The House of Favourite Newspapers

Magufuli: Niko fiti

0

MAGUFULI (3)Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli akipiga push up jukwaani.

Stori: Na Richard Bukos, Kagera

NIKO fiti! Ndivyo alivyosema mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli kuudhihirishia umma kwamba yupo fiti kimazoezi.

Tukio hilo lililoibua shangwe ya aina yake lilijiri juzi, Jumanne katika Viwanja vya Kayanga, Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera wakati Magufuli alipokuwa akiendelea na ziara zake za kampeni.

Mara baada ya kuwahutubia maelfu ya wakazi wa mkoa huo kwa kuwaeleza sera na ilani za chama chake, mgombea huyo ambaye amejijengea sifa ya ukakamavu kwa kupanda jukwaani kwa staili ya kukimbia mithili ya mwanariadha, aliwaambia wananchi wamchague yeye kwani yuko fiti.

“Msije mkachagua watu wenye afya mgogoro, wanaoshindwa kupanda jukwaani, wasiojua kuongea mpaka watembee na washenga wa kuwazungumzia…mgombea unatakiwa uwe fiti kama mimi.

MAGUFULI (2)“Hapa nilipo naweza hata kupiga push up , nipige nisipigi?” aliuliza Magufuli na kujibiwa piga na wananchi kisha akaanza kupiga.

Wakati akipiga push up, umati wa watu ambao ulifurika katika viwanjani hivyo ulisikika ukihesabu, moja…mbili..tatu na kuendelea huku wengine wakisema: “rais…rais…rais…rais..rais…”

Katika hotuba yake, Magufuli aliyekuwa akijinadi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa alisema wakulima wa kahawa waliopo eneo hilo atawafutia kodi mbalimbali ambazo zinamfanya mkulima asiambulie kitu baada ya kuuza.

Alisema katika kila kijiji cha wilaya hiyo ataanzisha mifuko ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukopesha wakazi wa eneo hilo huku akiahidi kutengeneza barabara ili kurahisisha usafiri katika mitaa yao.

Leave A Reply