Magufuli amaliza kazi

magufuli (2)Na Richard Bukos, Pwani

MGOMBEA Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, (pichani) amemaliza kazi huku akitarajia kumwaga sera za mwisho katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam kabla ya kesho kuhitimisha fainali kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Magufuli, ambaye ameongeza kasi na kubadili mitazamo ya watu kadiri siku za kampeni zilivyokuwa zikisonga, anaelezwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kwamba kwa taswira iliyopo, ana alama nyingi za ushindi ikilinganishwa na wagombea wengine, hususan Mgombea wa Chadema, Edward Lowassa.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi gazeti hili lilipokuwa linakwenda mitamboni jana, Magufuli alikuwa ametembea umbali wa kilometa 44,467 katika majimbo 247 ndani ya mikoa 30, ambapo ametumia gari na boti wakati mgombea wa Chadema ametembea kilometa zisizozidi 3,000 kwa gari, ametembelea majimbo 137 yaliyo kwenye mikoa 25.

Aidha, takwimu zinaonesha kwamba, Magufuli amefanya mikutano rasmi 265 na mikutano midogo 908 ikilinganishwa na Lowassa ambaye amehutubia mikutano mikubwa 103 tu tangu kuanza kwa kampeni wakati ambapo idadi ya mikutano isiyo rasmi ambayo haipo kwenye ratiba ni michache mno kwa vile amekuwa akitumia helikopta, hivyo kukosa fursa ya kusalimiana na wananchi.

Takwimu hizo zinaonesha kwamba, Magufuli amehutubia kwa saa 311 ukiwa ni wastani wa dakika 45 kwa kila mkutano mkubwa wa hadhara, wakati Lowassa amehutubia kwa saa 26, sawa na dakika 8.93 kwa kila mkutano rasmi.

Rekodi zinaonesha kwamba, Dk. Magufuli anakadiriwa kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 12 ana kwa ana na takriban milioni 36 kwa njia za mawasiliano ya redio, magazeti, televisheni na mitandao ya kijamii, wakati mgombea wa Ukawa amewafikia wananchi wasiozidi milioni tano ana kwa ana katika mikutano ya hadhara michache aliyofanya na amewafikia wananchi wasiozidi milioni 11 kwa njia za televisheni, magazeti, redio na mitandao ya kijamii.

CCM ina wanachama wanaokadiriwa kufikia milioni 8 nchi nzima, wakati Ukawa wana wanachama milioni 4, na ikiwa wanachama wa

CCM wanaoamini katika Lowassa watampigia kura, chama hicho tawala kinaweza kupoteza kura 800,000 za wanachama wake, japokuwa historia inaonesha kwamba wanaCCM huwa wagumu kumchagua kada mwenzao pindi anapohama chama kama ilivyokuwa kwa Augustine Mrema mwaka 1995.

Aidha, wachambuzi wanasema, ikiwa wanachama wa Ukawa wanaoamini katika Profesa Ibrahim Lipumba, Dk. Wilbrod Slaa, Mchungaji Christopher Mtikila, Dk. Emmanuel Makaidi (marehemu) na Zitto Kabwe wataamua kuchagua uadilifu wa Magufuli, CCM inakadiriwa kuvuna kura milioni moja na nusu kutoka upinzani.

Wakati CCM itakamilisha kampeni zake kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Chadema (Ukawa) watakamilisha kampeni zao kwenye Viwanja vya Jangwani wakati ACTWazalendo watafunga kazi kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Loading...

Toa comment