The House of Favourite Newspapers

Ombi la Mbowe, Wenzake Lakataliwa Kortini

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya upande wa utetezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo mwenyekiti wake Freeman Mbowe juu ya kuanza kwa mashahidi wao kujitetea na badala yake wataanza kujitetea washtakiwa wenyewe.

 

Baada ya kutolewa uamuzi huo wakili wa utetezi, Peter Kibatala aliomba muda wa wiki tatu kwa ajili ya wateja wake kujiandaa kutoa utetezi huku akisema aliyekuwa tayari ni shahidi hivyo anaomba wateja wake wapewe muda wa kujiandaa.

 

Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili Faraja Nchimbi umepinga muda huo ukisema hakuna sababu ya mahakama kuwapa muda huo hivyo hakimu kutokana na kuibuka kwa hoja hizo ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21 mwaka huu atakapotoa uamuzi wa lini wataanza kujitetea.

 

Uamuzi huo umetokana na upande wa mashtaka kuwasilisha hoja nne mahakamani hapo kupinga utaratibu wa kusikiliza mashahidi kabla ya viongozi hao tisa wa Chadema kuanza kujitetea.

 

Ikumbukwe Oktoba 15, mwaka huu upande wa utetezi katika kesi hiyo uliomba kuanza kutoa ushahidi kwa kuanza na shahidi badala ya washtakiwa wenyewe.

 

Hoja za kupinga jambo hilo ziliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza utetezi.

 

Akitoa hoja hizo, Wakili Nchimbi alidai kuwa ombi la upande wa utetezi la kuanza kusikiliza mashahidi kabla ya washtakiwa wenyewe kutoa utetezi, halitekelezeki kwa sababu linakiuka sheria ya ushahidi na mwenendo wa mashauri ya jinai inayotoa mwongozo wa kuendesha na kusikiliza mashauri.

 

Alidai kifungu cha 144 cha Sheria ya Ushahidi sura ya 6 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kinazungumzia uongozaji wa mashahidi na kuongeza kuwa wanashawishi mahakama, utaratibu wa uwasilishaji mashahidi wakati wa utetezi unatamkwa na kifungu cha 231 (1) (a) na (b) pamoja na mambo mengine kinazungumzia haki na utaratibu wa kuwasilisha utetezi.

 

Alidai mshitakiwa hawezi kuingia kwenye haki ya kuita mashahidi kama yeye mwenyewe hajaamua au hajatoa ushahidi. Wakili Nchimbi aliiomba Mahakama ijielekeze pia katika kifungu cha 38 (2) (a) na (b) kwani utaratibu wa utoaji wa ushahidi wa utetezi mahakama inapaswa kumuita mshtakiwa kama ushahidi ili atoe utetezi wake.

 

Alidai washtakiwa wanavaa kofia mbili kwa wakati mmoja kwa sababu wanasimama kama washtakiwa na mashahidi kwa wakati mmoja.

 

Nchimbi alidai sheria inataka ushahidi unapotolewa mashahidi wengine wasiwepo wakati wa ushahidi na kwamba iwapo upande wa utetezi watapewa nafasi ya kusikiliza mashahidi kabla ya washtakiwa kujitetea, washtakiwa hawataruhusiwa kusikiliza kinachosemwa na mashahidi.

 

Alidai ushahidi unapotolewa ni lazima washtakiwa wawepo hivyo hawawezi kuwaondoa washtakiwa hao wakati ni sehemu ya shauri hilo.

 

Hata hivyo, aliomba mahakama itoe mwongozo utakaowataka washtakiwa hao kutoa utetezi wao kabla ya mashahidi. Wakili wa Utetezi Peter Kibatala alidai kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria za hapa nchini au nje ya Tanzania ambacho kinazuia washtakiwa kusikiliza mashahidi wake kisha mshtakiwa mwenyewe.

 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendajia jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Global Publishers (@globalpublishers) on

Comments are closed.