The House of Favourite Newspapers

Mahakama ya Kisutu Yaagiza ‘Pedeshee Ndama’ Akamatwe

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein maarufu ‘Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng’ombe’ baada ya kukiuka taratibu za dhamanana kutoa barua ya wito kwa wadhamini wa mshtakiwa huyo, kufika mahakamani.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Maira Kasonde, ametoa hati hiyo jana, Jumatano Oktoba 24, 2018, baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani hapo bila kutoa taarifa, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Kabla ya kutolewa kwa amri hiyo, Wakili wa Serikali, Mosia Kaima, amedai mahakamani hapo kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini mshtakiwa hayupo mahakamani na hawana taarifa yoyote kuhusiana na mshtakiwa huyo.

“Mheshimiwa Hakimu, kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini mshtakiwa hayupo mahakamani na upande wa mashtaka hatuna taarifa zozote,” amedai Kaima.

Baada ya Wakili Kaima kueleza hayo, Hakimu Kasonde ametoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo na kufikishwa mahakamani hapo.

“Mshtakiwa akamatwe na aletwe mahakamani ili ajieleze kwa nini asifutiwe dhamana yake kwa kukiuka masharti ya dhamana,” amesema Hakimu Kasonde

Hakimu Kasonde, baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hadi Novemba 12, 2018, itatajwa.
Ndama anakabiliwa na mashtaka matano yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, baada ya shtaka la sita ambalo ni la kutakatisha fedha, kulipa faini baada ya kukiri shtaka hilo.

MAGAZETI YA LEO

Comments are closed.