The House of Favourite Newspapers

Mahakama ya Kisutu Yatupilia mbali pingamizi la Mbowe na wenzake

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali pingamizi la viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  akiwemo Freeman Mbowe la kutaka kesi ya kufanya maandamano ifutwe badala yake imeagiza hati ya mashtaka ibadilishwe.

 

Kwa upande  wa utetezi kupitia wakili wake, Peter Kibatala, umetangaza nia ya kukata rufaa kupinga uamuzi huo  kwa sababu kama mahakama imeona mashtaka hayo ni batili kwanini isingeyafuta badala yake imeagiza yabadilishwe.

Uamuzi wa pingamizi hilo  umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ambapo amesema anakubaliana na hoja mbili za upande wa mashtaka kati ya hoja zao nane  za mapingamizi.

 

Katika kesi hiyo pingamizi kuu la upande wa utetezi wameiomba mahakama hiyo ifute kesi hiyo kwa sababu baadhi ya mashtaka ni batili.

 

Mashauri amesema hakuna haja ya kesi hiyo kufutwa badala yake anaagiza upande wa mashtaka uifanyie marekebisho hati ya mashtaka.

 

Upande wa mashtaka kupitia Wakili wa serikali Mkuu, Paul Kadushi umedai kuwa kwa mujibu wa sheria ya Mahakama za Mahakimu hakuna uwezekano wa kukata rufaa katika uamuzi mdogo ambao hauwezi kuathiri kesi.

 

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa kibamba John Mnyika, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime mjini Esterher Matiko, Katibu wa chama hicho Dk Vicenti Mashinji, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, mbunge wa Tarime vijijini, John Heche na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Juni 12, mwaka huu  ili kutoa uamuzi kama upande wa mashtaka ukate rufaa ama la.

Comments are closed.