The House of Favourite Newspapers

Magufuli  amaliza amaliza bifu la Kiba, Diamond

0

kd1Manguli wawili wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Ikiwa imebaki siku moja kabla ya uchaguzi mkuu, hatimaye mgombea wa nafasi ya urais kwa leseni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli amemaliza yale mabifu sugu kati ya manguli wawili wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na lile la Wema Isaac Sepetu na Aunt Ezekiel, Ijumaa linaweza kuripoti.

KIBA NA DIAMOND

Uchunguzi wa gazeti hili ambalo limeambatana na Magufuli takriban mikoa yote ya Tanzania kwenye kampeni zake umeonesha wazi kuwa kwa sasa Kiba na Diamond wamezika tofauti zao.

Katika kuzunguka sehemu mbalimbali mikoani kwa ajili ya Magufuli, jamaa hao walikutana mara kadhaa na kuchangamkiana huku watu wakiwatania na kujikuta wakiishia kucheka.

KOLABO YA KIBA NA DIAMOND

Kwa mujibu wa Team Magufuli, watahakikisha wawili hao wanafanya kolabo hivi karibuni mara tu baada ya pilikapilika za uchaguzi kumalizika.

“Unajua mheshimiwa amefanikiwa kuwakutanisha mara nyingi sehemu mbalimbali mikoani na wote amezungumza nao juu ya kutaka kuwaona wakifanya kazi pamoja.

“Alichowasisitizia mheshimiwa ni kuona wasanii wanakuwa na umoja na kwamba atawaunganisha wote bila kujali tofauti zao ilimradi wawe kitu kimoja.

Magufuli akiwamwaga sera kwa wakazi wa nkome Geita VijijiniMgombea wa nafasi ya urais kwa leseni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli.

SASA MAMBO FRESHI

“Mheshimiwa yeye hajali wasanii wa CCM pekee, amesema hata wale wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) atawasaidia bila kujali itikadi ya vyama hata kama hawakumuunga mkono,” alisema mmoja wa Team Magufuli anayeshughulika na ratiba za wasanii kwenye kampeni na kuongeza:

“Hata wakati wa kusaini mikataba ya shoo walikuwa wanakutana mara kwa mara na kupeana tano kuonesha kwamba sasa mambo ya bifu yamekwisha.”

MSIKIE KIBA

Akizungumzia bifu lake la muda mrefu na Diamond, Kiba alifunguka: “Mimi sioni faida ya mabifu na mashabiki ndiyo wanakua mambo.”

HUYU HAPA DIAMOND

Kwa upande wake Diamond aliliambia Ijumaa kuwa, kwa sasa hana bifu lolote na jamaa huyo na kwamba mheshimiwa amewasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuufikisha muziki wa Bongo Fleva mbali na ikiwezekana duniani kote.

“Mheshimiwa ameahidi kutupiga tafu ili muziki wetu ufike mbali zaidi. Hayo mambo ya bifu yameshapitwa na wakati, sasa hivi ni kazi tu,” alisema Diamond.

MAKUNDI MITANDAO YA KIJAMII

Kufuatia hali iliyopo kwa sasa, hata yale makundi hasimu ya Team Kiba na Team Diamond yanaonekana kujirudi na kuwa kitu kimoja hasa lilipokuja suala la kumsapoti Magufuli ambapo imekuwa ni rahisi kwa kundi moja kuliunga mkono kundi lingine kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram, WhatsApp, Facebook na Twitter.

BIFU TANGU 2012

Kabla ya kumaliza tofauti zao, Kiba na Diamond wamekuwa kwenye bifu zito tangu mwaka 2012 ikielezwa ni ushindani katika muziki wao ambapo kila mmoja alikuwa akijiona yupo juu kuliko mwingine.

wemanadiamond (1)Wema na Diamond.

WEMA NA AUNT

Kwa upande wao, mashosti wawili ambao walikuwa wameshibana vilivyo kisha kuhitilafiana, Wema na Aunt, nao wamejikuta wakimaliza tofauti zao, kisa kumpigia kampeni Magufuli.

KISA DIAMOND

Awali, Aunt na Wema walikuwa hawaivi baada ya Aunt kuwa upande wa Diamond katika kipindi ambacho Wema alikuwa haivi na jamaa huyo ambaye alikuwa mwandani wake kabla ya kunasa kwenye penzi la mwanamama Zarinah Hassani ‘Zari The Boss Lady’.

Pia wakati kampeni zinaanza, Aunt alikuwa upande wa Ukawa, akiwa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akimuunga mkono Edward Lowassa hivyo bifu lake na Wema lilikuwa kama ndiyo limechochewa moto.

AUNT KUREJEA CCM

Lakini Aunt aliporejea CCM na kutangaza kumsapoti Magufuli ndipo Wema naye akarejesha urafiki wake na mwanadada huyo kwa msaada wa Team Magufuli.

Pamoja na kwamba kila mmoja alikuwa kitengo chake cha kampeni ambapo Wema alikuwa kwenye Kampeni ya Mama Ongea na Mwanao huku Aunt akiwa Nimestuka lakini bado walikuwa wakionesha ukaribu na ushosti wao kupitia mitandao ya kijamii.

AUNT ANASEMAJE?

Kuhusu kupatana na Wema, Aunt alifunguka: “Mambo ya bifu tupa kule hapa ni kazi tu!”

WEMA VIPI?

“Sina bifu na Aunt. Kwa sasa tunaweka nguvu zote kwenye ushindi wa Magufuli,” alisema Wema kwa kifupi.

WEMA NA DIAMOND

Duru za habari zilieleza kwamba ni kampeni hizihizi za Magufuli ambazo zimefanikisha kumaliza bifu la Wema na Diamond lililodumu kitambo tangu walipoachana mapema mwaka jana.

WEMA, DIAMOND URAFIKI UPYA

Wawili hao walifufua urafiki wao mapema wakati wa ufunguzi wa Kampeni za Magufuli kwenye Viwanja vya Jangwani jijini Dar ambapo inadaiwa walikutana nyuma ya jukwaa (back stage) na kuchangamkiana kisha kumaliza bifu lao na sasa kila wanapoonana ni kicheko tu.

Haikuwa kazi rahisi

Mmoja wa wadau wa muziki aliyekuwa kwenye kampeni za Magufuli anayedili na mastaa ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema: “Haikuwa rahisi kuwapatanisha mastaa hao ambao kila mmoja alikuwa akimpiga vita mwenzake na wanaomunga mkono.”

Leave A Reply