Magufuli kaanika; kero nyingi hazikufanyiwa kazi

MUNGU ni mwema sana na anastahili kuabudiwa milele. Baada ya kusema hayo nianze kwa kuandika kuwa kutokana na hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa Bungeni mwishoni mwa wiki wakati anafungua Bunge la 11, ni wazi kuwa kero nyingi za wananchi katika serikali ya awamu ya nne hazikufanyiwa kazi.

Kwa mtazamo wangu, hotuba ya Rais Magufuli ilikuwa ni ya kuwakemea watendaji wa serikali ambao hawakuwa wakitimiza majukumu yao enzi za uongozi wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na mbaya zaidi walijikita katika ubadhirifu wa mali za umma na kufuja mali kwa njia mbalimbali.

Rais Magufuli hakuficha jambo, alieleza jinsi kalamu ilivyokuwa inanunuliwa kwa bei mbaya, safari za nje ya nchi zilivyokuwa zinafanywa na wakubwa zilivyotafuna fedha za umma na uzembe uliokithiri ulivyokuwa ukidhoofisha au pengine kusababisha vifo kwa wananchi.

Kwa mtu anayefikiri, hotuba ya Rais Magufuli ilikuwa na maana kubwa na ishara njema kwa taifa hili ambalo wanaofaidi keki ya taifa ni wachache sana.

Hotuba ile haipaswi kupuuzwa na kiongozi yeyote wa serikali. Unyeti na ukweli ulioelezwa na Rais Magufuli ni wa wazi na sina nafasi ya kuunukuu hapa.

Niseme tu kuwa viongozi wa serikali chini ya CCM kiliwasahau wanyonge kulingana na misingi yake asilia iliyopaswa kurithi kutoka Tanu na ASP enzi za waasisi wake, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Aliyoyasema rais yalionwa na wazee wetu, kwa mfano mzee Peter Kisumo (kwa upande wa Bara) na Mzee Hassani Nassoro Moyo (Kwa upande wa Zanzibar), nikitaja wachache lakini wakawa wanapuuzwa bila shaka kwa kuwa hawakuwa na madaraka.
Viongozi wengi wa serikali walisahau kuwa penye wazee hapaharibiki kitu. Haifai na si busara kupuuza wazee hao.

Sasa kila mmoja anaona na anakiri kwamba Dk. Magufuli ni mtu aliyefaa kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi uliopita na Watanzania walifanya uamuzi sahihi wa kumfanya rais wa nchi hii na tayari kasema hawezi kupuuza busara za wazee.
Naamini mabadiliko ya kweli yatapatikana katika nchi hii kutokana na dira aliyotuonesha Dk. Magufuli.

Matatizo yanayolikabili taifa hivi sasa yanatokana na watendaji wabovu serikalini kama Magufuli alivyoweka wazi bungeni.

Kutojiheshimu na kutowajibika kwa viongozi hao kwa wananchi kunaleta kutoheshimika kwa viongozi mbele ya jumuiya ya kimataifa na ni fedheha kwa wananchi wanaowaongoza.

Mwalimu Nyerere aliheshimika siyo tu kwa kuwa alikuwa mkali bali kwa kuwa aliheshimu wadhifa aliopewa kama dhamana na wananchi.

Katika kipindi chote cha uongozi wake siyo tu hakupata kutuhumiwa na rushwa bali pia hakuwa na chembe ya harufu ya rushwa au ufisadi kama alivyo Magufuli.

Kutokana na ubadhirifu mwingi serikalini ndiyo maana wananchi wanadai Katiba mpya siyo tu kwa kuwa katiba iliyopo ina upungufu mwingi bali pia haiwapi wananchi mamlaka ya kusimamia wabunge na serikali yao.

Ili kumpunguzia rais kazi, vipengele vya kuwawajibisha watendaji wabovu na wabunge wasiowakilisha wananchi, virejeshwe kwenye Katiba Mpya.

Baadhi ya viongozi serikalini hawajiheshimu na wanatuhumiwa kuhusika na rushwa na ufisadi, jambo ambalo Rais Magufuli ameliona na amewatahadharisha.
Rais tupo nyuma yako!


Loading...

Toa comment