The House of Favourite Newspapers

Mahakama ya ICC Yamwachia huru Gbagbo

Laurent Gbagbo

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), imemwachia huru rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.

 

Gbagbo alifikishwa mbele ya mahakama hiyo mwaka 2011 kutokana na vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao ulishuhudia akishindwa mbele ya mpinzani wake, Alassane Ouattara.

 

Katika uamuzi wao, majaji wa ICC, waliamuru Rais Gbagbo kuachiwa huru kwa kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka hata moja kati ya yale aliyoshitakiwa mbele ya mahakama hiyo.
Gbagbo alishitakiwa kwa madai ya kuhusika na vurugu zilizosababisha mauaji ya watu 3,000 huku wengine 500,000 wakiyakimbia makazi yao.

 

Kwa mujibu wa rekodi za ICC, Gbagbo ni kiongozi mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi kupandishwa mbele ya mahakama hiyo. Kukamatwa kwake kulitekelezwa na vikosi vilivyokuwa vikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN) na Ufaransa.

 

Mbali na Gbagbo, mke wake Simone Gbagbo, naye alitiwa hatiani na mahakama za nchi hiyo kwa kuhusika na makossa mbalimbali ikiwemo kuratibu makundi ya ujambazi.

 

Serikali ya Ivory Coast ilikataa kumkabidhi Simone kwa ICC ikisema itamshitaki na kumhukumu katika mahakama za ndani.

Alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makossa mbalimbali ikiwamo ya uvunjifu wa sheria za nchi, kuvuruga usalama wa nchi na makossa dhidi ya ubinadamu.
Simone alinufaika na msamaha wa Rais Ouattara mwaka jana ambaye alisema ameamua kumsamehe ili kufungua milango ya majadiliano na maridhiano kwa mustakbali wa taifa hilo linaloongoza kwa kilimo cha kakao duniani.

Comments are closed.