Mahadhi aibuka, afungukia usajili wake Yanga SC

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Juma Mahadhi ameibuka na kudai kuwa yeye bado ni mchezaji wa Yanga na hivi karibuni atarejea kikosini kwa ajili ya kuipambania timu hake.

 

Nyota huyo hivi karibuni ilielezwa kuwa ameachwa na timu hiyo katika usajili huu wa Ligi Kuu Bara mara baada ya mkataba wake kumalizika.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mahadhi alisema kuwa matatizo ya majeraha ya goti ndiyo yamesababisha asionekane uwanjani.

 

Mahadhi alisema: “Ninapata maswali mengi kutoka kwa mashabiki wa Yanga wakiniulizia kuwa bado nipo Yanga au vipi.

 

“Ukweli ni kwamba mimi bado mchezaji wa Yanga ambaye nilisaini mkataba wa miaka miwili mara baada ya ule wa awali kumalizika.

“Hivi sasa nipo nje ya uwanja nikiuguza majeraha ya goti niliyoyapata kwenye msimu uliopita, hivyo bado sijapona na hivi karibuni nitaanza kuonekana uwanjani.

 

“Niwashukuru viongozi wangu kwa kufanikisha kunisafirisha nchini India kwa ajili ya matibabu yangu ya goti ambayo yanaendelea vizuri.”

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alizungumzia hilo kwa kusema kuwa ni kweli Mahadhi bado ni mchezaji halali wa Yanga mwenye mkataba wa miaka miwili aliousaini hivi karibuni.

WILBERT MOLANDI NA SAID ALLY, Dar


Loading...

Toa comment