The House of Favourite Newspapers

Magonjwa yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases)

0

Magonjwa haya kwa kifupi huitwa ‘NCD’s’. Haya ni magonjwa sugu ambayo humuathiri mtu kwa kipindi kirefu na kadiri siku zinavyoendelea na ugonjwa huendelea mwilini taratibu.
Wakati mwingine magonjwa haya yasiyoambukiza husababisha vifo mapema na kwa haraka yaani tangu mtu anapoanza kuugua kabla hajakamilisha vipimo au dozi aliyopangiwa hufariki.

Baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza ni kama vile matatizo ya mfumo wa kinga mwilini ambayo ni magonjwa ya moyo, kiharusi, kansa au saratani, kisukari, magonjwa sugu ya figo, magonjwa ya mifupa, kupoteza kumbukumbu na kutetemeka mwili ambalo ni tatizo la ubongo na huwapata  wazee, magonjwa yanayopunguza uwezo wa macho na mengine mengi.

Tunaposema magonjwa yasiyoambukiza maana yake hayatoki kwa mtu na kwenda kwa mtu na yanakuwa kwa muda mrefu hivyo tunasema ni  sugu. Pia yapo maambukizi ambayo ni sugu, mfano Ukimwi, ambayo hatuongelei katika hii makala yetu.
Magonjwa sugu hata matibabu huchukua muda mrefu ambapo kitaalam tunaita ‘Chronic Care Management’. Ni magonjwa ambayo huanza taratibu na hukaa muda mrefu ambapo mgonjwa hupata nafuu ya muda na wakati mwingine unalipuka tena.
Pia ni magonjwa ambayo aidha huchukua muda mrefu hadi kuona au hayaponi. Ni magonjwa ambayo huwa na mahudhurio makubwa katika kliniki za hospitali kubwa na hutibiwa na madaktari bingwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani ‘WHO’, mwaka 2012 magonjwa haya yasiyoambukiza yaliongoza kwa kusababisha vifo vya watu wengi duniani. Inaonesha kwamba, nusu ya waliofariki wana umri wa chini ya miaka sabini.

NANI YUPO HATARINI KUPATA MARADHI HAYA?
Watu ambao wapo hatarini kupata magonjwa yasiyoambukiza ni wale ambapo wapo kwenye familia zenye historia ya magonjwa hayo, utaratibu wa maisha mtu anayoishi inaweza kuwa chanzo, hali ya mazingira mfano uchafuzi wa mazingira hasa kemikali za viwandani zinaweza kuwa chanzo.
Uvutaji wa sigara pia ni chanzo kikubwa na takwimu zinaonesha kila mwaka takriban watu milioni tano hufariki kutokana na madhara ya tumbaku duniani kote.

Katika suala la mfumo wa maisha, watu wenye uzito mkubwa hufariki kutokana na maradhi yanayoambatana na uzito mkubwa na takriban watu milioni mbili na laki nane hufariki duniani kwa tatizo hili la ubonge. Tutakuja kuona madhara ya uzito mkubwa katika makala zetu zijazo.
Magonjwa haya yasiyoambukiza pia hutegemea umri wa mtu, jinsia na vinasaba na uchafuzi wa mazingira. Vilevile tabia inachangia sana mtu kupata maradhi haya.

Mfano uvutaji wa sigara, kutokula chakula bora au kula vyakula vinavyonenepesha sana mwili na kutofanya mazoezi ya mwili halijalishi hata kama wewe ni mwembamba ni vema ufanye mazoezi.
Kutofanya mazoezi na mlo usio wa afya kunaweza kukufanya uwe na kitambi na shinikizo la juu la damu. Hali hii itasababisha uandamwe na magonjwa mengi yasiyoambukiza.
Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply