The House of Favourite Newspapers

Magufuli: Pinda alinizuia kubomoa Jengo la Tanesco

0
Rais John Magufuli.

Rais John Magufuli amesema aliyekuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya nne, Mizengo Kayanda Pinda, alimzuia kubomoa jengo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopo Ubungo, wakati huo akiwa waziri wa ujenzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila leo, Rais Magufuli alisema mbele ya Pinda, aliyehudhuria hafla hiyo kuwa, alitii agizo hilo kwa vile aliogopa kufukuzwa kazi, lakini sasa akiwa rais, hana wa kumuogopa.

“Nilishatoa maagizo, najua Mizengo Pinda kwenye hili alinipinga wakati ule, lakini najua leo hawezi akanipinga kwa sababu mimi ndiye Rais. Wakati ule nilikuwa waziri wake, ndiyo maana nilinyamaza nilijua ninaweza nikafukuzwa, hutakiwi kumpinga mkubwa.

“Hilo jengo la Tanesco, narudia kama itakuwa ni kubomoa nusu, no problem (hakuna tatizo); kama ni lote hakuna tatizo, pamoja na jengo la wizara ya maji. Najua katibu mkuu wa wizara ya maji yupo hapa ananiangalia, wakaanze kulitoa eneo lililopo kwenye hifadhi ya barabara,” amesema.

Waziri Mkuu Pinda wakati huo, alimzuia Magufuli kuchukua hatua hiyo mwaka 2011 akisema ubomoaji huo utasitishwa hadi hapo serikali itakapotoa kauli nyingi juu ya suala hilo, kitu ambacho hakikuwahi kutokea hadi waziri huyo wa ujenzi aliposhinda na kuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania mwaka 2015.

Pinda alikuwa akizungumzia hatua ya Magufuli aliyekuwa amewaagiza wananchi waliojenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba hizo na wasitarajie kulipwa fidia.

Leave A Reply