The House of Favourite Newspapers

Mahakama Kuu ‘Yazipiga Pini’ Mali za Yusuf Manji

MAHAKAMA Kuu imezuia mali za mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuph Manji, kutokana na madeni anayodaiwa na Benki ya NBC.

 

Manji anadaiwa zaidi ya Sh25 bilioni na benki hiyo kwa kuwa ameshindwa kuzirejesha kwa wakati kwa mujibu wa mkataba, hivyo mali zake zilizopo Mwanza na Dar es Salaam ambazo ziliwekwa dhamana, zimezuiwa.

 

Mali hizo zimezuiwa kwa oda (amri) mbili tofauti za mahakama hiyo zilizotolewa Februari 19 mwaka huu zinazomzuia Manji kufanya muamala wa aina yoyote kuhusu mali hizo ikiwamo kuhamisha umiliki,kuzitoa kama zawadi, kuuza au kuweka dhamana.

 

Katika oda ya kwanza inayotokana na kesi ya biashara namba 54 ya mwaka 2018 inaizuia kampuni ya Manji Tanperch kufanya chochote kwenye kitalu namba 8, 9 na 127 vilivyopo eneo la viwanda Ilemela kwa jina la Tanperch Limited kwa kushindwa kulipa deni la Sh18.7 bilioni kutoka Benki ya NBC.

 

NBC ilifungua kesi mwaka 2016 ikizishtaki kampuni za Farm Equip (T) Limited, Tanperch Limited na Quality Group Limited zinazomilikiwa na Kaniz Manji na Yusuf Manji kwa kushindwa kurejesha Sh15.9 bilioni.

 

Desemba mwaka jana Jaji Butamo Philip aliwataka washtakiwa wote watano kulipa deni hilo ambalo lilikuwa limefika Sh18.7 bilioni linalojumuisha mkopo wa akaunti (overdraft) na wa kuingiza bidhaa nchini.

 

Kati ya washtakiwa hao, nyaraka za mahakama zinaonyesha Farm Equip ndiye mkopaji mkuu na wengine ni wadhamini. “Farm Tanperch inazuiliwa kuuza au kuhamisha umiliki kwa namna yoyote,” inasomeka sehemu ya oda.

Comments are closed.