojifungua. 

 

Katika kipindi chote cha kulea mimba, mwanamke hukumbana na matatizo mbalimbali ya kiafya yanayotokana na mabadiliko hayo.

 

Katika kipindi hiki, ujazo wa damu huongezeka mwilini, japo pia hutokea kwa wachache kupungua, kiwambo cha mbavu hutanuka na mabadiliko yanayotokea kwenye mfumo wa homoni hutokea na husababisha pia matatizo mbalimbali kiafya japo baadhi huwa ya kawaida.

 

Lakini hayatakiwi kufumbiwa macho, ni vyema kwa mjamzito kuwa karibu na upatikanaji wa huduma za afya badala ya kusubiri hadi siku ya kuhudhuria kliniki au muda wa kukaribia kujifungua.

 

Kuhudhuria hospitali mara kwa mara kunasaidia kugundua mapema dalili inayoashiria tatizo linaloweza kumuathiri mama na mtoto tumboni. Haya ni baadhi ya matatizo yanayojitokeza kwa mjamzito na namna ya kukabiliana nayo:

SHINIKIZO LA DAMU

Kitaalamu linaitwa “preeclampsia”. Hili ni shinikizo la juu la damu linalotokea ghafla kwenye wiki ya 20 ya ujauzito. Hali hii ikidumu kwa siku chache inaweza kusababisha kufeli kwa figo, kutetemeka mara kwa mara hata kama hakuna baridi, kutengeneza jeraha kwenye ini, kusababisha matatizo mengine kwenye mfumo wa upumuaji, hivyo kuhatarisha maisha ya mjamzito.

 

Ukiona dalili hizo unashauriwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta na fanya mazoezi madogomadogo ya mwili kwa kipindi cha miezi mitano na kuendelea ili kujiepusha na shinikizo la juu la damu linalojitokeza katika kipindi hicho. Ni vyema pia kuhudhuria hospitali mara kwa mara kupatiwa vipimo vya shinikizo la damu.

KISUKARI CHA MIMBA

Kisukari cha mimba huwapata karibu asilimia 15 ya wajawazito wote kutokana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni.

 

Hali hii hutokea wakati plasenta, sehemu ya pembeni ndani ya mfuko wa uzazi inayosaidia kupitisha chakula na mahitaji mengine kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ikishirikiana na mrija wa kitovu, kuzalisha homoni nyingi zinazozuia kichocheo cha insulini kuratibu kiwango cha sukari mwilini.

 

Kwa kawaida, insulini hufanya kazi ya kurekebisha kiwango cha sukari inayoingia mwilini mwa mjamzito, ikizidi inaweza kumuathiri mtoto aliyeko tumboni. Mwanamke anashauriwa kutokula vyakula vilivyosindikwa na vyenye sukari nyingi wakati wa ujauzito, afanye mazoezi ya mara kwa mara na apate vipimo vya sukari angalau kwa mwezi mara moja kuanzia miezi mitatu ya ujauzito wake.

MAUMIVU YA MGONGO

Tatizo la maumivu ya mgongo na kiuno linawapata takribani wanawake wote katika vipindi tofautitofauti. Wajawazito wengi hupata maumivu ya mgongo na kiuno mimba inapokuwa na umri wa miezi sita. Kwa baadhi yao tatizo hili huwaletea shida na kuwanyima uwezo wa kufanya shughuli nyingine.

 

Hii ni kawaida kutokana na mabadiliko ya mwili na maumbile yanayotokea siku hadi siku wakati wa ujauzito. Mjamzito anashauriwa kupata muda mrefu wa kupumzika na anaweza pia kutumia dawa za kutuliza maumivu lakini ni lazima matumizi ya dawa hizo yaambatane na ushauri wa daktari. Wajawazito wengi hupendelea kula vyakula ambavyo mtu mwenye afya ya kawaida hawezi kuvila.

ULAJI WA UDONGO

Ulaji wa udongo, vitu vyenye asidi na ukakasi. Tabia hii inawaweka hatarini kupata ugonjwa unaoitwa ‘Pica.’

Ni ugonjwa ambao wengi hawaufahamu. Pica unatokana na ulaji wa vitu ambavyo havipo kwenye kundi la chakula anachopaswa mtu kukila. Wajawazito wanashauriwa kuacha tabia ya kuvila vitu hivyo kwani vinaathari. Waepukane na vitu hivyo ili kuepuka maradhi yanayoweza kuathiri mfumo wa chakula wa mjamzito na hata kuzaa mtoto njiti.

MAJERUHI WA AZAM HOI KITANDANI AZUNGUMZA – VIDEO

Comments are closed.