The House of Favourite Newspapers

MAGONJWA YANAYOSABABISHWA NA MAZIWA

IKIWA unahisi kichefuchefu, tumbo linasokota, linafura, lina gesi, au unaharisha baada ya kunywa maziwa au kula vyakula vinavyotengenezwa na maziwa, elewa kuwa una ugonjwa unaosababishwa na maziwa kitaalamu huitwa lactose intolerance.  Mtoto mchanga akiathiriwa na maziwa na kukutwa na dalili hizo hapo juu, yeye pamoja na wazazi wake wanaweza kutatizika sana. Mtoto akianza kuharisha, anaweza kuishiwa maji mwilini. Iwapo itagunduliwa kwamba anaathiriwa na maziwa, iwe ya mama, ya ng’ombe au ya unga, madaktari hupendekeza apewe vyakula vingine badala ya maziwa. Wengi wamepata nafuu baada ya kufuata mapendekezo hayo.

Ugonjwa huo huwapata baadhi ya watu na watoto wanapotumia maziwa na bidhaa za maziwa. Kulingana na kitabu The Sensitive Gut, kilichochapishwa na Shule ya Kitiba ya Harvard, imekadiriwa kwamba karibu asilimia 70 ya watu ulimwenguni huathiriwa kiafya na maziwa.

Laktosi ni sukari inayopatikana katika maziwa. Utumbo mdogo hutoa kimeng’enya kinachoitwa lactase, ambacho huvunja laktosi ili iwe glukosi na galactose. Sasa damu inaweza kuitumia sukari hiyo. Lakini ikiwa hakuna kimeng’enya cha kutosha, laktosi huingia katika utumbo mkubwa bila kuvunjwa kisha huanza kuchacha na kutokeza asidi na gesi. Dalili za ugonjwa ni kufura kwa tumbo, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula na kutapika.

Kimeng’enya cha lactase hutengenezwa kwa wingi mtu anapokuwa mtoto wa miaka miwili, kisha baada ya hapo huanza kupungua. Watu wengi hufikiri kwamba wana mzio wa maziwa wanapougua magonjwa yanayosababishwa na maziwa.

Kwa ujumla, mizio ya chakula si mingi, na ni asilimia moja mpaka mbili ambao huathiriwa. Watoto wengi zaidi huathiriwa ingawa hawazidi asilimia nane. Dalili za mizio na za magonjwa ya maziwa zinaweza kufanana, lakini kuna tofauti chache. Mzio hutokea wakati mwili unapokuwa ukijikinga na kitu kibaya ambacho umekula au kunywa. Mwili hutokeza kemikali inayoitwa histamine.

Dalili nyingine za mzio zinaweza kuwa kufura mdomo au ulimi, vipele, au pumu. Dalili hizo hazitokei mtu anapougua ugonjwa unaosababishwa na maziwa kwa sababu kinga ya mwili haihusiki. Badala yake mtu huwa mgonjwa kwa sababu tumbo hushindwa kusaga chakula vizuri.

Lakini ikiwa ana mzio, kuna sababu ya kuhangaika. Madaktari wengine huwapa dawa ya kuzuia histamine. Hata hivyo, ikiwa anashindwa kupumua, daktari atahitaji kufanya mengi zaidi ili kuzuia hali hiyo. Mtoto akianza kutapika, huenda ana ugonjwa mwingine unaoitwa galactosemia ambao hutokea mara chache. Kama tulivyotaja mapema, lactase hutokeza sukari ya galactose,ambayo pia huhitaji hubadilishwa iwe glukosi.

Sukari ya galactose ikirundamana mwilini, inaweza kuharibu ini, figo, kupungukiwa na akili, kupata ugonjwa wa hypoglycemia, na hata mtoto wa jicho (cataract). Hivyo ni muhimu kuacha kabisa kumpa mtoto maziwa au bidhaa za maziwa mapema ikiwa ataonyesha dalili tajwa hapo juu.

Kwa sasa hakuna matibabu yanayoweza kumsaidia mgonjwa atokomeze kimeng’enya cha lactase. Hata hivyo, kwa kawaida magonjwa yanayosababishwa na maziwa hayasababishi kifo.

MATIBABU NA KINGA

Wengine wameamua kutotumia bidhaa za maziwa hata kidogo baada ya kuona matatizo wakiyatumia.

Wale wanaotaka kuendelea kutumia bidhaa za maziwa wanaweza kwenda kwa daktari na akawaandikia dawa ambazo zina lactase ili kusaidia matumbo kuvunjavunja laktosi. Dawa hizo zinaweza kumsaidia mtu asiathiriwe na maziwa. Kwa ushauri wasiliana na daktari kwa namba ya simu hiyo hapo, ushauri ni bure.

Comments are closed.